Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba na
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe Charles Mwijage wakijadili jambo
wakati walipotembelea kiwanda cha Sukari Kagera wakiwa kwenye ziara ya siku
tatu ya kikazi Mkoani humo iliyoanza.
Na Mathias Canal-WK, Kagera
Waziri wa kilimo Mhe. Dkt Charles Tizeba (Mb)
amekamilisha ziara ya kikazi ya siku tatu Mkoani Kagera iliyoanza 10
Julai 2018 hadi 13 Julai 2018 kwa kutembelea katika Wilaya tano za Bukoba, Kyerwa, Karagwe,
Missenyi, na Muleba ikiwa ni sehemu ya
utekelezaji wa maagizo ya Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Dkt John Pombe Magufuli aliyoyatoa wakati akiwaapisha viongozi mbalimbali
Ikulu Jijini Dar es salaam tarehe 2 Julai 2018 na kuitaka Wizara ya Kilimo
kufuatilia kwanini wakulima wa zao la Kahawa wanacheleweshewa malipo yao
sambamba na kujua kwanini wakulima wanauza Kahawa yao nchini Uganda na endapo
kama kuna mnunuzi wa kahawa kwa bei nzuri kutoka nchini humo aletwe Tanzania
kunuua.
Baada ya agizo la Rais Magufuli, Waziri huyo wa
Kilimo Mhe Tizeba alimuagiza Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Omary Mgumba (Mb)
kufanya ziara ya siku tatu kuanzia tarehe 4 Julai 2018 mpaka 6 Julai 2018
Mkoani Kagera ili kubaini changamoto za uuzaji wa kahawa ambapo pamoja na mambo
mengine alibaini changamoto zinazowakabili wakulima hao na hatimaye
kucheleweshewa fedha ni pamoja na mikopo ya vyama vikuu vya ushirika KCU na KDCU.
Tarehe 6 Julai 2018 Mhe Tizeba aliitisha kikao
kazi kilichofanyika kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza na
kuhudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa
Halmashauri za Mkoa wa Kagera, Maafisa kilimo na ushirika, pamoja na wakaguzi
wa Pamba ili kupokea taarifa ya kile alichobaini Waziri Mgumba katika ziara
yake hiyo.
Kumalizika kwa kikao hicho kulimlazimu Waziri
Tizeba kuzuru Mkoa Kagera ili kutatua changamoto zinazowakabili wakulima ambapo
pamoja na mambo mengine alikutana na makundi mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupokea
taarifa Mkoa huo iliyowasilishwa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali
Mstaafu Salum Kijuu kuhusu sekta ya Kilimo hususani zao la kahawa, Kukutana na
wadau wa kahawa, kutembelea vyama vya msingi, sambamba na kukutana na wadau wa
Kahawa na viwanda vinavyokoboa Kahawa.
MARUFUKU YA KUUZA BUTURA NA BIASHARA YA MAGENDO
Waziri wa Kilimo Mhe.
Dkt Charles Tizeba akieleza maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha
Mapinduzi wakati akizungumza na wadau wa zao la kahawa kwenye mkutano
uliofanyika katika ukumbi wa Isingiro Wilayani Kyerwa
Akizungumza na wadau wa zao la
kahawa 10 Julai 2018 kwenye mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Isingiro
Wilayani Kyerwa Waziri wa Kilimo Mhe. Dkt Charles Tizeba alikemea vikali biashara
ya kuuza Kahawa nje ya nchi pasina kufuata utaratibu wa kisheria (magendo) hivyo
kwa mwananchi atakayebainika kuendelea na biashara hiyo atachukuliwa hatua Kali
za kisheria ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani.
Agizo hilo lilihusisha pia zuio
la wananchi kuuza kahawa mbichi ingali bado shambani ikiwa haijakomaa (Butura)
kwani kufanya hivyo ni kudhoofisha na kuzorotesha juhudi za muda mrefu
alizotumia mkulima wa kahawa na kumkosesha mapato stahiki.
