Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. (Mst) Nicodemus
Mwangela ameagiza kushikiliwa na polisi kwa masaa 24 Kaimu Mkurugenzi wa
Mamlaka ya Mji Mdogo wa Mlowo Seriadi Mbugi kutokana na kurundika takataka
jirani na makazi ya wananchi pamoja na shule ya Msingi Mlowo na hivyo
kuhatarisha maisha yao.
Brig. Jen. (Mst) Mwangela amefikia uamuzi huo
mapema leo wakati akifanya ukaguzi wa hali ya usafi katika Mamlaka ya Mji Mdogo
wa Mlowo na kukuta takataka zimemwagwa katikati ya makazi ya wananchi ikiwa ni
siku saba tangu amuelekeze Kaimu Mkurugenzi huyo kuhakikisha mji huo unakuwa
Msafi.
“Nilifanya Mkutano na wananchi wa Mji wa Mlowo na
malalamiko yao makubwa yalikuwa mrundikano wa takataka na madampo katikati ya
miji yao, nilimuagiza na kumpa siku saba Mkurugenzi wa Mji mdogo wa Mlowo
kuhakikisha anausafisha mji huu lakini leo siku saba zimepita ninakagua na
kukuta takataka zimemwaga katikati ya makazi ya watu, naambiwa watoto wanacheza
na kuokota taka hapa, huu sio ubinadamu”, amesema Brig. Jen. (Mst) Mwangela
Ameongeza kuwa Mkurugenzi huyo amekiuka agizo lake
na hivyo kuhatarisha maisha ya wananchi hao kwa kuwawekea takakata wananchi
katikati ya makazi yao kinyume na taratibu za kiafya zinavyoelekeza.
“Huu sio utendaji wa serikali kabisa, licha ya
Kaimu Mkurugenzi wa Mji Mdogo kukaa ndani, namuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa
Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi kuhakikisha ndani ya masaa manne takataka hizo
ziwe zimetolewa na dampo hilo lifutwe”, amesisitiza Brig. Jen. (Mst) Mwangela
Kwa upande wake mkazi wa mtaa wa shule Bi Salehemu
Filimon Mwaihojo amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kutembelea eneo hilo na kutatua
kero hiyo kwakuwa wamekuwa wakipata hofu ya magonjwa kutokana na uwepo wa
takataka hizo
“Hii ni wiki ya pili wanamwaga matakataka hapa,
watoto wanachezea na kuokota makopo wanachota maji machafu na kunywa kwenye
makopo hayo machafu wengine unakuta wanaokota kondomu zinazomwaga hapa
wanapuliza wao wanajua mipira, kwakweli tulikuwa na hali mbaya, kwakuwa tuliona
wametumwagia magonjwa hapa”, amesema Mwaihojo
Ameongeza kuwa dampo hilo lipo pia jirani na Shule
ya Msingi Mlowo na hivyo wanafunzi hupita na kuchezea hapo hali ambayo
wangeweza kudhuriwa na vipande vya chupa na taka ngumu zinazo mwagwa hapo huku
wengine wakiokota na kula mabaki ya vyakula yanayotupwa hapo na hivyo
kuhatarisha afya zao.
0 comments:
Post a Comment