Waziri wa nishati Mhe Medard Kalemani amepiga marufuku wafanyakazi wa shirika la umeme nchini TANESCO kuruka nyumba wakati wa uendeshaji wa zoezi la uunganishaji umeme vijijini REA
Waziri Kalemani ametoa onyo hilo akiwa wilaya ya Ilemela jijini Mwanza wakati wa uzinduzi wa zoezi la uunganishaji wa umeme katika mtaa wa Igalagala kata ya Sangabuye ambapo amekemea vitendo vinavyofanywa na wataalamu wa shirika hilo vya kuruka baadhi ya nyumba bila kuwa na sababu za msingi ikiwemo uzembe kazini na usimamizi mbovu kwa wakandarasi wanaotekeleza mradi huo kunakopelekea kuchelewa kukamilika kwa wakati kwa mradi, kuwasababishia wananchi usumbufu na mkandarasi kutokuwepo eneo la kazi.
‘… Nimepita hapa nmejionea mwenyewe baadhi ya nyumba hazina umeme na nmeletewa malalamiko ya chini chini kwamba wakandarasi na wataalamu wangu mmekuwa na sababu zisizo za lazima za kuruka baadhi ya nyumba za wananchi jambo hili nalikemea na naomba msirudie …’ Alisema
Aidha Waziri Kalemani ameelekeza kuunganishwa kwa mitaa 16 katika mpango huo wa umeme vijijini kutoka katika mitaa 56 iliyokuwa ikikosa kabisa huduma hiyo huku akiahidi kuimalizia mitaa 40 iliyobaki kwa awamu inayofuata kufuatia ombi la mbunge wa jimbo hilo Mhe Dkt Angeline Mabula huku akimsimamisha kazi technician wa mradi huo pamoja na kumpa barua ya onyo meneja wa tanesco wa wilaya hiyo inayomtaka kujieleza ni kwanini asitolewe kwenye nafasi yake kwa sababu za usimamizi mbovu wa mradi huo kabla ya kuwahakikishia umeme wananchi wa maeneo yote ya jimbo la Ilemela ifikapo mwaka 2020 na kupiga marufuku uvaaji wa tai kwa wafanya kazi wote wa shirika la umeme nchini Tanesco wawapo kazini.
Akimkaribisha Waziri huyo, mbunge wa jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula amemshukuru Rais Mhe Dkt John Magufuli kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuwaletea waTanzania maendeleo kwa kushirikiana na wasaidizi wake huku akiwaasa wananchi kuendelea kumuombea na kuunga mkono jitihada zote zinazofanywa na Serikali ya awamu ya tano katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.
Uzinduzi huo ulihudhuriwa na wataalam wa wizara ya nishati, shirika la umeme Kanda ya Ziwa, shirika la umeme mkoa wa Mwanza, mstahiki meya wa manispaa ya Ilemela na mkururgenzi wake.
' Ilemela ni yetu, tushirikiane kuijenga'
Imetolewa na
Ofisi ya mbunge
Jimbo la Ilemela
22.07.2018
0 comments:
Post a Comment