Alisema serikali itajitahidi
kutafuta bei nzuri ya zao la kahawa ndani na nje ya Afrika Mashariki ili
wananchi wapate faida na tija ya Kilimo huku akieleza kuwa wakulima wa kahawa
kote nchini hawawezi kuona mafanikio ya Kilimo hicho kwa kuendeleza biashara ya
magendo sambamba na biashara ya kahawa mbichi ikiwa shambani (Butura).
Sambamba na hayo pia Waziri wa
Kilimo Mhe Tizeba amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa Ndg
Shadrack Mhagama kukamilisha haraka iwezekanavyo kiwanda cha kukoboa kahawa cha
Omkagando kilichozinduliwa na Mwenge wa Uhuru tangu mwaka 2016 kwa gharama za
serikali lakini mpaka sasa kimeshindwa kuendekezwa.
ZIARA YA WAZIRI WA
BIASHARA WA UGANDA ALIPOZURU TANZANIA YABAINISHA HAKUNA BEI NZURI YA KAHAWA NCHINI UGANDA
Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba
akisalimiana na Waziri wa biashara na ushirika nchini Uganda Mhe Fredric
Ngobi Gume muda mchache kabla ya kuanza kwa mkutano wa mawaziri wa nchi
hizo mbili, mkutano uliohudhuriwa pia Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji
Mhe Charles Mwijage
Kikao kazi
Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba akisisitiza jambo wakati wa
mkutano na Waziri wa biashara na ushirika nchini Uganda Mhe Fredric Ngobi Gume
(Kushoto), Mwingine ni Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe Charles Mwijage (Katikati).
Imebainika kuwa bei ya uuzaji wa Kahawa nchini Uganda haina tofauti kubwa na bei ambayo ingepatikana nchini Tanzania endapo wakulima wangeuza Kahawa zao kwenye soko la awali jambo ambalo linawatoa wasiwasi wakulima wa Kahawa nchini waliokuwa wakidanganywa kuwa bei ya Uganda ni kubwa na yenye tija kwa wakulima kuliko hapa nchini.
Kilogramu moja ya Kahawa ya maganda nchini
Uganda inanunuliwa kwa shilingi 2000 ya Uganda sawa na Shilingi 1400 za
Kitanzania (exchange rate 1.7) kwa mfano hapa nchini Tanzania kwa wiki
iliyopita ambayo mnada wake umefanyika Mjini Moshi tarehe 12 Julai 2018 bei ya
Kahawa ya Kagera ya chama kikuu cha ushirika (KCU) iliuzwa kwa kilo moja ya
maganda kwa wastani wa ni Shilingi 1460 ya bei elekezi ya chini ya kila wiki (Indicative
price) inayotolewa na Bodi ya Kahawa kulingana na bei ya Kahawa katika soko la
dunia.
Hata hivyo, wakulima wa Tanzania watapata
zaidi kwa kuuza mnadani moja kwa moja na kuachana na bei ya shambani kwa
kutumia ushirika wao ambapo bei ya chini inayopatikana ni wastani wa Shilingi
1900 kabla ya gharama za uendeshaji, Kwa kuuza mnadani mkulima anapata bei
kutokana na Ubora wa Kahawa yake na ikiwa kwenye madaraja na hivyo kutoa
motisha kwa wakulima kuzalisha Kahawa bora kuliko kuuza ikiwa ghafi.
Hayo yalibainishwa tarehe 11
Julai 2018 na Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba wakati akizungumza na
wadau wa biashara ya Kahawa katika ukumbi wa Happiness Hoteli uliopo katika
eneo la Mtukula Wilayani Misenyi muda mchache baada ya kukutana na kufanya
mazungumzo na Waziri wa Biashara na Ushirika nchini Uganda Mhe Fredrick Ngobi
Gume katika mkutano uliohudhuriwa pia na Waziri wa Viwanda, Biashara na
Uwekezaji Mhe Charles Mwijage.
