Afisa afya wa mkoa wa Mwanza(R.S.O) Fungo S Masalu, akitoa ufafanuzi wa kuhusu madhara yatokanayo na uchafu wa mazingira katika jiji la Mwanza, pamoja na kueleza namna mradi wa usafi wa mazingira jijini Mwanza (Pro poor WASH entreprise) utakavyowanufaisha wakazi wa jiji hilo. |
Wadau wakifuatilia kwa makini mkutano huo wa uzinduzi wa mradi wa usafi wa mazingira jijini Mwanza. |
Picha ya pamoja mara baada ya uzinduzi wa uzinduzi wa mradi wa usafi wa mazingira jijini Mwanza. |
Jiji la Mwanza lililoko mwaloni mwa ziwa Victoria ambalo ni chanzo kikuu cha maji kwa wakazi wa mikoa ya kanda ya ziwa, lina wakazi takribani 819,796 huku ongezeko la watu likiwa ni asilimia 3.2 kwa mwaka. Asilimia 66 ya wakazi wa jiji la Mwanza hawana huduma za usafi wa mazingira, ambapo zaidi ya asilimia 20 hawana vyoo, huku zaidi ya asilimia 90 ya vyoo haviko kwenye mtandao wa maji taka wa MWUWASSA. Jiji la Mwanza huzalisha taka ngumu kwa wastani wa tani 813 kwa siku, ambapo ni asilimia 74 tu ya taka zinazozalishwa ndio hukusanywa na kupelekwa dampo. Hivyo taka ngumu bado ni chanagamoto kutokana na uchafuzi wa mazingira na vyanzo vya maji, hivyo kupelekea milipuko ya magonjwa na vifo hasa kwenye jamii masikini.
Amref Tanzania ikishirikiana na ofisi ya RAS Mwanza, kwa msaada wa kifedha toka Manispaa ya jiji la Madrid nchini Hispania, inaanzisha mradi wa kuboresha usafi wa mazingira kwa watu wenye kipato cha chini kibiashara jijini Mwanza. Mradi huu unalenga kusaidia juhudi za Serikali ya Tanzania kuongeza na kuboresha huduma za usafi wa mazingira kupitia kamapeni ya kitaifa NSC-II (2016-2020); Mkakakati wa Kitaifa wa kukuza uchumi na kupunguza umasikini (MKUKUTA-2015) na kufikia Malengo Endelevu ya Millenia (SDGs-2030). Lengo mahususi la mradi ni kuchangia utekelezaji wa mpango mkakati wa jiji la Mwanza wa mwaka 2004 wa kusimamia taka ngumu na kuboresha vyoo.
Mradi huu utawalenga akinamama na vijana katika maeneo ya wakazi wenye kipato cha chini kwa kuwezesha fursa za kukua kiuchumi kwa kufanya ujasiriamali kwa kuzalisha bidhaa mbadala kutokana na taka ngumu na vinyesi. Mradi unatarajia kuongeza fursa kwa jamii nzima katika uelewa na mahitaji ya kusimamia na kuondoa taka katika maeneo ya makazi. Mradi utatoa elimu ya ujenzi wa vyoo bora na huduma za kuondoa vinyesi katika ngazi ya kaya, huku ukiijengea Serikali uwezo wa kutoa huduma kwa kushirikiana na taasisi binafisi/wananchi kupitia mbinu za kibiashara. Mradi huu kwa kuanzia utatekelezwa katika Wilaya ya Ilemela na Nyamagana , ambapo unarajia kufikia walengwa 200,000.
Kuhusu Amref Health Africa.
Amref Health Africa ni shirika la kimataifa lisilo la Kiserikali lililoanzishwa mwaka 1957 kama Madaktari wa Anga (Flying Doctors) wa Afrika Mashariki kwa lengo la kutoa msaada wa matibabu katika maeneo magumu kufikika ndani ya Afrika Mashariki. Mwaka 1987, Amref Health Africa ilifungua rasmi ofisi yake jijini Dar es Salaam Tanzania, ikiwa na lengo la kuchangia juhudi za Serikali ya Tanzania katika kutekeleza miradi ya kuboresha huduma za afya na maendeleo ya Jamii kupitia sera na miongozo ya afya ya kitaifa. Kwa sasa Amref iko katika nchi 35-barani Africa, Asia, Ulaya na Marekani.
Hivi sasa, Amref Health Africa Tanzania ina miradi zaidi ya 25 katika mikoa mbalimbali nchini Tanzania (takribani asilimia 45 ya miradi yote inatekelezwa katika mikoa ya kanda ya ziwa). Vile VileAfrica Tanzania ina miradi yenye mtazamo wa Kitaifa kama vile mpango wa elimu kwa njia ya masafa (eLearning) na mradi wa kuimarisha Maabara. ambao unatekelezwa katika mikoa tofauti nchini ikiwemo na Zanzibar. Miradi Amref nchini Tanzania imegawanyika katika maeneo makuu manne ambayo ni: Afya ya uzazi, watoto wachanga na vijana (RMNCAH); Mpango wa Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (DCP) ambao unajumuisha programu za VVU na UKIMWI, Kifua Kikuu (TB), Huduma za Maabara, Fistula ya Uzazi na Malaria; Maji safi, Usafi wa mazingira na mwili (WASH) na Mpango wa Kujenga Uwezo kupitia mafunzo (Capacity Building).
Kupitia miradi hii, Amref Health Africa imeendelea kujibu vipaumbele vya afya ya kitaifa na malengo ya maendeleo endelevu katika kushughulikia mahitaji ya afya ya wanawake na watoto. Amref Health Africa inajitahidi kuongeza ufanisi na uendelevu wa huduma hizi kwa kiuchangia kuimarisha mifumo ya afya, kuboresha upatikanaji wa huduma na kuhamasisha mifumo ya afya ya jamii na sera kwa ujumla. Pamoja na mkakati wake mpya wa 2018-2022, badoAmref Heath Africa ni msaidizi mkubwa wa ajenda ya Huduma ya Afya kwa Wote.
0 comments:
Post a Comment