Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Omary Mgumba (Mb)
akijibu swali bungeni leo tarehe 8 Mei 2019 wakati wa mkutano wa kumi
na tano wa Bunge la Bajeti Jijini Dodoma. (Picha Zote Na
Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Omary Mgumba (Mb) akijibu swali bungeni leo tarehe 8 Mei 2019 wakati wa mkutano wa kumi na tano wa Bunge la Bajeti Jijini Dodoma.
Na
Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma
Serikali kwa kushirikiana na taasisi za sekta
binafsi imeendelea kutoa elimu ya kilimo bora inayojumuisha matumizi sahihi ya
mbolea za asili, viuatilifu vya asili, mbegu bora na hifadhi ya mazingira ili
kuzalisha mazao kwa tija na kuwa na kilimo endelevu.
Naibu
Waziri wa Kilimo Mhe Omary Mgumba (Mb) ameyasema hayo bungeni Jijini Dodoma leo
tarehe 8 Mei 2019 wakati akijibu swali la Mbunge wa Chambani Mhe Yussuf Salim
Hussein aliyetaka kufahamu Serikali imeweka mikakati gani ya kutoa elimu ya
mbolea ya asili kwa wakulima na hatua Serikali inayoichukua ili kuona kuwa
Tanzania ni nchi inayoongoza kwa kuzalisha mazao yasiyotumia mbolea za viwandani.
Alisema
kuwa katika kutekeleza mpango wa muda mrefu wa matumizi sahihi ya virutubisho
vya udongo, Serikali kupitia Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI)
inafanya utafiti wa afya ya udongo katika Kanda zote saba za kiikolojia za
kilimo nchini.
Utafiti
huo unalenga kubaini aina za virutubisho na tabia za udongo katika maeneo
mbalimbali nchini ili kuweza kutoa elimu kwa wakulima kuhusu kiasi, aina na
matumizi sahihi ya mbolea za viwandani na asili. Utafiti huo umeanza kwa
kuchukua sampuli za udongo katika Kanda za Nyanda za Juu Kusini, Kanda ya Kati,
Kanda ya Kaskazini na sehemu ya Kanda ya Mashariki (Mkoa wa Morogoro) na
utaendelea katika maeneo mengine nchini na kukamilika Juni 2020.
Alisema, kwa kutambua
ongezeko la mahitaji ya mazao na bidhaa za kilimo zinazozalishwa kwa kutumia
mbolea za asili na viuatilifu vya asili, Serikali imeboresha mtaala wa mafunzo
katika vyuo vya kilimo ambapo mada za kilimo hai na hifadhi ya mazingira
zimejumuishwa ili kuwawezesha maafisa ugani na wakulima kupata elimu hiyo.
Mhe Mgumba aliongeza kuwa
Serikali kwa kushirikiana
na Tanzania Organic Agriculture Movemet (TOAM), Sustainable Agriculture
Tanzania (SAT), Ecology Agriculture chini ya SWISSAID, Zanzibar Organic
Producers (ZANOP), Tanzania Alliance for Biodiversity (TABIO) na TANCERT inatoa
elimu ya kilimo hai kwa wakulima na kutoa vyeti vya ubora wa mazao kwa ajili ya
masoko maalum. Baadhi ya mazao ambayo yanazalishwa katika mfumo wa kilimo hai hapa
nchini ni pamoja na kakao, kahawa, pamba na viungo.
Kadhalika,
akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Mhe Easter Michael Mmasi aliyetaka kufahamu
kuhusu ushiriki wa wanawake kwenye sekta ya kilimo, Mhe Mgumba alisema kuwa Sekta
ya Kilimo inajumuisha sekta ndogo za kilimo mazao, mifugo, uvuvi na misitu.
Bajeti
za Wizara za Sekta ya Kilimo zinajumuisha bajeti za Wizara za sekta husika,
Bodi za mazao na Taasisi mbalimbali zilizo chini ya Wizara za Kisekta. Utekelezaji
wa bajeti hizo huwawezesha wanaume na wanawake
katika shughuli za kilimo. Wanawake wanachangia asilimia 90.4 ya nguvukazi ya
wanawake inayotumika katika shughuli za kilimo na kuchangia wastani wa asilimia
70 ya mahitaji ya chakula nchini.
Mhe
Mgumba alisema kuwa katika kutatua changamoto hizo Serikali inaendelea
kusimamia utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ya mwaka
2004 kupitia mifuko ya uwezeshaji ikiwemo Mfuko wa Maendeleo wa Wanawake (Women
Development Fund - WDF) ambao huchangiwa asilimia 4 ya mapato ya Mamlaka za
Serikali za Mitaa kwa kila mwaka. Katika mwaka 2017/2018, jumla ya Shilingi
15,633,312,764.91 zimetolewa kwa vikundi 2,919 vya wanawake na vijana vyenye
jumla ya wanawake wajasiriamali 29,190 katika Halmashauri mbalimbali nchini.
Aidha,
alisema kutokana na umuhimu wa wanawake katika kilimo Serikali imeielekeza Benki
ya Maendeleo ya Kilimo (Tanzania Agricultural Development Bank – TADB) katika
mikopo inayotoa asilimia 20 ya mikopo itolewe kwa vikundi vya wanawake. Hadi
Januari 2019, asilimia 33 ya mikopo imetolewa katika vikundi vya wanawake
kupitia Benki ya TADB. Vilevile, benki za NMB na Azania zimeanzisha dirisha
maalumu la kutoa mikopo kwa vikundi vinavyo jishughulisha na kilimo na miradi
mbalimbali. Pia Serikali imehamasisha wanawake kujiunga kwenye vikundi vya
ushirika wa akiba na mikopo kama SACCOS, VICOBA ili kupata huduma za kifedha na
mikopo kwa urahisi ili kuongeza mitaji yao katika kilimo.
Mhe
Mgumba aliongeza kuwa, Serikali imeuelekeza Mfuko wa Pembejeo za Kilimo (Agricultural
Input Trust Fund - AGITF) kutoa kipaumbele kwa vikundi vya wanawake vinavyoomba
mikopo ya kuendeleza kilimo. Vile vile, Serikali imeendelea kutoa hati miliki
za ardhi za kimila na hati miliki za ardhi kwa ajili ya kuwawezesha wanawake
kumiliki ardhi na kuzitumia kama dhamana kukopa katika taasisi mbalimbali za
kifedha ili waweze kupata mitaji ya kununua pembejeo na zana bora za kilimo ili
kuongeza uzalishaji, tija na kuanzisha viwanda vidogo vidogo vya usindikaji wa
mazao ya kilimo.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment