*Asifu amani iliyopo nchini, upendo wa Watanzania
*Asema mahujaji wa Tanzania hawana rekodi za uovu
WAZIRI wa Mambo ya Dini wa Saudi Arabia, Dk. Saleh Ali Sheikh amesema Tanzania ni mfano wa kuigwa na nchi nyingine kutokana na amani iliyopo.
Ametoa kauli hiyo jana usiku (Jumapili, Mei 27, 2018) wakati akitoa nasaha kwa wageni walioshiriki futari iliyoandaliwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwenye makazi yake jijini Dar es Salaam.
“Ninaomba nipelekewe shukrani zangu kwa umma wa Watanzania kutokana na upendo walionao. Ukiwaona ni watu wa amani, furaha na upendo na hili linathibitishwa na amani iliyopo nchini mwenu,” alisema.
Alisema uwepo wa amani na upendo miongoni mwa wananchi ni kielelezo tosha cha kazi kubwa inayofanywa na viongozi wa dini ambao ndiyo wanawalea Watanzania. “Kilichofanyika leo ni daraja kati ya Tanzania na Saudi Arabia, ni asubuhi njema ambayo pia ni dalili kwamba kuna mchana mwema unakuja,” alisema.
Alimshukuru Waziri Mkuu kwa ukaribisho aliopewa kushiriki futari nyumbani kwake na kuongeza kuwa hicho ni kitendo cha udugu na utu na kitazidi kujenga mahusiano baina ya nchi hizo mbili.
Alisema tabia hizo njema ni urithi kutoka kwa maulamaa waliotumwa na Mungu ambao kazi yao kubwa ilikuwa ni kuwatengeneza watu wawe na tabia njema na siyo kuwafundisha junsi ya kurusha ndege.
“Matendo haya yanaonekana wazi kwa Watanzania kwani hata wakati wa hijja kuna nchi nyingi zinakuja kule kwetu, lakini haijawahi kuripotiwa kuwa hujaji wa Tanzania ameingia katika utovu wa adabu,” alisema.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alimshukuru Waziri huyo na ujumbe wake kwa kuitembelea Tanzania na kushiriki kwenye mashindano ya 19 ya kuhifadhi Quran Afrika.
Waziri Mkuu alisema amefarijika na uamuzi wa Waziri huto wa Saudi Arabia na ujumbe wake wa watu 16 kuamua kuongeza siku zaidi za ziara yao hapa nchini hadi Jumatano (Mei 30, 2018) badala ya kuondoka Jumatatu (Mei 28, 2018) ili waweze kutembelea vituo vya watoto yatima na kuona maeneo mengine jijini Dar es Salaam.
“Tumefarijika na ahadi uliyoitoa pale uwanjani kwamba mwaka kesho utahakikisha kwamba Sheikh Mkuu wa Msikiti wa Makkah, Sheikh Abdul Rahman Abd al Aziz al Sudais anakuja nchini kuhudhuria mashindano ya 20 ya kuhifadhi Quran tukufu,” alisema.
Viongozi wengine waliohudhuria futani hiyo ni Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir bin Ally na Rais wa taasisi ya Al-Hikma, Sheikh Sharif Abdilkadir Al-Ahdal, na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana. Wengine ni Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mstahiki Meya wa Kinondoni wa Meya wa Temeke.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATATU, MEI 28, 2018.
0 comments:
Post a Comment