Msaidizi wa Askofu wa Kanisa la Waadventista Wasabato, ukanda wa AfrikaMashariki na Kati(nchi 11), Mchungaji Emanuel Pelote akizungumza na Wanachama wa Wanataaluma na Wajasiriamali wa Kanisa la Waadventista Wasabato Tanzania (ATAPE) katika vipindi maalum vinavyoendelea katika Mkutano wa Chama hicho unaofanyika katika Shule ya Sekondari ya Kusekwa Memorial Mjini Bariadi Mkoani Simiyu kuanzia Aprili 16 hadi Aprili 21, 2019.
Baadhi ya Viongozi na Wanachama wa Chama cha Wanataaluma na Wajasiriamali wa Kanisa la Waadventista Wasabato Tanzania (ATAPE), wakiwa katika vipindi maalum vinavyoendelea katika Mkutano wa Chama hicho unaofanyika katika Shule ya Sekondari ya Kusekwa Memorial Mjini Bariadi Mkoani Simiyu kuanzia Aprili 16 hadi Aprili 21, 2019.
Baadhi ya wananchi wakinunua bidhaa mbalimbali kutoka kwa wajasiriamali ambao ni Wanachama wa Chama cha Wanataaluma na Wajasiriamali wa Kanisa la Waadventista Wasabato Tanzania (ATAPE), katika Viwanja vya Shule ya Sekondari ya Kusekwa Memorial Mjini Bariadi ambako unafanyika Mkutano mkuu wa 20 wa Chama hicho unaofanyika Mkoani Simiyu kuanzia Aprili 16 hadi Aprili 21, 2019.
Na Stella Kalinga, Simiyu
Chama cha Wanataaluma na
Wajasiriamali wa Kanisa la Waadventista Wasabato(ATAPE), kinakusudia kuwekeza
katika ujenzi wa mradi wa maji kuunga mkono juhudi za Serikali katika utoaji wa
huduma ya maji kwa wananchi na ujenzi wa hosteli ili kutoa huduma za malazi
katika Mkoa wa Simiyu.
Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa
Chama hicho Bw. Freddie Manento, Aprili 17, 2019 wakati alipozungumza na
waandishi wa habari katika Viwanja vya Shule ya Sekondari ya Kusekwa Memorial
Mjini Bariadi, ambako unafanyika Mkutano Mkuu wa 20 wa Chama hicho kwa
takribani siku saba ambao umeanza Aprili 16 na utahitimishwa Aprili 21, 2019.
Manento amesema ATAPE
imedhamiria kuwekeza kwenye miradi itakayokuwa na tija kwa Watanzania wote kwa
ujumla huku akieleza kuwa timu ya wataalam wa uwekezaji wa chama hicho
inaendelea kufanya utafiti, ili kubaini eneo litakalofaa kuchimba kisima cha
maji na kujenga hosteli mkoani Simiyu.
“Tumedhamiria kuacha alama katika
Mkoa wa Simiyu kupitia mkutano wetu wa 20 wa ATAPE, tumepewa fursa ya kiwanja
kwa ajili ya kujenga hosteli katika kukabiliana na changamoto ya malazi, lakini
pia wataalam wetu wanaendelea na utafiti kubaini mahali tutakapochimba kisima
kwa ajili ya huduma ya maji kwa Wanasimiyu” alisema Manento
Pamoja na miradi hiyo inayotarajiwa kutekelezwa mkoani Simiyu, Manento
amesema ATAPE imewekeza katika kilimo kwenye mashamba ya miti, miwa, mikorosho,
miti ya maparachichi ambayo kwa ujumla yana ukubwa wa ekari 10,000 na ekari
zaidi 3500 ambazo zinatarajiwa kufanyiwa uwekezaji mwingine.
Amesema hadi sasa ni takribani shilingi bilioni 1.039 imewekezwa
katika miradi hiyo ambayo pia imechangia kutoa ajira za kudumu na za msimu kwa
Watanzania walio katika maeneo yenye miradi hiyo, huku akibainisha kuwa katika baadhi
ya maeneo hayo ATAPE imetoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa miradi mbalimbali ya
maendeleo kwa jamii husika.
Katika hatua nyingine Mwenyekiti huyo wa ATAPE ametoa wito kwa wananchi
mkoani Simiyu hususani Bariadi kutumia mkutano huo kama fursa kiuchumi kupitia
biashara ya bidhaa na huduma mbalimbali ikiwemo usafiri wa kuwatoa na
kuwapeleka wajumbe katika eneo la mkutano
Kwa upande wao baadhi ya wajasiriamali wa Mkoa wa Simiyu wamesema
Mkutano wa ATAPE umekuwa fursa kwao kwa kuwa utawasaidia kujiingizia kipato na
kupata ujuzi mpya kupitia huduma na bidhaa zitakazouzwa kwenye mkutano huo.
“ Binafsi ninashukuru uwepo wa mkutano huu, mimi kama mjasiriamali
nimepata pesa, nimepata ujuzi mpya kutoka kwa wenzetu waliotoka nje ya Simiyu,
hivyo ninaendelea kuwaomba viongozi wetu waendelee kutuletea matukio kama haya
ili tupate pesa zaidi” alisema Bw. John Bubinza mjasiriamali kutoka Bariadi.
Nao wajasirimali wanaoshiriki katika mkutano huo kutoka nje ya mkoa wa
Simiyu wametoa wito kwa Wananchi mkoani Simiyu kufika katika viwanja vya Shule
ya Sekondari Kusekwa Memorial kujifunza na kujionea kazi mbalimbali za
ujasirimali ili waweze kupata ujuzi na maarifa mapya ya kufanya kazi za
ujasiriamali kwa ufanisi na kununua bidhaa mbalimbali.
“ Binafsi nawakaribisha wananchi wa Mkoa wa Simiyu kufika katika viwanja
hivi waje wajionee, wakifika hapa watapata bidhaa kwa bei za jumla na rejareja,
laikini pia nawasisitiza wanawake wainuke waje waone maana ujasiriamali
unatuinua sana wanawake” alisema Mjasiriamali Esther Jichogo kutoka Jijini Dar
es salaam.
Wanachama zaidi ya 1500 wa Chama cha Wanataaluma na Wajasiriamali wa
Kanisa la Waadventista Wasabato(ATAPE) wanaendelea na mkutano wao wa 20 mkoani
Simiyu, ukiwa na Kauli mbiu “KUSONGA MBELE NA MUNGU” ambao
utachukua takribani siku saba kuanzia tarehe 16/04/2019 hadi 21/04/2019.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment