Na Stella
Kalinga, Simiyu
Mkuu wa Mkoa
wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka ametoa wito kwa viongozi na watendaji wa Serikali
mkoani hapa kuona umuhimu wa kuwashirikisha viongozi wa dini, siasa na wa
kimila katika utoaji wa elimu kwa jamii na kuwahamasisha wanawake wajawazito
kuhudhuria kliniki na kujifungulia katika vituo vya kutolea huduma za afya ili
kuzuia vifo vitokanavyo na uzazi.
Mtaka
ameyasema hayo wakati wa Uzinduzi wa Kampeni ya Uwajibikaji katika kuzuia
vifo vitokanavyo na uzazi ijulikanayo kama JIONGEZE, Tuwavushe Salama uliofanyika
Mei 02, 2019 Mjini Bariadi.
“ Ni vizuri tukaongeza wigo wa kutoa elimu kwa
jamii kuhusu umuhimu wa mama wajawazito kuhudhuria kliniki kipindi cha
ujauzito na kuhakiksha wanajifungulia kwenye vituo vya kutolea huduma za afya;
viongozi wa dini,siasa na wa kimila wana nafasi kubwa kwenye jambo hili muone
namna ya kuwashirikisha “ alisema Mtaka.
Amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau
mbalimbali wa afya ikiwa ni pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa
linaloshughulikia idadi ya watu Duniani(UNFPA) imeboresha vituo vya kutolea
huduma, hivyo ni vema jamii ikaelimishwa umuhimu wa kutumia huduma za afya ili
kuokoa maisha ya mama na mtoto.
Katika hatua nyingine Mtaka ameishukuru UNFPA kwa
namna ilivyosaidia katika ujenzi wa miundombinu ya afya,vifaa na vitendea kazi
kama magari ya kubeba wagonjwa huku akisisitiza viongozi na watendaji
walioshiriki katika uzinduzi wa kampeni hii kutoka na dhamira ya kuwavusha
salama akina mama wajawazito na watoto na kupinga vifo vitokanavyo na uzazi..
Mwakilishi wa Ofisi ya Rais Tawala za
Mikoa na Serikali za Mitaa, Dinna Atinda ameusisitiza uongozi wa
mkoa kusimamia vituo vinavyotoa huduma za afya za msingi na dharura
kuhakikisha vinatoa huduma bora kwa wananchi.
Naye Mwakilishi wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Salome Mwijuma ametoa wito kwa
jamii kuendelea kuwasaidia wanawake wajawazito waweze kuhudhuria kliniki muda
wote, wapate lishe bora na kujifungulia katika vituo vya kutolea huduma ili
wajifungue salama.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Dkt. Mageda
Kihulya amesema mwaka 2015 watoto 680 walifariki na mwaka 2018 watoto 640
walifariki, wakati kwa upande wa akina mama wanaojifungua vifo vimepungua
kutoka 48 mwaka 2015 na kufikia 40 mwaka 2018, jambo ambalo linaonesha
kuwa nguvu ya ziada kutoka wadau mbalimbali inahitajika kumaliza tatizo hili.
Dkt. Mageda amesema sababu zinazosababisha vifo
vingi vya akina mama wajawazito kama vile kutokwa na damu nyingi wakati wa
kujifungua na mkingamo wa uzazi zinaweza kuzuilika, hivyo akatoa wito kwa
wakina mama kujifungulia katika vituo vya kutolea huduma kuzuia vifo hivyo,
huku akisisitiza watoto chini ya miaka mitano nao wapewe chanjo kuzuia vifo.
Makamu Mwakilishi mkaazi wa Shirika la Umoja wa
Mataifa linaloshughulikia idadi ya watu Duniani(UNFPA) hapa nchini, Dkt.
Hashina Begum amesema shirika hilo litaendelea kushirikiana na Serikali katika
jitihada mbalimbali za kupunguza vifo vya akina mama wajawazito na watoto.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment