Wednesday, July 18, 2018

DKT TIZEBA AMALIZA MZIZI WA FITINA, KERO YA BIASHARA YA KAHAWA YAPATIWA UFUMBUZI

Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe Charles Mwijage wakijadili jambo wakati walipotembelea kiwanda cha Sukari Kagera wakiwa kwenye ziara ya siku tatu ya kikazi Mkoani humo iliyoanza.

Na Mathias Canal-WK, Kagera

Waziri wa kilimo Mhe. Dkt Charles Tizeba (Mb) amekamilisha ziara ya kikazi ya siku tatu Mkoani Kagera iliyoanza 10 Julai 2018 hadi 13 Julai 2018 kwa kutembelea katika Wilaya tano za Bukoba, Kyerwa, Karagwe, Missenyi, na Muleba ikiwa ni sehemu ya  utekelezaji wa maagizo ya Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli aliyoyatoa wakati akiwaapisha viongozi mbalimbali Ikulu Jijini Dar es salaam tarehe 2 Julai 2018 na kuitaka Wizara ya Kilimo kufuatilia kwanini wakulima wa zao la Kahawa wanacheleweshewa malipo yao sambamba na kujua kwanini wakulima wanauza Kahawa yao nchini Uganda na endapo kama kuna mnunuzi wa kahawa kwa bei nzuri kutoka nchini humo aletwe Tanzania kunuua.

Baada ya agizo la Rais Magufuli, Waziri huyo wa Kilimo Mhe Tizeba alimuagiza Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Omary Mgumba (Mb) kufanya ziara ya siku tatu kuanzia tarehe 4 Julai 2018 mpaka 6 Julai 2018 Mkoani Kagera ili kubaini changamoto za uuzaji wa kahawa ambapo pamoja na mambo mengine alibaini changamoto zinazowakabili wakulima hao na hatimaye kucheleweshewa fedha ni pamoja na mikopo ya vyama vikuu vya ushirika KCU na KDCU.

Tarehe 6 Julai 2018 Mhe Tizeba aliitisha kikao kazi kilichofanyika kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza na kuhudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa Halmashauri za Mkoa wa Kagera, Maafisa kilimo na ushirika, pamoja na wakaguzi wa Pamba ili kupokea taarifa ya kile alichobaini Waziri Mgumba katika ziara yake hiyo.

Kumalizika kwa kikao hicho kulimlazimu Waziri Tizeba kuzuru Mkoa Kagera ili kutatua changamoto zinazowakabili wakulima ambapo pamoja na mambo mengine alikutana na makundi mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupokea taarifa Mkoa huo iliyowasilishwa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salum Kijuu kuhusu sekta ya Kilimo hususani zao la kahawa, Kukutana na wadau wa kahawa, kutembelea vyama vya msingi, sambamba na kukutana na wadau wa Kahawa na viwanda vinavyokoboa Kahawa.

MARUFUKU YA KUUZA BUTURA NA BIASHARA YA MAGENDO

Waziri wa Kilimo Mhe. Dkt Charles Tizeba akieleza maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi wakati akizungumza na wadau wa zao la kahawa kwenye mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Isingiro Wilayani Kyerwa

Akizungumza na wadau wa zao la kahawa 10 Julai 2018 kwenye mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Isingiro Wilayani Kyerwa Waziri wa Kilimo Mhe. Dkt Charles Tizeba alikemea vikali biashara ya kuuza Kahawa nje ya nchi pasina kufuata utaratibu wa kisheria (magendo) hivyo kwa mwananchi atakayebainika kuendelea na biashara hiyo atachukuliwa hatua Kali za kisheria ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani.

Agizo hilo lilihusisha pia zuio la wananchi kuuza kahawa mbichi ingali bado shambani ikiwa haijakomaa (Butura) kwani kufanya hivyo ni kudhoofisha na kuzorotesha juhudi za muda mrefu alizotumia mkulima wa kahawa na kumkosesha mapato stahiki.

Alisema serikali itajitahidi kutafuta bei nzuri ya zao la kahawa ndani na nje ya Afrika Mashariki ili wananchi wapate faida na tija ya Kilimo huku akieleza kuwa wakulima wa kahawa kote nchini hawawezi kuona mafanikio ya Kilimo hicho kwa kuendeleza biashara ya magendo sambamba na biashara ya kahawa mbichi ikiwa shambani (Butura).

Sambamba na hayo pia Waziri wa Kilimo Mhe Tizeba amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa Ndg Shadrack Mhagama kukamilisha haraka iwezekanavyo kiwanda cha kukoboa kahawa cha Omkagando kilichozinduliwa na Mwenge wa Uhuru tangu mwaka 2016 kwa gharama za serikali lakini mpaka sasa kimeshindwa kuendekezwa.

ZIARA YA WAZIRI WA BIASHARA WA UGANDA ALIPOZURU TANZANIA YABAINISHA HAKUNA BEI NZURI YA KAHAWA NCHINI UGANDA

Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba akisalimiana na Waziri wa biashara na ushirika nchini Uganda Mhe Fredric Ngobi Gume muda mchache kabla ya kuanza kwa mkutano wa mawaziri wa nchi hizo mbili, mkutano uliohudhuriwa pia Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe Charles Mwijage
Kikao kazi
Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba akisisitiza jambo wakati wa mkutano na Waziri wa biashara na ushirika nchini Uganda Mhe Fredric Ngobi Gume (Kushoto), Mwingine ni Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe Charles Mwijage (Katikati).

Imebainika kuwa bei ya uuzaji wa Kahawa nchini Uganda haina tofauti kubwa na bei ambayo ingepatikana nchini Tanzania endapo wakulima wangeuza Kahawa zao kwenye soko la awali jambo ambalo linawatoa wasiwasi wakulima wa Kahawa nchini waliokuwa wakidanganywa kuwa bei ya Uganda ni kubwa na yenye tija kwa wakulima kuliko hapa nchini.

Kilogramu moja ya Kahawa ya maganda nchini Uganda inanunuliwa kwa shilingi 2000 ya Uganda sawa na Shilingi 1400 za Kitanzania (exchange rate 1.7) kwa mfano hapa nchini Tanzania kwa wiki iliyopita ambayo mnada wake umefanyika Mjini Moshi tarehe 12 Julai 2018 bei ya Kahawa ya Kagera ya chama kikuu cha ushirika (KCU) iliuzwa kwa kilo moja ya maganda kwa wastani wa ni Shilingi 1460 ya bei elekezi ya chini ya kila wiki (Indicative price) inayotolewa na Bodi ya Kahawa kulingana na bei ya Kahawa katika soko la dunia. 

Hata hivyo, wakulima wa Tanzania watapata zaidi kwa kuuza mnadani moja kwa moja na kuachana na bei ya shambani kwa kutumia ushirika wao ambapo bei ya chini inayopatikana ni wastani wa Shilingi 1900 kabla ya gharama za uendeshaji, Kwa kuuza mnadani mkulima anapata bei kutokana na Ubora wa Kahawa yake na ikiwa kwenye madaraja na hivyo kutoa motisha kwa wakulima kuzalisha Kahawa bora kuliko kuuza ikiwa ghafi.

Hayo yalibainishwa tarehe 11 Julai 2018 na Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba wakati akizungumza na wadau wa biashara ya Kahawa katika ukumbi wa Happiness Hoteli uliopo katika eneo la Mtukula Wilayani Misenyi muda mchache baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Biashara na Ushirika nchini Uganda Mhe Fredrick Ngobi Gume katika mkutano uliohudhuriwa pia na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe Charles Mwijage.