"Ndugu zangu kuna jambo
hamlifahamu wale wanaosema Uganda bei ya Kahawa ni nzuri kuliko Tanzania wanawadanganya
hakuna bei nzuri Kule kinachofanya watu kupeleka Kahawa Uganda ni kutokana na
mikopo wanayokopeshana isiyo rasmi (Butura) hivyo makubaliano ya kurejesha
mkopo yanakuwa na masharti magumu yanayowataka wakulima wa Kahawa nchini kulipa
madeni kwa kupeleka Kahawa sio fedha" Alisisitiza Dkt Tizeba wakati
akizungumza na wadau wa Kahawa eneo la Mtukula Wilayani Misenyi
Waziri wa biashara na ushirika
nchini Uganda Mhe Fredric Ngobi Gume alimuhakikishia mwenyeji wake kuwa
biashara ya Kahawa nchini humo ina changamoto sawa katika nchi zote mbili kwa
kuwa swala la mikopo isiyo rasmi inayowanyonya wakulima (Butura) nchini Uganda
ipo kwa kiwango cha juu kiasi kwamba aliomba kuja nchini Tanzania kuanzia tarehe
16-19 Julai 2018 kwa miadi maalumu kwa minajili ya kujifunza kuhusu namna bora
kuendesha ushirika na kuanzisha mfumo wa stakabadhi ghalani.
Waziri Gume alisema kuwa
serikali ya Uganda inayoongozwa na Rais wa nchi hiyo Mhe Yoweri Kaguta Museveni
itaendeleza ushirikiano na serikali ya Tanzania inayoongozwa na Mhe Rais Dkt
John Pombe Magufuli hivyo panapohitajika ushirikishwaji katika biashara
hususani kwenye sekta ya Kilimo watakuwa na msimamo wa pamoja.
SERIKALI KUPAMBANA NA WABADHIRIFU KWENYE VYAMA VYA USHIRIKA
Waziri wa Kilimo Mhe. Dkt Charles Tizeba akitoa
salamu za Wizara ya Kilimo kwa Waziri Mkuu wakati wa kilele cha siku ya ushirika Duniani kwenye dhifa iliyofanyika katika uwanja wa Furahisha Jijini Mwanza. Tarehe 7 Julai 2018
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Kassim M. Majaliwa (Mb) akimkabidhi tuzo ya heshima Waziri wa Kilimo Mhe. Dkt Charles Tizeba kwa kuimarisha sekya ya ushirika nchini wakati wa kilele cha siku ya ushirika Duniani kwenye dhifa iliyofanyika katika uwanja wa Furahisha Jijini Mwanza. Tarehe 7 Julai 2018
Serikali ilitangaza Kiama kwa
viongozi na baadhi ya watendaji wa vyama vya ushirika waofanya ubadhilifu wa
Mali za ushirika kwa manufaa yao pekee pasina kuwanufaisha wanachama wote.
Imeelezwa kuwa ubadhilifu wa
rasilimali za ushirika unaofanywa na baadhi ya viongozi na watendaji wa vyama
vya ushirika umekuwa ni tatizo sugu na hata kuwakatisha tamaa baadhi ya
wananchi kujiunga na vyama hivyo.
Kalipio kwa wabadhilifu hao lilitolewa
na Waziri wa Kilimo Mhe. Dkt Charles Tizeba tarehe 6 Julai 2018 wakati wa hafla
ya ufunguzi wa Kongamano la Kitaifa la wanaushirika Tanzania linalofanyika
katika uwanja wa Furahisha Jijini Mwanza ikiwa ni siku chache kabla ya kuanza
ziara ya kikazi Mkoani Kagera.
Kongamano hilo la Siku mbili
liliambatana na maonesho ya bidhaa na shughuli zinazofanywa na vyama hivyo vya
ushirika kote nchini ambapo wanachama walipata fursa ya kubadilishana uzoefu,
na kujadili mafanikio na changamoto wanazokabiliana nazo katika uendeshaji wa
sekta ya ushirika nchini.
Alisema, serikali inatambua kuwa
ushirika ni nyenzo muhimu ya kuwasaidia wananchi katika upatikanaji wa mtaji na
kuwawezesha kuunganisha nguvu zao za kiuchumi katika kujiendeleza kiuchumi.
