Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya chakula Bi Vumilia L. Zikankuba (Kushoto) akimuongoza Naibu Waziri wa kilimo Mhe Omary Mgumba (Mb) kutembelea maghala ya hifadhi ya mahindi mara baada ya kutembelea Ofisi za wakala zilizopo Mtaa wa Relini-Kizota nje kidogo ya Manispaa ya Dodoma, Jana 17 Julai 2018.(Picha Zote Na Mathias Canal-NFRA)
Naibu Waziri wa kilimo Mhe Omary Mgumba (Mb) akisisitiza jambo wakati akizungumza na watumishi wa wakala wa Taifa wa hifadhi ya Chakula mara baada ya kutembelea Ofisi za wakala zilizopo Mtaa wa Relini-Kizota nje kidogo ya Manispaa ya Dodoma, Jana 17 Julai 2018.
Naibu Waziri wa kilimo Mhe Omary Mgumba (Mb) akikagua eneo litakalojengwa Vihenge vya Kisasa Kanda ya Dodoma mara baada ya kuzungumza na watumishi wa wakala wa Taifa wa hifadhi ya Chakula ikiwa ni ziara yake ya kwanza kutembelea Ofisi za wakala zilizopo Mtaa wa Relini-Kizota nje kidogo ya Manispaa ya Dodoma, Jana 17 Julai 2018.
Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya chakula Bi Vumilia L. Zikankuba akitoa taarifa ya NFRA mbele ya Naibu Waziri wa kilimo Mhe Omary Mgumba (Mb) mara baada ya kutembelea Ofisi za wakala zilizopo Mtaa wa Relini-Kizota nje kidogo ya Manispaa ya Dodoma, Jana 17 Julai 2018.
Naibu Waziri wa kilimo Mhe Omary Mgumba (Mb) akikagua vifaa vitakavyotumika kwa ajili ya ujenzi wa Vihenge vya Kisasa Kanda ya Dodoma mara baada ya kuzungumza na watumishi wa wakala wa Taifa wa hifadhi ya Chakula ikiwa ni ziara yake ya kwanza kutembelea Ofisi za wakala zilizopo Mtaa wa Relini-Kizota nje kidogo ya Manispaa ya Dodoma, Jana 17 Julai 2018.
Na Mathias Canal-NFRA, Dodoma
Maafisa ugani katika
ngazi zote za utendaji wametakiwa kuwa na mashamba ya mfano ili kuwasaidia
wakulima kwa nadharia kupitia mashamba yao jambo litakalopelekea wakulima
kufikia uzalishaji wenye tija na kuimarisha kipato chao ikiwa ni pamoja na
kukuza uchumi wa nchi.
Agizo hilo limetolewa jana 17
Julai 2018 na Naibu waziri wa kilimo Mhe Omary Mgumba (Mb) wakati akizungumza na watumishi wa wakala wa Taifa wa hifadhi
ya Chakula akiwa katika ziara ya kikazi ya kutembelea taasisi za umma ili
kujionea namna ya uendeshaji na utendaji wa taasisi hizo.
“Tumekuwa na maafisa ugani kila kona nchini lakini hawana
hata heka moja ya mashamba, sasa tunategemea wakulima wetu wajifunze vipi
kupitia wataalamu wetu ambao tumewaajiri, hivyo ili kuwa na tija katika
uzalishaji wa mazao kwa kutumia mbinu bora za kilimo cha kisasa ni lazima
maafisa ugani kuwa na maeneo ya kulima ambayo yatatumika kama mashamba darasa”
Alikaririwa Mhe Mgumba
Alisema pamoja na kuwepo kwa wataalamu hao wa
kilimo bado uzalishaji wa mazao mbalimbali nchini yakiwemo mazao ya chakula na
biashara si wa kuridhisha ambapo wakulima wanalima na kupanda pasina hata
kufuata hatua za kitaalamu.
Mhe Mgumba aliongeza
kuwa lengo la Serikali kusambaza Maafisa Ugani kwenye Halmashauri mbali
mbali nchini ilikuwa kuwasaidia wakulima waweze kufanya
Kilimo kwa Ufanisi na kuongeza mavuno lakini imekuwa kinyume maafisa ugani
wanajifungia ofisini badala ya kwenda shambani walipo wakulima.
Naibu Waziri huyo wa
kilimo amepongeza mradi wa ujenzi wa maghala na vihenge vya kisasa huku akisema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano
inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe
Magufuli inaendelea na utekelezaji wa mkakati wa kuwanufaisha wakulima kupitia
kilimo sambamba na kuimarisha bei ya mazao yao.
Alisema Serikali imefungua mipaka na inaendelea na jitihada za
kutafuta masoko ya nje pamoja na kuboresha miundombinu ya kuhifadhi chakula kwa
kujenga maghala na vihenge vya kisasa katika maeneo mengine yenye uzalishaji
mkubwa wa chakula.
Akitoa taarifa ya mradi huo wa
kuongeza uwezo wa kuhifadhi, Kaimu
Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya chakula Bi Vumilia L. Zikankuba alisema
kuwa mradi huo pindi utakapokamilika utafungua fursa kubwa kwa wakulima nchini
kwani uwezo wa kuhifadhi wa Wakala wa Taifa wa Kuhifadhi Chakula utakuwa mara
mbili ya uwezo wa sasa yaani kutoka tani 251,000 hadi tani 501,000 huku
ikitarajiwa kufikia Tani 700,000 kufikia mwaka 2025.
Bi Vumilia alieleza kuwa
Mikataba ya mradi wa kuongeza uwezo wa kuhifadhi chakula, ilisainiwa na kuanza
kazi tarehe 09 Desemba 2017 kati ya (NFRA) na makampuni mawili toka nchini
Poland ambayo ni Feerum S.A na Unia Araj Realizacje Sp.o.o. Aidha, mradi huo
utatekelezwa kwa gharama ya Dola za kimarekani milioni 55 na unatarajiwa
kukamilika ndani ya kipindi cha miezi kumi na nane (18) kuanzia mwezi Mei 2018.
Bi Zikankuba, aliongeza kuwa Wakala
wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula unamiliki maghala ya kuhifadhi nafaka 34 yenye
uwezo wa jumla ya Tani 251,000. Uwezo huu wa sasa wa maghala hautoshelezi
mahitaji ya dharula ya chakula kwa mfululizo wa miezi mitatu kwa akiba isiyo
pungua Tani 700,000, hivyo kupelekea uhitaji wa kuongeza uwezo wa uhifadhi.
MWISHO.
0 comments:
Post a Comment