"Ndugu zangu kuna jambo hamlifahamu wale wanaosema Uganda bei ya Kahawa ni nzuri kuliko Tanzania wanawadanganya hakuna bei nzuri Kule kinachofanya watu kupeleka Kahawa Uganda ni kutokana na mikopo wanayokopeshana isiyo rasmi (Butura) hivyo makubaliano ya kurejesha mkopo yanakuwa na masharti magumu yanayowataka wakulima wa Kahawa nchini kulipa madeni kwa kupeleka Kahawa sio fedha" Alisisitiza Dkt Tizeba wakati akizungumza na wadau wa Kahawa eneo la Mtukula Wilayani Misenyi

Waziri wa biashara na ushirika nchini Uganda Mhe Fredric Ngobi Gume alimuhakikishia mwenyeji wake kuwa biashara ya Kahawa nchini humo ina changamoto sawa katika nchi zote mbili kwa kuwa swala la mikopo isiyo rasmi inayowanyonya wakulima (Butura) nchini Uganda ipo kwa kiwango cha juu kiasi kwamba aliomba kuja nchini Tanzania kuanzia tarehe 16-19 Julai 2018 kwa miadi maalumu kwa minajili ya kujifunza kuhusu namna bora kuendesha ushirika na kuanzisha mfumo wa stakabadhi ghalani.

Waziri Gume alisema kuwa serikali ya Uganda inayoongozwa na Rais wa nchi hiyo Mhe Yoweri Kaguta Museveni itaendeleza ushirikiano na serikali ya Tanzania inayoongozwa na Mhe Rais Dkt John Pombe Magufuli hivyo panapohitajika ushirikishwaji katika biashara hususani kwenye sekta ya Kilimo watakuwa na msimamo wa pamoja.

SERIKALI KUPAMBANA NA WABADHIRIFU KWENYE VYAMA VYA USHIRIKA 

Waziri wa Kilimo Mhe. Dkt Charles Tizeba akitoa salamu za Wizara ya Kilimo kwa Waziri Mkuu wakati wa kilele cha siku ya ushirika Duniani kwenye dhifa iliyofanyika katika uwanja wa Furahisha Jijini Mwanza. Tarehe 7 Julai 2018
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Kassim M. Majaliwa (Mb) akimkabidhi tuzo ya heshima Waziri wa Kilimo Mhe. Dkt Charles Tizeba kwa kuimarisha sekya ya ushirika nchini wakati wa kilele cha siku ya ushirika Duniani kwenye dhifa iliyofanyika katika uwanja wa Furahisha Jijini Mwanza. Tarehe 7 Julai 2018

Serikali ilitangaza Kiama kwa viongozi na baadhi ya watendaji wa vyama vya ushirika waofanya ubadhilifu wa Mali za ushirika kwa manufaa yao pekee pasina kuwanufaisha wanachama wote.

Imeelezwa kuwa ubadhilifu wa rasilimali za ushirika unaofanywa na baadhi ya viongozi na watendaji wa vyama vya ushirika umekuwa ni tatizo sugu na hata kuwakatisha tamaa baadhi ya wananchi kujiunga na vyama hivyo.

Kalipio kwa wabadhilifu hao lilitolewa na Waziri wa Kilimo Mhe. Dkt Charles Tizeba tarehe 6 Julai 2018 wakati wa hafla ya ufunguzi wa Kongamano la Kitaifa la wanaushirika Tanzania linalofanyika katika uwanja wa Furahisha Jijini Mwanza ikiwa ni siku chache kabla ya kuanza ziara ya kikazi Mkoani Kagera.

Kongamano hilo la Siku mbili liliambatana na maonesho ya bidhaa na shughuli zinazofanywa na vyama hivyo vya ushirika kote nchini ambapo wanachama walipata fursa ya kubadilishana uzoefu, na kujadili mafanikio na changamoto wanazokabiliana nazo katika uendeshaji wa sekta ya ushirika nchini.

Alisema, serikali inatambua kuwa ushirika ni nyenzo muhimu ya kuwasaidia wananchi katika upatikanaji wa mtaji na kuwawezesha kuunganisha nguvu zao za kiuchumi katika kujiendeleza kiuchumi.

Alisema kuwa zipo juhudi kubwa zinazofanywa na serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanahamasishwa na hatimae kujiunga kwenye vyama vya ushirika kulingana na shughuli zao za kiuchumi ili kuondoa dhana kuwa vyama vya ushirika ni kwa ajili ya Kilimo cha Mazao ya biashara ya nchi za nje.

Sambamba na hayo Mhe Tizeba aliitaka Tume ya Maendeleo ya ushirika na shirikisho la vyama vya ushirika kuendelea kuwahamasisha wananchi kuendelea kutambua umuhimu wa kujiunga katika vyama vya ushirika kulingana na shughuli za wananchi mfano ushirika wa Viwanda, Madini, Ufugaji, Usafirishaji, Uvuvi na Kilimo.

Aliongeza kuwa serikali inatambua na kuthamini mchango wa ushirika wa Taifa katika kuyafikia malengo ya milenia na malengo mbalimbali ya nchi kama uimarishwaji wa sekta ya viwanda, Kilimo, uvuvi na biashara na kuchangia katika ongezeko la kipato kwa wananchi na hatimaye kuchangia katika ukuaji wa pato la Taifa.

Tarehe 7 Julai 2018  Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim M. Majaliwa (Mb) alimkabidhi tuzo ya heshima Waziri wa Kilimo Mhe. Dkt Charles Tizeba kwa kazi kubwa aliyoifanya na anayoendelea kuifanya katika kuimarisha sekta ya ushirika nchini katika kipindi cha muda mfupi wa miaka miwili tangu alipoteuliwa kuhudumu katika nafasi hiyo.

Tuzo hiyo imetolewa wakati wa kilele cha siku ya ushirika Duniani na Mhe. Waziri Mkuu kwa niaba ya wanaushirika ambao ndio wameandaa Tuzo hizo ikiwa ni heshima na Utumishi mkubwa kwa Waziri Tizeba katika kipindi kifupi kwa kurudisha imani ya ushirika kwa wananchi waliokuwa wamepoteza matumaini kutokana na baadhi ya viongozi wabadhilifu kujinufaisha na Ushirika kinyume na utaratibu.

Tuzo hiyo kwa Dkt Tizeba inatolewa wakati ambapo ni siku moja pekee imepita tangu Waziri huyo wa kilimo kutangaza Kiama kwa viongozi na baadhi ya watendaji wa vyama vya ushirika wanaofanya ubadhilifu wa Mali za wanaushirika kwa manufaa yao pekee pasina kuwanufaisha wanachama wote.

Kwa msisitizo mkubwa Julai 6, 2018 Mhe. Dkt Tizeba alieleza kwa ukali kuhusu ubadhilifu wa rasilimali za ushirika unaofanywa na baadhi ya viongozi na watendaji wa vyama vya ushirika kwenye hafla ya ufunguzi wa Kongamano la Kitaifa la wanaushirika Tanzania linalofanyika kwa siku mbili katika uwanja wa Furahisha Jijini Mwanza.

Katika mkutano huo Tuzo hiyo ya kuimarisha sekta ya ushirika nchini pia ilitolewa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli sambamba na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Kassim M. Majaliwa (Mb) kwa usimamizi madhubuti wa ushirika na wenye mafanikio makubwa.

GRARAMA ZA UENDESHAJI WA VYAMA VIKUU VYA USHIRIKA KUDHIBITIWA, DKT TIZEBA AIELEZA HALMASHAURI KUU YA CCM MKOA WA KAGERA

Waziri wa Kilimo Mhe. Dkt Charles Tizeba akitoa ufafanuzi kuhusu sintofahamu ya biashara ya kahawa wakati akizungumza kwenye mualiko maalumu na wajumbe wa Halmshauri kuu ya Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Kagera kwenye Hoteli ya Bukoba Coop, 12 Julai 2018.

Malalamiko ya muda mrefu ya wakulima yaliyokuwepo kwamba ushirika unatoa bei ndogo, sasa yamepatiwa muarobaini baada ya serikali kupitia kwa kina gharama za uendeshaji na uongezaji thamani kwa zao la kahawa kwa Vyama vikuu vya ushirika Mkoani Kagera.

Serikali imepiga marufuku kwa vyama hivyo vya ushirika kutoza zaidi ya shilingi 490 kwa kilo moja ya Kahawa ya maganda kama gharama za uendeshaji na uongezaji thamani, Awali maainisho ya gharama hizo yalikuwa ni makubwa ambapo kiasi cha shilingi 1350 kwa kilo moja ya Kahawa ya maganda ilianishwa kama gharama za uendeshaji.

Waziri wa Kilimo Mhe. Dkt Charles Tizeba alieleza agizo hilo Tarehe 12 Julai 2018 wakati akizungumza na wajumbe wa Halmshauri kuu ya Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Kagera kwenye Hoteli ya Bukoba Coop ambapo miongoni mwa ajenda ya kikao hicho ilikuwa ni kujadili kuhusu soko la Kahawa na uendeshaji wa ushirika.

Dkt Tizeba amewaeleza wajumbe hao kuwa amepiga marufuku hiyo kufuatia malalamiko ya wadau wa Kahawa Mkoani Kagera ambapo gharama hizo zilionekana kuwa kubwa ukilinganisha na gharama halisi.

"Ndugu zangu wajumbe wa Halmashauri kuu ya CCM inawezekanaje shilingi mia mbili inatozwa kama ushuru wa chama kikuu, na shilingi mia mbili tena inatozwa kama ushuru wa chama cha msingi, ni nani anaweza kukupa faida namna hii sasa rasmi ushuru huu tumeupunguza kama nilivyoeleza" Alikaririwa Mhe Tizeba

Aliongeza kuwa swala la ushirika ni utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi ambayo ndiyo mkataba kati ya wananchi na serikali katika kipindi cha miaka mitano kuanzia 2015-2020 inatoa maelekezo ya kuwezesha upatikanaji wa Masoko ya Mazao ya Kilimo kwa kuviimarisha na kuviwezesha vyama vya ushirika kuwa na uwezo wa kutafuta masoko ya mazao ya wakulima ya ndani na nje kwa kuweka mfumo madhubuti wa ukusanyaji, uchambuzi na uenezaji wa taarifa za Masoko na kutoa elimu juu ya uongezaji thamani na biashara kwa imani kubwa kwamba ndicho chombo pekee kitakacho mkwamua mkulima na changamoto anazo kabiliana nazo kwenye Kilimo na masoko ikiwa ni pamoja na kujiondoa katika umasikini.

Aidha, waziri Tizeba alisema kuwa ameagiza Wakulima waliouza kiasi kidogo cha kahawa wasilipwe kwa utaratibu wa benki ili kuepusha usumbufu badala yake kwa wale wakulima waliolima hekari nyingi na malipo yao yatahusisha kiasi kikubwa cha fedha ndio walipwe kwa utaratibu wa njia ya Benki.

Aliongeza kuwa mafanikio ya Kilimo nchini hususani zao la kahawa ni lazima kuuza kupitia Vyama vya msingi vya ushirika ambapo ilani ya Chama Cha Mapinduzi sura ya pili kipengele cha 21 (n) inaeleza jinsi sheria ilivyofanyiwa marekebisho na kuanzisha sheria mpya ambayo imeanzisha tume huru ya ushirika ili kuwa na tija kwa wakulima kwa ajili ya kuwapatia faida kubwa ya  kuuza kupitia ushirika.

Aidha, Dkt Tizeba aliwaeleza wajumbe hao kuwa vyama vya ushirika havipaswi kuendeleza mazoea ya kujiwekea gharama bila kwanza kutazama kipato cha mkulima huku akieleza kuwa amewaelekeza wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi ambapo Wilaya zao zinalima Kahawa kote nchini kufuatilia kwa karibu mwenendo wa masoko ya Kahawa kuanzia inavyokusanywa mpaka wakati inapouzwa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Kagera Bi Costansia Buhiye alimpongeza Waziri huyo wa kilimo kwa kujibu kero namba 10 ya kikao cha Halmshauri kuu ya CCM kuhusu wasiwasi wa bei ya kahawa na namna ya uendeshaji wa ushirika.

Buhiye alimpongeza Waziri huyo kwa kutatua kadhia mbalimbali za wakulima wa Kahawa katika ziara yake ya siku tatu Mkoani humo huku akieleza kuwa ana imani kubwa kwamba wajumbe hao watatembea kifua mbele endapo wakulima wao watapatiwa bei nzuri.

AGIZO KWA CRDB KULIPA FEDHA ZA USHIRIKA (KCU)


Waziri wa Kilimo Mhe. Dkt Charles Tizeba akisisitiza jambo wakati akizungumza na wadau wa Kahawa Wilayani Muleba wakati wa ziara ya siku tatu ya kikazi Mkoani Kagera,12 Julai 2018. 

Katika hatua nyingine Benki ya CRDB imetakiwa kulipa haraka malipo ya fedha za Ushirika za Chama Kikuu cha Kagera (KCU) kulingana na hatma ya kesi iliyokuwa mahakamani mwaka 2003 ambapo wakulima walikuwa wakikatwa kiasi cha shilingi 10 kwa kila kilo moja ya Kahawa ili kujenga mfuko wa Mazao kwa miaka mitatu kuanzia mwaka 1990 hadi 1993.

Waziri wa Kilimo Mhe. Dkt Charles Tizeba tarehe 12 Julai 2018 alitoa agizo hilo wakati akizungumza kwenye mkutano uliowakutanisha wadau wa Kahawa Wilayani Muleba ikiwa ni siku ya tatu ya ziara ya kikazi mkoani Kagera na kuhudhuriwa pia na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe Charles Mwijage.

Swala la madai hayo katika mkutano huo liliibuka baada ya baadhi ya wakulima kuonyesha vitabu vya mfuko huo ambapo makato hayo ya shilingi 10 kwa kilo kwa kipindi cha miaka mitatu jinsi ambavyo yalikuwa yakifanyika.

Madai ya wakulima hao yamekuwa yakilalamikiwa kwa kipindi kirefu na kuchangia kwa kiasi kikubwa kupungua kwa imani ya wakulima kwa chama kikuu cha ushirika Kagera (KCU).

Chanzo cha kesi hiyo ni baada ya Benki ya CRDB kuzuia fedha za malipo yaliyotokana na mauzo ya Kahawa ili kulipia deni la msimu wa mwaka 1997/1998.

Hukumu ya kesi iliyotolewa tarehe 28 Octoba 2009 na mfuko wa Mazao wa wakulima Mkoani Kagera kupewa tahfifu ulizoomba ambapo tangu wakati huo Benki ya CRDB iliweza kulipa fedha za mfuko ilizochukua kiasi cha shilingi milioni 525 na fedha zilizobaki bado hazijalipwa kwa kisingizio cha kuwa na nia ya kukata rufaa ambayo bado haijakatwa ambapo hata hivyo hawawezi kukata rufaa kutokana na muda kuwa umepita.

Dkt Tizeba alisema kuwa Jumla ya madai hayo sambamba na riba ni shilingi Bilioni sita za kitanzania huku akisisitiza kuwa Benki hiyo ya CRDB inapaswa kuwa mfano wa Benki zingine nchini hivyo kushindwa kuwalipa wakulima kwa wakati ni kushindwa kwenda na serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli.

Wakati huo huo Waziri Tizeba aliagiza Halmashauri zote nchini zinazolima Kahawa kusimamia ukusanyaji wa Kahawa kwenda vyama vya Msingi (AMCOS) kwani kutokana na usimamizi huo ndipo utapatikana kwa wingi ushuru wa Halmshauri.

