Kaimu Mkuu wa Kitengo cha
Mawasiliano na Hifadhi Hati Bi. Rose Mdami akikagua fomu ya Bwana
Kitomari baada ya kukamilisha hatua ya kwanza ya usajili Vitambulisho
vya Taifa kabla ya kwenda kwenye hatua ya upigaji picha. Hapa ni Kata ya
Makiba kituo cha CCM Arumeru Arusha ambako zoezi hilo linafanyika.
Hawa ni Watendaji katika
vitongoji viwili vya Kijiji cha Valeska wakiendelea na zoezi la
kuwahakiki wananchi wao na kuwathibitisha kuwa ni wakazi halali wa eneo
lao kabla ya kuwaidhinisha kupigwa picha na kuchukuliwa alama za vidole
wakati wa zoezi la Usajili linaloendelea Wilayani Arumeru.
Huu ni muonekano wa nje ya jengo
ambako usajili wa Vitambulisho vya Taifa unaendelea Kata yaMakiba kijiji
cha Valeska. Baadhi ya wananchi wakiwa wanabadilishana mawazo huku
wakisubiri kupatiwa huduma.
Afisa Usajili Wilaya ya Arumeru
ndugu Edward Bujune akitoa maelezo kwa wananchi kuhusu umuhimu na faida
za Vitambulisho vya Taifa wakati zoezi la kuwasajili wananchi wa Wilaya
ya Arumeru likiendelea.
Meneja Mifumo ya Komputa ndugu
Mohamed Mashaka akirekebisha moja ya Kamera ili iweze kufanya kazi kwa
ufanisi zaidi wakati wa ziara ya kukagua utekelezaji wa zoezi la Usajili
Wilayani Arumeru.
Meneja Uthibiti na Usambazaji
ndugu George Mwandezi aliyeshika Kitambulisho akitoa elimu kwa wananchi
kuhusu ubora wa Vitambulisho vya Taifa wakati wakiendelea na zoezi la
Usajili Kata ya Makiba wakati viongozi hao walipofanya ziara kukagua
maendeleo ya zoezi linaloendelea sasa katika Kata hiyo.
Mtendaji katika Kijiji cha
Valeska Kata ya Makiba akihakiki fomu za wananchi kabla ya kuingia
kwenye chumba cha uchukuaji alama za vidole, picha na saini ya
kielektroniki. Fomu hizo zimekuwa zikusanywa na kupitiwa iwapo
zimekamilika kujazwa vipengele vyote 72 vinavyohitajika
Hawa ni baadhi tu ya wananchi
katika kijiji cha Valeska wakiwa kwenye foleni ya picha na uchukuaji
alama za kibaiolojia wakati zoezi la Usajili likiendelea kijini hapo.
……………………………………………………………………….
Katika hali isiyokuwa ya kawaida,
wananchi katika Wilaya ya Arumeru Kata ya Makiba kijiji cha Valeska
mkoani Arusha; wameonyesha kuelewa umuhimu wa Vitambulisho vya Taifa
kiasi cha kujiwekea mkakati wa kuhakikisha nishati ya umeme muda wote
inakuwepo ili zoezi la Usajili linaloendelea kutosimama.
Pengine hii ni tofauti na mazoea
ya siku zote katika uendeshaji wa zoezi la Usajili na Utambuzi wa Watu
kwa maeneo ambayo zoezi kama hilo limewahi kufanyika kiasi cha kuamsha
morali zaidi kwa watumishi kutokana na mwamko mkubwa wa wananchi
kushiriki zoezi hilo.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi
wa Kata hiyo; mtendaji wa Kata hiyo amesema wao kama Kata wamehamasisha
wananchi kujitokeza kusajiliwa na kutokana na ushirikiano mkubwa
ulioonyeshwa na wananchi wana imani Kata yao watakamilisha zoezi la
Usajili ndani ya muda uliopangwa.
“Kama unavyoona hapa wananchi ndo
wamekwenda wenyewe kutafuta genereta baada ya umeme kukatika na
hawajashurutishwa na mtu… wamekusanyana na ghafla tunashtukia wanafunga
genereta wakati tukiwa bado tunatafakari namna ya kufanya na wapi pa
kupata huduma hiyo.
Hii kwangu siyo kawaida kuona wananchi wakijituma
hivi kwenye zoezi la kitaifa. Wananchi wana mwamko na shauku kubwa ya
kuwa na Vitambulisho vya Taifa” alisema
Zoezi la kuwasajili wananchi
katika Mkoa wa Arusha limeanza kwa kasi kubwa na katika Wilaya ya
Arumeru zoezi hilo linaendelea katika Kata za Makiba, Maroroni na Kikwe.
Usajili huu unahusisha wananchi wote wenye umri wa miaka 18 na
kuendelea na unafanyikia kwenye vituo vya Usajili vilivyoanishwa na NIDA
kwa kushirikiana na Uongozi wa Wilaya ya Arumeru.
0 comments:
Post a Comment