Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizindua Ripoti ya Matokeo ya Utafiti wa Msingi kuhusu Haki na Usalama wa Umiliki wa Rasilimali Ardhi na Makazi Tanzania jijini Dodoma leo tarehe 3 Mei 2019. Kushoto ni Mwakilishi wa kutoka Taasisi ya Prindex David Ameyaw na wa pili kulia ni Mtakwimu Mkuu Serikali Dkt Albina Chuwa.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wawakilishi wa taasisi wakati wa uzindua Ripoti ya Matokeo ya Utafiti wa Msingi kuhusu Haki na Usalama wa Umiliki wa Rasilimali Ardhi na Makazi Tanzania jijini Dodoma leo tarehe 3 Mei 2019. Wa pili kushoto waliokaa ni Mwakilishi wa kutoka Taasisi ya Prindex David Ameyaw na wa pili kulia waliokaa ni Mtakwimu Mkuu Serikali Dkt Albina Chuwa.(PICHA NA WIZARA YA ARDHI)
Na Munir Shemweta, DODOMA
Tanzania imeshika nafasi ya nne kati ya nchi tisa
za Kusini na Mashariki mwa Afrika zilizofanyiwa utafiti kwa kuwa na asilimia 64
ya watu wanaoamini kuwa hali ya umiliki wa ardhi na makazi ni salama.
Hayo yalibainika leo tarehe 3 Mei 2019 wakati wa
uzinduzi wa Ripoti ya Matokeo ya Utafiti wa Msingi kuhusu Haki na Usalama wa
Umiliki wa Rasilimali Ardhi na Makazi Tanzania uliofanywa na Ofisi ya Taifa ya
Takwimu, uzinduzi ulifanyika jijini Dodoma.
Akizungumza wakati wa kuzindua Ripoti hiyo, Naibu
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula alisema
kiwango hicho ni kikubwa zaidi ya wastani wa asilimia 61 kwa nchi tisa
zilizofanyiwa utafiti katika Afrika ya Magharibi.
Aidha, Utafiti wa Ripoti hiyo unaonesha Tanzania imeshika nafasi ya kumi kati
ya nchi 33 zilizoshiriki katika Utafiti huo kwa kuwa na asilimia zaidi ya
hamsini ya watu wanaomiliki makazi yao wenyewe.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi
alisema, matokeo ya utafiti huo yametokana na hatua mbalimbali ambazo serikali
imeendelea kuzichukua ili kuhakikisha wananchi wake wanakuwa na usalama wa
umiliki wa ardhi na makazi.
Kawa mujibu wa Dkt Mabula, kama ungefanyika
utafiti mwingine leo basi huenda matokeo yake yangekuwa
tofauti kutokana na Serikali kudhamiria kupanga , kupima na kumilikisha kila
kipande cha ardhi na kutolea mfano katika mwaka wa fedha 2018/2019
Serikali ilipanga kupima na kumilikisha vipande vya ardhi.
Dkt Mabula alibainisha kuwa, takwimu zinaonesha
kati ya mwezi Agosti 2018 na Machi 2019 Hatimiliki 36,428 zimeandaliwa kwa
wamiliki wa viwanja na mashamba na Hatimili za kimila 286472 ziliandaliwa kwa
ajili ya wamiliki wa ardhi walioko vijijini.
Dkt Mabula alisema, hatua nyingine ambazo serikali
imechukua ni pamoja na kuanza kutumia mifumo ya kielektroniki katika
utoaji huduma za ardhi ambapo Mfumo Unganishi wa Kumbukumbu za Sekta
ya Ardhi (ILMIS) umeendelea kufanyiwa majaribio katika wilaya za Ubungo na
Kinondoni na kusisistizia kuwa mfumo huo utasaidia kuongeza kasi ya
umilikishaji ardhi na kupunguza gharama kwa kiasi kikubwa.
Kwa upande wake Mtakwimu Mkuu wa Serikali kutoka
Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt Albina Chuwa alisema utafiti uliofanyika
ulishirikisha sekta zote muhimu na kuzitaja baadhi yake kuwa ni pamoja na
Wizara ya Ardhi, Global Land Allience, DFID sambamba na wananchi wote wakiwemo
wakuu wa kaya za Tanzania Bara na Zanzibar.
Alisema, Tanzania ni nchi ya kwanza kutoa ripoti
yake mwenyewe kati ya nchi 33 na ripoti hiyo itatumiwa na Wizara ya Ardhi
Nyumba na Maendeleo ya Makazi katika kupanga mipango yake na kuzitaka taasisi
za vyuo kutumia ripoti hiyo kufanyia utafiti ili kuisaidia sekta ya ardhi.
0 comments:
Post a Comment