Alisema kuwa zipo juhudi kubwa
zinazofanywa na serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha
wananchi wengi zaidi wanahamasishwa na hatimae kujiunga kwenye vyama vya
ushirika kulingana na shughuli zao za kiuchumi ili kuondoa dhana kuwa vyama vya
ushirika ni kwa ajili ya Kilimo cha Mazao ya biashara ya nchi za nje.
Sambamba na hayo Mhe Tizeba aliitaka
Tume ya Maendeleo ya ushirika na shirikisho la vyama vya ushirika kuendelea
kuwahamasisha wananchi kuendelea kutambua umuhimu wa kujiunga katika vyama vya
ushirika kulingana na shughuli za wananchi mfano ushirika wa Viwanda, Madini,
Ufugaji, Usafirishaji, Uvuvi na Kilimo.
Aliongeza kuwa serikali
inatambua na kuthamini mchango wa ushirika wa Taifa katika kuyafikia malengo ya
milenia na malengo mbalimbali ya nchi kama uimarishwaji wa sekta ya viwanda,
Kilimo, uvuvi na biashara na kuchangia katika ongezeko la kipato kwa wananchi
na hatimaye kuchangia katika ukuaji wa pato la Taifa.
Tarehe 7 Julai 2018 Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Kassim M. Majaliwa (Mb) alimkabidhi tuzo ya heshima Waziri wa Kilimo Mhe. Dkt
Charles Tizeba kwa kazi kubwa aliyoifanya na anayoendelea kuifanya katika
kuimarisha sekta ya ushirika nchini katika kipindi cha muda mfupi wa miaka
miwili tangu alipoteuliwa kuhudumu katika nafasi hiyo.
Tuzo hiyo imetolewa wakati wa
kilele cha siku ya ushirika Duniani na Mhe. Waziri Mkuu kwa niaba ya
wanaushirika ambao ndio wameandaa Tuzo hizo ikiwa ni heshima na Utumishi mkubwa
kwa Waziri Tizeba katika kipindi kifupi kwa kurudisha imani ya ushirika kwa
wananchi waliokuwa wamepoteza matumaini kutokana na baadhi ya viongozi
wabadhilifu kujinufaisha na Ushirika kinyume na utaratibu.
Tuzo hiyo kwa Dkt Tizeba
inatolewa wakati ambapo ni siku moja pekee imepita tangu Waziri huyo wa kilimo
kutangaza Kiama kwa viongozi na baadhi ya watendaji wa vyama vya ushirika
wanaofanya ubadhilifu wa Mali za wanaushirika kwa manufaa yao pekee pasina
kuwanufaisha wanachama wote.
Kwa msisitizo mkubwa Julai 6,
2018 Mhe. Dkt Tizeba alieleza kwa ukali kuhusu ubadhilifu wa rasilimali za
ushirika unaofanywa na baadhi ya viongozi na watendaji wa vyama vya ushirika
kwenye hafla ya ufunguzi wa Kongamano la Kitaifa la wanaushirika Tanzania
linalofanyika kwa siku mbili katika uwanja wa Furahisha Jijini Mwanza.
Katika mkutano huo Tuzo hiyo ya kuimarisha sekta ya ushirika nchini pia ilitolewa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli sambamba na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Kassim M. Majaliwa (Mb) kwa usimamizi madhubuti wa ushirika na wenye mafanikio makubwa.
GRARAMA ZA UENDESHAJI WA VYAMA VIKUU VYA USHIRIKA KUDHIBITIWA, DKT TIZEBA AIELEZA HALMASHAURI KUU YA CCM MKOA WA KAGERA
Waziri
wa Kilimo Mhe. Dkt Charles Tizeba akitoa ufafanuzi kuhusu sintofahamu ya
biashara ya kahawa wakati akizungumza kwenye mualiko maalumu na wajumbe wa
Halmshauri kuu ya Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Kagera kwenye Hoteli ya Bukoba
Coop, 12 Julai 2018.
Malalamiko ya muda mrefu ya
wakulima yaliyokuwepo kwamba ushirika unatoa bei ndogo, sasa yamepatiwa
muarobaini baada ya serikali kupitia kwa kina gharama za uendeshaji na
uongezaji thamani kwa zao la kahawa kwa Vyama vikuu vya ushirika Mkoani Kagera.
