Na Stella Kalinga, Simiyu
Mkuu wa Mkoa
wa Simiyu Mhe. Anthony Mtaka amesema Viongozi Mkoani Simiyu
wataendelea kufanya kazi na kuwahudumia wananchi kwa
kuzingatia utawala bora, utawala unaofuata sheria na uongozi wa kuheshimiana na
kusikilizana.
Mtaka
ameyasema hayo Mei Mosi, 2019 wakati alipokuwa akizungumza na wafanyakazi na
wananchi mkoani humo katika Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Kimkoa,
yaliyofanyika katika Uwanja wa Nguzonane Wilayani Maswa.
“Tungependa
tujenge utumishi ambao ni wa kipekee sana kwenye mkoa na kila mtumishi aliye
kwenye mkoa huu ajisikie fahari kufanya kazi Simiyu; ahadi yangu kwenu ni
kwamba tutaendelea kufanya kazi kwa kuheshimiana,kusikilizana na kutiana moyo
katikati ya changamoto ambazo watumishi wanazipitia” alisema
Aidha, amewashukuru wafanyakazi kwa namna
walivyojitoa kwa hali na mali kuhakikisha kwamba malengo ya Serikali ya
kuwahudumia wananchi yanatekelezeka na kusisitiza kuwa mkoa utaendelea
kufanya kazi kwa ushirikiano na Vyama vyote vya wafanyakazi na kuwataka waajiri
wote wathamini vipaji vya watumishi wao.
Kwa upande wake Katibu wa Shirikisho la Vyama vya
Wafanyakazi Mkoa wa Simiyu, Bw. Said Mselem ameomba Serikali kushughulikia
suala la upandaji wa mishahara na madaraja kwa watumishi ili kuwaongezea ari na
motisha katika kazi.
Katika hatua nyingine Mselem ameiomba Serikali kuu
kuona uwezekano wa kuwabadilishia mfumo wa malipo ya mshahara watumishi
wanaolipwa kupitia mapato ya ndani na kuanza kuwalipa kupitia HAZINA, ili wawe
na uhakika wa kupata mishahara yao na michango yao ya mifuko ya hifadhi ya
jamii iwasilishwe kwa wakati.
Nao baadhi ya wafanyakazi kutoka vyama
tofauti vya wafanyakazi wamesema Wafanyakazi Mkoani Simiyu wanapenda kazi zao
na wanafanya kazi kwa uadilifu, hivyo wameiomba Serikali iendelee
kuboresha mazingira na kuwasaidia kutatua changamoto zao ili waweze kufanya
kazi wa uhuru na kujituma zaidi.
‘Watumishi tunapenda kazi zetu na tunafanya kwa
bidii na uadilifu, tunajua wapo wachache wanaotuangusha lakini tunaendelea
kuwahimiza wawajibike kutimiza azma ya kuwatumikia wananchi, ombi letu kwa
Serikali itukumbuke kwenye kupanda madaraja wapo ambao hawajapanda toka mwaka
2015” alisema Mwenyekiti CWT Itilima Mwl. Rehema Shalali.
“Watumishi wanaolipwa kwa mapato ya ndani
wanakutana na changamoto ya mafao yao wanapostaafu, mafao hayaendi kwenye
mifuko ya hifadhi ya jamii kwa kuwa wakati maana hawalipwi mishahara kwa wakati
tunamwomba Mhe. Rais aliangalie hili, ili watumishi hao nao waweze kulipwa na
HAZINA moja kwa moja” alisema Sara Kiyuga Mjumbe wa Baraza Kuu TALGWU Taifa.
Maadhimisho
ya Mei Mosi kwa mwaka 2019 yamebebwa na Kauli Mbiu “ TANZANIA YA
UCHUMI WA KATI INAWEZEKANA, WAKATI WA MISHAHARA NA MASLAHI BORA KWA WAFANYAKAZI
NI SASA” ambapo yamefanyika kwa mara ya saba sasa Kimkoa
tangu mkoa wa Simiyu kuanziswa mwezi Machi, 2012.
0 comments:
Post a Comment