Dar es Salaam. Jalada la kesi inayomkabili
mfanyabiashara, Yusuf Ali maarufu kama Mpemba na wenzake watano bado
lipo mikononi mwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Mashtaka (DPP).
Hayo
yalisemwa jana na upande wa mashtaka katika kesi ya kujihusisha na
biashara haramu ya meno ya tembo inayomkabili mfanyabiashara huo.
Yusuf
na wenzake wanakabiliwa na mashtaka manne ya kujihusisha na biashara
haramu ya meno ya tembo yenye thamani ya Sh785.6 milioni na tayari
upelelezi wa kesi hiyo umekamilika.
Wakili wa Serikali,
Elia Athanas aliieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu
Mkazi Mkuu, Thomas Simba kuwa jalada hilo lipo kwa DPP kwa ajili ya
hatua zaidi za kisheria.
Kesi hiyo jana ilifikishwa mahakamani hapo kwa ajili ya kutajwa.
Athanas alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo umeshakamilika na kuiomba mahakama kupanga tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Kutokana na maelezo hayo, Hakimu Simba aliahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 17 itakapofikishwa tena kwa ajili ya kutajwa.
Washtakiwa
wengine katika kesi hiyo ni mkazi wa Mlimba mkoani Morogoro, Charles
Mrutu; mkazi wa Mbagala Chamazi, Benedict Kungwa; mkazi wa Mbezi,
Jumanne Chima; Ahmed Nyagongo ambaye ni dereva na Pius Kulagwa ambao kwa
pamoja wanakabiliwa na mashtaka manne ya kujihusisha na biashara ya
meno ya tembo.
Inadaiwa kwamba katika tarehe tofauti
kati ya Januari, 2014 na Oktoba, 2016 wakiwa Dar es Salaam, Tanga,
Iringa na Mtwara walijihusisha na mtandao wa ujangili.
Katika
mashtaka hayo inadaiwa walijihusisha na mtandao huo kwa kukusanya na
kuuza nyara za Serikali ambazo ni vipande 50 vya meno ya tembo vyenye
thamani ya Dola 180,000 za Marekani (sawa na Sh392.8 milioni) bila kuwa
na kibali cha mkurugenzi wa wanyamapori nchini.
Katika
shtaka la pili inadaiwa kuwa Oktoba 26, 2016 wakiwa Mbagala Zakhem
jijini Dar es salaam walikutwa na vipande 10 vya meno ya tembo vyenye
uzito wa kilo 13.85 vikiwa na thamani ya Dola 30,000 za Marekani (Sh
65.4 milioni).
Kwenye shtaka la tatu washtakiwa hao
inadaiwa kwamba Oktoba 27, 2016 wakiwa Tabata Kisukuru walikutwa na
vipande vinne vya meno hayo vikiwa na uzito wa kilo 11.1 na thamani ya
Dola 15,000 za Marekani (sawa na Sh32.7 milioni).
Aidha, Oktoba 29, 2016 walikutwa na vipande 36 vya thamani ya Sh294.6 milioni bila kuwa na kibali cha mkurugenzi wa wanyamapori.
0 comments:
Post a Comment