Serikali imepiga marufuku kwa
vyama hivyo vya ushirika kutoza zaidi ya shilingi 490 kwa kilo moja ya Kahawa
ya maganda kama gharama za uendeshaji na uongezaji thamani, Awali maainisho ya
gharama hizo yalikuwa ni makubwa ambapo kiasi cha shilingi 1350 kwa kilo moja
ya Kahawa ya maganda ilianishwa kama gharama za uendeshaji.
Waziri wa Kilimo Mhe. Dkt
Charles Tizeba alieleza agizo hilo Tarehe 12 Julai 2018 wakati akizungumza na
wajumbe wa Halmshauri kuu ya Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Kagera kwenye Hoteli
ya Bukoba Coop ambapo miongoni mwa ajenda ya kikao hicho ilikuwa ni kujadili
kuhusu soko la Kahawa na uendeshaji wa ushirika.
Dkt Tizeba amewaeleza wajumbe
hao kuwa amepiga marufuku hiyo kufuatia malalamiko ya wadau wa Kahawa Mkoani
Kagera ambapo gharama hizo zilionekana kuwa kubwa ukilinganisha na gharama
halisi.
"Ndugu zangu wajumbe wa
Halmashauri kuu ya CCM inawezekanaje shilingi mia mbili inatozwa kama
ushuru wa chama kikuu, na shilingi mia mbili tena inatozwa kama ushuru wa chama
cha msingi, ni nani anaweza kukupa faida namna hii sasa rasmi ushuru huu
tumeupunguza kama nilivyoeleza" Alikaririwa Mhe Tizeba
Aliongeza kuwa swala la ushirika
ni utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi ambayo ndiyo mkataba kati ya
wananchi na serikali katika kipindi cha miaka mitano kuanzia 2015-2020 inatoa
maelekezo ya kuwezesha upatikanaji wa Masoko ya Mazao ya Kilimo kwa
kuviimarisha na kuviwezesha vyama vya ushirika kuwa na uwezo wa kutafuta masoko
ya mazao ya wakulima ya ndani na nje kwa kuweka mfumo madhubuti wa ukusanyaji,
uchambuzi na uenezaji wa taarifa za Masoko na kutoa elimu juu ya uongezaji
thamani na biashara kwa imani kubwa kwamba ndicho chombo pekee kitakacho
mkwamua mkulima na changamoto anazo kabiliana nazo kwenye Kilimo na masoko
ikiwa ni pamoja na kujiondoa katika umasikini.
Aidha, waziri Tizeba alisema
kuwa ameagiza Wakulima waliouza kiasi kidogo cha kahawa wasilipwe kwa utaratibu
wa benki ili kuepusha usumbufu badala yake kwa wale wakulima waliolima hekari
nyingi na malipo yao yatahusisha kiasi kikubwa cha fedha ndio walipwe kwa
utaratibu wa njia ya Benki.
Aliongeza kuwa mafanikio ya
Kilimo nchini hususani zao la kahawa ni lazima kuuza kupitia Vyama vya msingi
vya ushirika ambapo ilani ya Chama Cha Mapinduzi sura ya pili kipengele cha 21
(n) inaeleza jinsi sheria ilivyofanyiwa marekebisho na kuanzisha sheria mpya
ambayo imeanzisha tume huru ya ushirika ili kuwa na tija kwa wakulima kwa ajili
ya kuwapatia faida kubwa ya kuuza kupitia ushirika.
Aidha, Dkt Tizeba aliwaeleza
wajumbe hao kuwa vyama vya ushirika havipaswi kuendeleza mazoea ya kujiwekea
gharama bila kwanza kutazama kipato cha mkulima huku akieleza kuwa amewaelekeza
wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi ambapo Wilaya zao zinalima Kahawa kote nchini
kufuatilia kwa karibu mwenendo wa masoko ya Kahawa kuanzia inavyokusanywa mpaka
wakati inapouzwa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa
Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Kagera Bi Costansia Buhiye alimpongeza Waziri huyo
wa kilimo kwa kujibu kero namba 10 ya kikao cha Halmshauri kuu ya CCM kuhusu
wasiwasi wa bei ya kahawa na namna ya uendeshaji wa ushirika.
