Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akizungumza na Waandishi wa Habari wakati alipokutana na Watendaji wa Makampuni yanayofanya ya Urasimishaji pamoja na wale wa sekta ya ardhi kuzungumzia zoezi la Urasimishaji na utoaji leseni za Makazi katika jiji la Dar es Salaam.
Na Munir Shemweta, WANNM
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amesema
kuanzia sasa gharama za urasimishaji haitazidi shilingi 150,000 badala ya
250,000 iliyopangwa awali na makampuni yatakayoenda kinyume yatachukuliwa hatua
ikiwemo kufutwa.
Lukuvi alitoa kauli hiyo leo jijini Dar es Salaam alipokutana na
Makampuni ya Upangaji na Upimaji yanayofanya kazi ya urasimishaji katika mitaa
mbalimbali nchini pamoja na watendaji wa sekta ya ardhi.
Kwa mujibu wa Lukuvi, baada ya Wizara yake kuona zoezi la urasimishaji linasuasua
wamegundua asilimia 30 pekee ndiyo iliyorasimishwa tangu kuanza zoezi hilo na
hali hiyo imechangiwa na uwezo mdogo wa wananchi wengi kumudu gharama za
urasimishaji.
Waziri Lukuvi alisema, alichotegemea kwa makampuni yaliyopewa kazi ya
urasimishaji ni kuwa na uzalendo kwa kushusha gharama lakini yameshindwa
kupunguza gharama jambo lililoifanya serikali kuona haja ya kupitia upya
gharama hizo na kubaini gharama za msingi ili kumuwezesha mwananchi
kupata hati na kusisitiza punguzo hilo halitawahusu waliolipia gharama za
urasimishaji.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ameyataka makampuni
yanaoyoendesha zoezi la urasimishaji kuhakikisha kiasi cha fedha inachowatoza
wananchi kinaishia hatua ya Hati na gharama itakayolipwa na mwananchi baada ya
kurasimishwa ni kodi ya ardhi na kuyatahadharisha kutochukua muda mrefu
kukamilisha zoezi hilo.
Amewataka wananchi wote wanaoishi kwenye maeneo yasiyo rasmi kuhakikisha
wanaingia katika zoezi la urasimishaji ili kupata hati itakayowawezesha
kiuchumi na kusisitiza kuwa suala hilo linafanyika kwa nia njema kwa nia ya
kuwaongezea mtaji wananchi kwa kupatiwa nyaraka itakayowasiadia kukopa fedha
benki.
Akigeukia suala la Leseni za Makazi, Waziri Lukuvi alisema zoezi
hilo linaendelea vizuri katika jiji la dar es Salaama kwa gharama ya shilingi
elfu tano hadi hatua ya upatiwaji leseni ya makazi na kusisitiza kuwa leseni
hiyo siyo ya kudumu bali itakuwa kwa miaka mitano na kuwataka wananchi walio
katika maeneo ya urasimishaji kuendelea na zoezi hilo kwa kuwa wizara inayo
kanzi data itakayotunza takwimu za mazoezi yote mawili.
‘’Tunataka kuwa na database ya nani anamiliki ardhi kiasi gani na kila
mwananchi lazima awe na leseni ya makazi au hati kwa lengo la kushiriki kulipa
kodi’’ alisema Lukuvi
Hata hivyo, Lukuvi alisikitishwa na baadhi ya Makampuni ya urasimishaji
kushindwa kutoa takwimu wakati wa zoezi la upimaji zinazoendana na miongozo ya
wizara na kuyataka yote yaliyoenda kinyume kurudia zoezi na kuongeza kuwa
kuna makampuni 34 yaliyotuma takwimu ambazo ni chafu na kuyapongeza makampuni
mawili ya Visible Planners na Afro Max kwa kufuata taratibu zote za
urasimishaji.
Lukuvi alionya baadhi ya makapuni ya urasimishaji kuacha kuwalaghai
wananchi kwa kuwapatia leseni za makazi badala ya hati kwa gharama za urasimishaji
na kusema kufanya hivyo ni kosa la uhujumu uchumi na hatua kali zitachukuliwa
dhidi yao.
Vile vile Lukuvi amewataka watendaji wa serikali ambao wana makampuni
yanayofanya kazi ya urasimishaji kuchagua jambo moja la kuitumikia serikali ama
makampuni yao kwa kuwa wanatumia muda mwingi kufanya kazi katika makampuni yao
badala ya kuitumikia serikali.
‘’Ninyi watendaji wa serikali badhi yenu mna makampuni ya urasimishaji
na ndiyo mnaoharibu zoezi mnataka squatters ziendelee ili mnufaike na mnapima
halafu michoro mnapitisha ninyi hii ni conflict of interest’’ alisema Likuvi.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment