WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema
viongozi wa dini waendelee kuimarisha malezi na mafundisho ya kiroho kwa
vijana na kuepusha mmomonyoko wa maadili ili Taifa liendelee kung’ara,
kuheshimika na kusifika duniani kwa utulivu, amani na umoja.
Amesema Serikali inatambua mchango wa
madhehebu ya dini ikiwemo CCT katika kutengeneza mustakabali mwema na
ustawi wa familia kupitia mahubiri ya injili na malezi ya kiroho kwa
waamini. “Mtakubaliana nami kuwa siku zote Taifa imara msingi wake
hujengwa na familia imara.”
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Ijumaa,
Julai 5, 2019) wakati alipomwakilisha Rais Dkt. John Magufuli kwenye
Mkutano wa Halmashauri Kuu ya 53 ya Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT)
ulioambatana na harambee ya kukusanya fedha kwa ajili ya ujenzi wa
kitegauchumi cha jumuiya hiyo. Mkutano huo umefanyika jijini Dodoma.
Amesema Serikali inatambua mchango wa
malezi ya kiroho katika ustawi wa wananchi na Taifa kwa ujumla na
mafundisho yake kwani yamesaidia kujenga watumishi wa umma ambao
wamelelewa katika misingi bora ya kumcha Mwenyezi Mungu.
Waziri Mkuu amesema Serikali inaamini
kwamba watumishi wa namna hiyo watachapa kazi kwa bidii, uadilifu,
uaminifu na kupiga vita vitendo vyote vya rushwa na ubadhilifu wa mali
za umma. Serikali itaendelea kushirikiana na Taasisi za kidini kwa ajili
ya ustawi wa Taifa na watu wake.
Akizungumzia kuhusu harambee hiyo ambayo
jumla ya sh. milioni 357.35 zilipatikana, Waziri Mkuu amesema ni sehemu
ya utekelezaji wa Mkakati wa CCT wa miaka mitano (2017 – 2022) wenye
lengo la kuiwezesha CCT kujitegemea kwa kuwa na vitega uchumi vyake
ambavyo vitawawezesha kujiendesha kwa asilimia 80.
Waziri Mkuu ameipongeza CCT kwa kuanza
kuchukua hatua za kujenga uwezo wa ndani wa kujitegemea kiuchumi kwani
zinahitajika nguvu za pamoja katika kuhakikisha wanawahudumia Watanzania
na kuwaletea maendeleo.
“Kujizatiti kwa CCT katika kufikia
malengo yake ya kujitegemea kiuchumi ni muhimu katika kutimiza kusudio
na agizo la Mungu la kuwahudumia wahitaji ambao ni Watanzania lakini pia
mtakuwa mnajaliza juhudi za Serikali katika wajibu wake wa kuwahudumia
wananchi.”
Waziri Mkuu amesema kwa msingi huo,
Serikali itaendelea kuunga mkono juhudi za CCT na madhehebu mengine ya
dini katika kuwahudumia Watanzania kupitia sekta za elimu, maji, afya na
shughuli za ujasiriamali.
Amesema suala la kujitegemea ndiyo msingi
wa uongozi wa Rais Dkt. Magufuli wa kujenga uchumi wa kati unaoongozwa
na viwanda ifikapo mwaka 2025 na katika kufanikisha hilo, Serikali
imeendelea kupunguza kiwango cha utegemezi.
Amesema kiwango cha utegemezi kutoka kwa
Washirika wa Maendeleo katika bajeti kimepungua kutoka asilimia 12.5
mwaka 2017/2018 hadi asilimia nane 2019/2020. “Kuimarika huko kwa bajeti
yetu kunakwenda sambamba na kuimarika kwa huduma za kijamii kama vile
elimu, maji na kupungua kwa umaskini wa mahitaji muhimu.”
Kwa upande wake, Katibu
Mkuu wa CCT, Mchungaji Canon Moses Matonya, amesema jumuiya hiyo
imeanzisha mkakati wa kuwa na vitegauchumu vyake kwa lengo kuondokana na
utegemezi wa fedha za ufadhili ambazo zimekuwa zikipungua mwaka hadi
mwaka.
0 comments:
Post a Comment