Buhiye alimpongeza Waziri huyo
kwa kutatua kadhia mbalimbali za wakulima wa Kahawa katika ziara yake ya siku
tatu Mkoani humo huku akieleza kuwa ana imani kubwa kwamba wajumbe hao
watatembea kifua mbele endapo wakulima wao watapatiwa bei nzuri.
AGIZO KWA CRDB KULIPA
FEDHA ZA USHIRIKA (KCU)
Waziri wa Kilimo Mhe. Dkt Charles Tizeba akisisitiza jambo wakati akizungumza na wadau wa Kahawa Wilayani Muleba wakati wa ziara ya siku tatu ya kikazi Mkoani Kagera,12 Julai 2018.
Katika hatua nyingine Benki ya
CRDB imetakiwa kulipa haraka malipo ya fedha za Ushirika za Chama Kikuu cha
Kagera (KCU) kulingana na hatma ya kesi iliyokuwa mahakamani mwaka 2003 ambapo
wakulima walikuwa wakikatwa kiasi cha shilingi 10 kwa kila kilo moja ya Kahawa
ili kujenga mfuko wa Mazao kwa miaka mitatu kuanzia mwaka 1990 hadi 1993.
Waziri wa Kilimo Mhe. Dkt Charles
Tizeba tarehe 12 Julai 2018 alitoa agizo hilo wakati akizungumza kwenye mkutano
uliowakutanisha wadau wa Kahawa Wilayani Muleba ikiwa ni siku ya tatu ya ziara
ya kikazi mkoani Kagera na kuhudhuriwa pia na Waziri wa Viwanda, Biashara na
Uwekezaji Mhe Charles Mwijage.
Swala la madai hayo katika
mkutano huo liliibuka baada ya baadhi ya wakulima kuonyesha vitabu vya mfuko
huo ambapo makato hayo ya shilingi 10 kwa kilo kwa kipindi cha miaka mitatu
jinsi ambavyo yalikuwa yakifanyika.
Madai ya wakulima hao yamekuwa
yakilalamikiwa kwa kipindi kirefu na kuchangia kwa kiasi kikubwa kupungua kwa
imani ya wakulima kwa chama kikuu cha ushirika Kagera (KCU).
Chanzo cha kesi hiyo ni baada ya
Benki ya CRDB kuzuia fedha za malipo yaliyotokana na mauzo ya Kahawa ili
kulipia deni la msimu wa mwaka 1997/1998.
Hukumu ya kesi iliyotolewa
tarehe 28 Octoba 2009 na mfuko wa Mazao wa wakulima Mkoani Kagera kupewa
tahfifu ulizoomba ambapo tangu wakati huo Benki ya CRDB iliweza kulipa fedha za
mfuko ilizochukua kiasi cha shilingi milioni 525 na fedha zilizobaki bado
hazijalipwa kwa kisingizio cha kuwa na nia ya kukata rufaa ambayo bado
haijakatwa ambapo hata hivyo hawawezi kukata rufaa kutokana na muda kuwa
umepita.
Dkt Tizeba alisema kuwa Jumla ya
madai hayo sambamba na riba ni shilingi Bilioni sita za kitanzania huku
akisisitiza kuwa Benki hiyo ya CRDB inapaswa kuwa mfano wa Benki zingine nchini
hivyo kushindwa kuwalipa wakulima kwa wakati ni kushindwa kwenda na serikali ya
awamu ya tano inayoongozwa na Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt
John Pombe Magufuli.
Wakati huo huo Waziri Tizeba
aliagiza Halmashauri zote nchini zinazolima Kahawa kusimamia ukusanyaji wa
Kahawa kwenda vyama vya Msingi (AMCOS) kwani kutokana na usimamizi huo ndipo utapatikana
kwa wingi ushuru wa Halmshauri.
KIWANDA CHA SUKARI
KAGERA CHAAGIZWA KUACHA URASIMU KATIKA KUUZA SUKARI WANAYOZALISHA
Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba
akikagua uzalishaji wa sukari wakati walipotembelea kiwanda cha Sukari Kagera
wakiwa kwenye ziara ya siku tatu ya kikazi Mkoani humo iliyoanza Jana 10 Julai
2018, 11 Julai 2018.