KIWANDA CHA SUKARI KAGERA CHAAGIZWA KUACHA URASIMU KATIKA KUUZA SUKARI WANAYOZALISHA


Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba akikagua uzalishaji wa sukari wakati walipotembelea kiwanda cha Sukari Kagera wakiwa kwenye ziara ya siku tatu ya kikazi Mkoani humo iliyoanza Jana 10 Julai 2018, 11 Julai 2018. 

Wawaziri wa sekta ya Kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba na waziri wa sekta ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe Charles Mwijage waliutaka Uongozi wa kiwanda cha Sukari Kagera kuacha urasimu katika mfumo wa uuzaji wa Sukari wanayozalisha badala yake kuingiza mtaani kwa wingi Sukari kwa wananchi ili kuepuka kadhia ya upungufu wa huduma hiyo muhimu katika jamii.

Agizo hilo lilitolewa wakati wakizungumza na uongozi wa kiwanda hicho tarehe 11 Julai 2018 walipotembela kiwanda hicho cha Sukari wakiwa kwenye ziara ya siku tatu ya kikazi Mkoani humo.

Mawaziri hao kwa kauli moja walitoa siku 14 kwa kiwanda hicho kuongeza kasi ya uzalishaji kutoka uzalishaji wa Sukari kwa Tani 350-360 kwa siku ili kufikia walau Tani 450 mpaka 500 kwa siku kwani kufanya hivyo wataimalisha uwezo wa Sukari kupatikana kwa wingi kwa wananchi hivyo kuondoa usumbufu wa gharama katika ununuzi wa bidhaa hiyo.

Aidha, Mawaziri hao walitoa kalipio Kali kwa uongozi wa kiwanda hicho kwa kuwa na mawakala wachache wa usambazaji wa sukari jambo ambalo linapelekea ushindani wa kibiashara kuwa mchache mbinu inayopelekea Sukari kuuzwa kwa gharama isiyokuwa rafiki kwa watumiaji (Wananchi).

Walisema kuwa ndani ya muda mfupi uongozi wa kiwanda hicho unapaswa kutathmini upya namna ya kuongeza Uwekezaji ili kurahisisha huduma za wananchi ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2015-2020 hatimaye kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ifikapo mwaka 2025.

Dkt Tizeba alisema kuwa kumekuwa na uingizaji wa Sukari kwa magendo kutoka nje ya nchi kwa sababu Viwanda vya Sukari ndani ya nchi vimefungia sukari kwenye magodauni bila kuingiza sokoni kwa wingi kuwafikia watumiaji.

Pia, alisema kuwa wataalamu wa kiwanda cha Sukari wanapaswa kutoa elimu ya muwa kwa umma ili kuona umuhimu wa uzalishaji wa zao hilo sambamba na kushirikiana na wakulima wadogo zaidi ya 490 katika vijiji vya jirani na kiwanda hicho.

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe Charles Mwijage alisema kuwa serikali inatazama namna bora zaidi ya kukuza takwimu za uzalishaji wa Sukari nchini hivyo Viwanda vya Sukari vinapaswa kuunga mkono juhudi hizo kwa kuchochea Uwekezaji ili kuongeza tija katika uzalishaji.

Pia alisisitiza kuwa serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli haitasita kuvifungia Viwanda vyote vitakavyobainika kukiuka taratibu, sheria na kanuni za nchi katika utekelezaji wa majukumu yake.

TAASISI ZA UTAFITI MARUKU-BUKOBA ZAPIGWA MSASA


Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba mbegu za maharege zinazofanyiwa utafiti na Taasisi ya utafiti wa kilimo Tanzania (TARI) kituo cha Maruku, wakati akiwa katika ziara ya kikazi katika kijiji cha Butairuka Kata ya Maruku Wilayani Bukoba vijijini, 13 Julai 2018.
Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba mbegu za maharege zinazofanyiwa utafiti na Taasisi ya utafiti wa kilimo Tanzania (TARI) kituo cha Maruku, wakati akiwa katika ziara ya kikazi katika kijiji cha Butairuka Kata ya Maruku Wilayani Bukoba vijijini, Leo 13 Julai 2018.

Katika ziara ya kikazi ya Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba ya siku tatu mkoani Kagera alizungumza na uongozi wa Taasisi ya utafiti wa kilimo Tanzania (TARI) kituo cha Maruku, Taasisi ya utafiti wa kahawa (TACRI) na kuwataka watafiti hao kuongeza ufanisi katika utaalamu wao ili kuwanufaisha wakulima kote nchini kwani kwa sasa Benki ya Tafiti zilizopo hazijatumika ipasavyo.

Alisema, Wataalamu wa utafiti wanapaswa kufanya vizuri pia katika eneo la kutangaza tafiti zao ikiwemo Kuongeza ujuzi katika Utafiti wa Mazao mbalimbali ikiwa ni pamoja na zao la kahawa ili kuongeza uwezo wa uzalishaji wa miche.

Tizeba alisema hayo tarehe 13 Julai 2018 wakati alipokuwa akizungumza kwenye kikao kazi kilichowakutanisha watendaji wa taasisi hizo za utafiti sambamba na uongozi wa chuo cha mafunzo ya Kilimo MARUKU katika kijiji cha Butairuka Kata ya Maruku Wilayani Bukoba vijijini.

Waziri huyo wa kilimo aliwasihi watafiti hao Kuendelea kufanya juhudi kubwa kuandika miradi mbalimbali (Reseach Proposals) kwa ajili ya kusaidia shughuli za uendelezaji wa utafiti kwani bajeti ya serikali pekee haiwezi kutosha kukamilisha kila changamoto zinazowakabili.

Alisema wataalamu hao wanapaswa kufanya tafiti kwa kuendana na matakwa ya sekta ya kilimo na serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli ili kuongeza tija katika uzalishaji wa Kahawa nchini sambamba na Mazao mengine.

Aliwasihi kuongeza ushirikiano ili kuendelea na utafiti kuhusu njia bora za uzalishaji mazao, urutubishaji udongo, mfumo wa usambazaji wa teknolojia, masoko yenye tija, tathmini ya uenezaji wa teknolojia na mchango wa matokeo ya utafiti katika kuboresha hali ya maisha ya wananchi na uchumi wa taifa kwa ujumla.

Alisema kuwa kituo cha utafiti wa kilimo kinapaswa kuendelea na juhudi za uzalishaji wa mbegu bora za mazao mbalimbali kama vile maharage, viazi vitamu, muhogo na mengineyo.

Kituo cha utafiti wa kilimo cha Maruku (TARI-MARUKU) ni kati ya vituo viwili vya utafiti wa kilimo katika Kanda ya ziwa ambapo makao makuu yake yapo Ukiriguru-Mwanza ambapo kinatoa mafunzo na ushauri kwa wakulima na wadau mbalimbali wa kilimo juu ya teknolojia mbalimbali za kilimo.

Katika hatua nyingine Waziri Tizeba amemuagiza Mkuu wa chuo cha mafunzo ya kilimo Maruku Ndg Laurent Mathew Luhembe ndani ya mwaka mmoja kutatua changamoto ya ukosefu wa bweni la chakula.

Aliongeza kuwa chuo hicho kinapaswa kubuni mbinu mbadala za mapato ikiwa ni pamoja na kujenga kitalu nyumba (Green House) kwani itasaidia kuongeza kipato mahususi na hatimaye chuo kujiendesha badala ya kutaka changamoto zote zitatuliwe na serikali.

Aidha,Taasisi hizo za utafiti ikiwa ni pamoja na Chuo cha Maendeleo ya kilimo Maruku zimetakiwa kuhakikisha wanatunza ardhi yao ili kuondosha hofu ya uvamizi wa maeneo.

MWISHO

No comments:

Post a Comment