****************
Na: Frank Shija – MAELEZO, Dodoma.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amempongeza Rais Uhuru Kenyatta kwa
kuwa Rais wa kwanza wa nje kutembelea Wilaya ya Chato.
Amesema kuwa ukiachilia mbali
ujirani uliopo baina ya Tanzania na Kenya, pia kuna undugu kwa kuwa
tunazungumza lugha moja, tunamuingiliano wa kijamii ikiwemo kuoana na
kuwa na utamaduni unaofanana.
“Kufika kwako umeudhihirishia umma
wa dunia kuwa sisi ni majirani, na marafiki wa kweli siku zote
tutatembea pamoja kamwe tusikubali kulaghaiwa na watu,” amesema Rais
Magufuli.
Rais Magufuli amesema kuwa
kutokana na ushirikiano huo wafanyabiasha wa Kenya na Tanzania wamekuwa
wakishirikiana katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo na kijamii
ikiwemo kuwekeza katika nchi zetu.
Kwa ujibu wa takwimu za Kituo cha
Uwekezaji Tanzania (TIC), Kenya imewekeza miradi 504 yenye thamani ya
dola 1.7 biloni ikiwa na idadi ya watu 50,956 huku wawekezaji wa
Tanzania nchini Kenya wakiwa wakekezaji 24.
Aidha katika Sekta ya Utalii,
Tanzania ni nchi ya pili kwa watu wake kutembela nchini Kenya
ikitanguliwa na nchi ya Marekani ambapo kwa mujibu ya takwimu za Bodi ya
utalii ya Kenya ya Mwaka 2018 Watanzania 222,216 walitembelea Kenya
ambayo ni zaidi ya 10% ya watu wote waliotembelea Kenya.
Katika hatua nyingine Rais
Magufuli ameitaja miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwa kwa ushirikiano
wan chi hizi mbili ikiwemo barabara ya Holili- Arusha hadi Namanga
pamoja na maandalizi ya ujenzi wa Barabara kutoka Mombasa hadi Bagamoyo.
Rais Magufuli amesema kuwa
Tanzania ipo katika hatua mbalimbali za kujenga meli tano ambapo
itaanzisha safari za kutoka Bukoba – Mwanza – Kisumu na Jinja.
Vile vile Rais Dkt. Magufuli
ametoa wito kwa wawekezaji kutoka Kenya kuja kuwekeza nchini hapa kwa
kuwa milango ipo wazi kwa mwekezaji yeyote na Watanzania waendelee
kuwekeza Kenya ili kuendeleza ushirikiano uliopo kwa mustakabari wa
maendeleo ya nchi zote mbili.
Kwa upande wake Rais wa Jamhuri ya Kenya, Uhuru Kenyata amesema anayofuraha kuwa Rais wa kwanza wa nje kukanyaga ardhi ya Chato.
Ameongeza kwamba uwepo wake Chato
Mkoani Geita ni udhibitisho kuwa nchi hizi ni ndugu na wapo kwa ajili ya
kuendelea kuimarisha ushirikiano uliopo baina ya Tanzania na Kenya.
“Hakuna mtu anayeweza
kututenganisha kamwe, sisi kama watu wa Afrika Mashariki yatupasa
kuhakikisha tunaondoa vikwazo vyote vitakavyozuia kutembeleana,
kufanyabiashara pamoja na pengine hata kuoana.” Alisema Kenyatta.
Apongeza Ujenzi Uwanja wa Ndege Chato
Rais Kenyatta ameipongeza Serikali
kwa kujenga uwanja wa ndege wa Chato kwa kuwa ni utaimarisha na kukuza
ukuaji wa biashara na shughuli nyingine za kimaendelea katika ukanda huo
jambo ambalo halipaswi kubezwa.
Amesema anashangazwa na baadhi ya
wanasiasa ambao wamekuwa wakipuuza jitihada hizo za kujenga uwanja huo
kwani ni muhimu na yeye kama Rais wa Kenya angependa kuona Afrika ya
Mashariki inakuwa kitu kimoja.
Amechukizwa na kauli za baadhi ya
wanasiasa na kusema haiwezekani kumzuia Mtanzania kufanya biashara au
kuoa nchini Kenya vivyo hivyo kwa Wakenya nchini Tanzania.
Rais Kenyatta yupo hapa nchini
ikiwa ni ziara yake binafsi kwa siku mbili kuanzia leo tarehe 05 Julai
hadi siku ya kesho Jumamosi ya tarehe 06 Julai 2019.
0 comments:
Post a Comment