Wawaziri wa sekta ya Kilimo Mhe
Dkt Charles Tizeba na waziri wa sekta ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe
Charles Mwijage waliutaka Uongozi wa kiwanda cha Sukari Kagera kuacha urasimu
katika mfumo wa uuzaji wa Sukari wanayozalisha badala yake kuingiza mtaani kwa
wingi Sukari kwa wananchi ili kuepuka kadhia ya upungufu wa huduma hiyo muhimu
katika jamii.
Agizo hilo lilitolewa wakati
wakizungumza na uongozi wa kiwanda hicho tarehe 11 Julai 2018 walipotembela
kiwanda hicho cha Sukari wakiwa kwenye ziara ya siku tatu ya kikazi Mkoani humo.
Mawaziri hao kwa kauli moja walitoa
siku 14 kwa kiwanda hicho kuongeza kasi ya uzalishaji kutoka uzalishaji wa
Sukari kwa Tani 350-360 kwa siku ili kufikia walau Tani 450 mpaka 500 kwa siku
kwani kufanya hivyo wataimalisha uwezo wa Sukari kupatikana kwa wingi kwa
wananchi hivyo kuondoa usumbufu wa gharama katika ununuzi wa bidhaa hiyo.
Aidha, Mawaziri hao walitoa
kalipio Kali kwa uongozi wa kiwanda hicho kwa kuwa na mawakala wachache wa
usambazaji wa sukari jambo ambalo linapelekea ushindani wa kibiashara kuwa
mchache mbinu inayopelekea Sukari kuuzwa kwa gharama isiyokuwa rafiki kwa
watumiaji (Wananchi).
Walisema kuwa ndani ya muda mfupi
uongozi wa kiwanda hicho unapaswa kutathmini upya namna ya kuongeza Uwekezaji
ili kurahisisha huduma za wananchi ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya
uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2015-2020 hatimaye kufikia malengo ya
Dira ya Taifa ya Maendeleo ifikapo mwaka 2025.
Dkt Tizeba alisema kuwa kumekuwa
na uingizaji wa Sukari kwa magendo kutoka nje ya nchi kwa sababu Viwanda vya
Sukari ndani ya nchi vimefungia sukari kwenye magodauni bila kuingiza sokoni
kwa wingi kuwafikia watumiaji.
Pia, alisema kuwa wataalamu wa
kiwanda cha Sukari wanapaswa kutoa elimu ya muwa kwa umma ili kuona umuhimu wa
uzalishaji wa zao hilo sambamba na kushirikiana na wakulima wadogo zaidi ya 490
katika vijiji vya jirani na kiwanda hicho.
Waziri wa Viwanda, Biashara na
Uwekezaji Mhe Charles Mwijage alisema kuwa serikali inatazama namna bora zaidi
ya kukuza takwimu za uzalishaji wa Sukari nchini hivyo Viwanda vya Sukari
vinapaswa kuunga mkono juhudi hizo kwa kuchochea Uwekezaji ili kuongeza tija
katika uzalishaji.
Pia alisisitiza kuwa serikali ya
awamu ya tano inayoongozwa na Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.
John Pombe Magufuli haitasita kuvifungia Viwanda vyote vitakavyobainika kukiuka
taratibu, sheria na kanuni za nchi katika utekelezaji wa majukumu yake.
TAASISI ZA UTAFITI MARUKU-BUKOBA ZAPIGWA MSASA
Waziri wa Kilimo Mhe Dkt
Charles Tizeba mbegu za maharege zinazofanyiwa utafiti na Taasisi ya utafiti wa kilimo
Tanzania (TARI) kituo cha Maruku, wakati akiwa katika ziara ya kikazi katika kijiji cha Butairuka
Kata ya Maruku Wilayani Bukoba vijijini, 13 Julai 2018.
Waziri wa Kilimo Mhe Dkt
Charles Tizeba mbegu za maharege zinazofanyiwa utafiti na Taasisi ya utafiti wa kilimo
Tanzania (TARI) kituo cha Maruku, wakati akiwa katika ziara ya kikazi katika kijiji cha Butairuka
Kata ya Maruku Wilayani Bukoba vijijini, Leo 13 Julai 2018.
Katika
ziara ya kikazi ya Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba ya siku tatu mkoani
Kagera alizungumza na uongozi wa Taasisi ya utafiti wa kilimo Tanzania (TARI)
kituo cha Maruku, Taasisi ya utafiti wa kahawa (TACRI) na kuwataka watafiti hao
kuongeza ufanisi katika utaalamu wao ili kuwanufaisha wakulima kote nchini
kwani kwa sasa Benki ya Tafiti zilizopo hazijatumika ipasavyo.
Alisema, Wataalamu wa utafiti
wanapaswa kufanya vizuri pia katika eneo la kutangaza tafiti zao ikiwemo
Kuongeza ujuzi katika Utafiti wa Mazao mbalimbali ikiwa ni pamoja na zao la
kahawa ili kuongeza uwezo wa uzalishaji wa miche.
Tizeba alisema hayo tarehe 13
Julai 2018 wakati alipokuwa akizungumza kwenye kikao kazi kilichowakutanisha
watendaji wa taasisi hizo za utafiti sambamba na uongozi wa chuo cha mafunzo ya
Kilimo MARUKU katika kijiji cha Butairuka Kata ya Maruku Wilayani Bukoba
vijijini.
Waziri huyo wa kilimo aliwasihi
watafiti hao Kuendelea kufanya juhudi kubwa kuandika miradi mbalimbali (Reseach
Proposals) kwa ajili ya kusaidia shughuli za uendelezaji wa utafiti kwani
bajeti ya serikali pekee haiwezi kutosha kukamilisha kila changamoto
zinazowakabili.
Alisema wataalamu hao wanapaswa
kufanya tafiti kwa kuendana na matakwa ya sekta ya kilimo na serikali ya
awamu ya tano inayoongozwa na Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt
John Pombe Magufuli ili kuongeza tija katika uzalishaji wa Kahawa nchini
sambamba na Mazao mengine.
Aliwasihi kuongeza ushirikiano
ili kuendelea na utafiti kuhusu njia bora za uzalishaji mazao, urutubishaji
udongo, mfumo wa usambazaji wa teknolojia, masoko yenye tija, tathmini ya
uenezaji wa teknolojia na mchango wa matokeo ya utafiti katika kuboresha hali
ya maisha ya wananchi na uchumi wa taifa kwa ujumla.
Alisema kuwa kituo cha utafiti
wa kilimo kinapaswa kuendelea na juhudi za uzalishaji wa mbegu bora za mazao
mbalimbali kama vile maharage, viazi vitamu, muhogo na mengineyo.
Kituo cha utafiti wa kilimo cha
Maruku (TARI-MARUKU) ni kati ya vituo viwili vya utafiti wa kilimo katika Kanda
ya ziwa ambapo makao makuu yake yapo Ukiriguru-Mwanza ambapo kinatoa mafunzo na
ushauri kwa wakulima na wadau mbalimbali wa kilimo juu ya teknolojia mbalimbali
za kilimo.
Katika hatua nyingine Waziri
Tizeba amemuagiza Mkuu wa chuo cha mafunzo ya kilimo Maruku Ndg Laurent Mathew
Luhembe ndani ya mwaka mmoja kutatua changamoto ya ukosefu wa bweni la chakula.
Aliongeza kuwa chuo hicho
kinapaswa kubuni mbinu mbadala za mapato ikiwa ni pamoja na kujenga kitalu
nyumba (Green House) kwani itasaidia kuongeza kipato mahususi na hatimaye chuo
kujiendesha badala ya kutaka changamoto zote zitatuliwe na serikali.
Aidha,Taasisi hizo za utafiti
ikiwa ni pamoja na Chuo cha Maendeleo ya kilimo Maruku zimetakiwa kuhakikisha
wanatunza ardhi yao ili kuondosha hofu ya uvamizi wa maeneo.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment