Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (katikati) akitoa maelekezo kwa meneja wa pori la Akiba la Uwanda Jovine Nachihangu (kulia) juu ya kuhakikisha alama zinazowekwa kwenye mipaka ya hifadhi hiyo inakuwa na maandishi yanayoosomeka kuwa unaingia katika hifadhi ili kupunguza migogoro na wananchi. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dkt Khalfan Haule.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewaonya wananchi wa Kijiji
cha Nankanga, Kata ya Nankanga, Wilayani Sumbawanga kuacha tabia ya kuharibu
mali za serikali ili kutafuta suluhu ya migogoro iliyopo baina yao na askari wa
hifadhi ya Pori la Akiba Uwanda katika bonde la ziwa Rukwa huku akimuagiza
kamanda wa polisi Mkoa kuwasaka na kuwakama wote waliohusika na uharibifu huo.
Ametoa maagizo hayo baada ya gari ya hifadhi hiyo kushambuliwa na wavuvi
waishio katika kambi ya uvuvi ya Kijiji cha Nankanga kilichopo pembezoni mwa
ziwa Rukwa, tukio lililotokea tarehe 10.4.2019 ambapo wavuvi hao walivunja vioo
vya gari, kuchomoa tairi pamoja na kuchukua vitu vilivyokuwamo ndani ya gari
huku dereva wa gari hiyo kukimbia na kuicha gari hiyo.
Alisisitiza kuwa wananchi hawawezi kufanya uhalifu ili kuhalalisha madai
yao na uhalifu haulipwi kwa uhalifu na kuongeza kuwa mahali popote penye
uhalifu, sheria huchukua mkondo wake, sio kuanza uharibifu na vitendo vingine
vya uvunjifu wa amani mpaka kutishia uhai wa watu hivyo aliwataka wana Nankanga
kujitafakari kwa kina na kujitambua.
“Hebu fikiria hiyo gari kama ingechomwa moto na uvunjifu mwingine wa
amani mkubwa ungetokea mnadhani mngelala kwenye Kijiji chenu hiki, wengine
mngetumbukia kwenye maji, wengine mngepanda mlima bila ya kujua na wengine
msingekaa kurudi hapa, kwahiyo mimi ninawaonya na ninawakanya iwe ni mara ya
kwanza na ya mwisho, ninyi kama wanakijiji kuleta uvunjifu wa amani ndani ya
Kijiji, msije mkagusa tena mali ya serikali, bahati mbaya sikujua gharama za uharibifu
mlioufanya mngechanga Kijiji kizima kulipa huo uharibifu ambao mmeshaufanya,”
Alisisitiza.
Kwa upande wake Meneja wa Pori la Akiba la Uwanda Jovine Nachihangu
alisema kuwa mgogoro huo ulitokana na askari wa hifadhi hiyo kukamata mitumbwi
sita na wavuvi 18 waliokuwa wakivua katika eneo la hifadhi ndani ya ziwa Rukwa
ambapo hifadhi hiyo ina ukubwa wa kilomita za mraba 5000 huku eneo la nchi kavu
likiwa na kilomita za mraba 490.
“Wakati nipo Mbeya, nilipokea simu kutoka kwa Mkuu wa Wilaya kwamba kuna
watu wanataka kuvamia kambini kwahiyo nichukue tahadhari, kwahiyo nilianza
kuwasiliana na watu waliomo humu kuwa kuna jambo hili na hili linataka kutokea,
gari ilipata pancha Kijiji kwasababu tunakawaida ya kumchukua mwenyekiti wa
Kijiji ili kuwatambua watu wake lakini muda huo dereva alinipigia simu kunambia
hali siyo nzuri na ameiacha gari kijijini, hivyo tuliwasiliana na polisi ili
kuomba msaada,” Alieleza.
Wakati akifafanua tukio hilo Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dkt. Khalfan
Haule alisema kuwa mahusiano baina ya wananchi na askari wa hifadhi hiyo sio
mazuri lakini kitendo cha wananchi kuvamia gari ya serikali kuipiga mawe na
kuiba hakifai na kuongeza kuwa hifadhi hiyo ina mipaka ya muda na mipaka ya
kudumu bado infanyiwa tathmini na Kamati iliyoundwa na Waziri wa Maliasili na
Utalii Dkt. Hamis Kigwangala.
“Waziri Kigwangala mwaka jana alikuwa hapa na miongoni mwa matatizo
tuliyomueleza ni mgogoro wa mpaka kati ya hifadhi na wavuvi, nchi kavu huku
tunashukuru alama zimewekwa na zimepunguza migogoro iliyopo kati ya wananchi na
hifadhi, bado tuna changamoto ya mifugo nae neo la wavuvi bado wavuvi wanaingia
hifadhini,” Alisema.
Wakati huo huo Diwani wa Kata ya Nankanga Anyisile Kayuni alisema kuwa
tukio lililotokea limetokana na chuki kati ya wavuvi na wahifadhi na kudai kuwa
wavuvi wanahisi wanaonewa wakati wahifadhi wanatekeleza majukumu yao ya
kisheria.
“Mgogoro huu nimeukuta tangu naingia udiwani umepitia hatu anyingi sana
hadi kufikia Waziri Dkt. Kigwangala kuwasimamisha watumishi 27 wa wanayapori
lakini mgogorio huu bado haujaisha, Mh. Mkuu wa Mkoa wakazi hawa wa Nankanga
wamepungua idadi uliyoikuta wakati ule wa masika sio hii asilimia kubwa
wamekimbilia forodha ya masuche jirani hapo (wilaya ya) Momba (Mkoani Songwe)
wakitokea mwalo huu hapa,” Alieleza.
Katika hatua nyingine Mh. Wangabo aliwatahadharisha askari wa
wanayamapori kutotumia sheria vibaya na hatimae kuwaonea wananchi kwa kuwapiga
bila ya mpangilio na huku akiwataka wananchi hao kuhakikisha wanatii sheria na
inapotokea wanakiuka sheria hizo basi waache ubishi wakati wanapokamatwa.
Katika kipindi cha mwezi Novemba mwaka 2018 hadi Machi 2019, Wanyama
walioonekana katika pori hilo la Akiba la Uwanda lililopo chini ya Mamlaka ya
Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) Wanyama walioonekana ni Nyati, Swala,
Fisi na Tembo.
0 comments:
Post a Comment