Na Munir Shemweta, Tabora
Kamishna
Msaidizi wa Ardhi Kanda ya Magharibi Idrisa Keyera amesema manispaa ya Tabora
pekee inadai zaidi ya shilingi bilioni sita kwa wamiliki wa ardhi na mashamba
mkoani humo kama kodi ya ardhi.
Kayera
alisema hayo jana wakati akizungumza na watendaji kata wa Manispaa ya Tabora
alipokutana na watendaji hao kuhamasisha ulipaji wa kodi ya ardhi na mashamba
katika mkoa huo, mkutano uliofanyika ukumbi wa VETA Tabora.
Alisema,
mpaka kufikia sasa katika manispaa ya Tabora zimekusanywa jumla ya shilingi
bilioni 3.2 ikiwa ni pungufu ya malengo waliyojiwekea ya kukusanya shilingi
bilioni nne katika mwaka huu wa fedha unaoishia juni mwaka 2018.
Alisema,
kanda yake inayohusisha mikoa ya Tabora, Shinyanga, Kigoma na Katavi imeanza
kuchukua hatua kwa wadaiwa sugu wa kodi za ardhi kwa kuwapatia hati za madai
ambapo wahusika watatakiwa kulipa madeni yao ndani ya wiki mbili na wasipofanya
hivyo wanapelekwa mahakamani na huko vifaa vyao au nyumba zitauzwa kufidia deni
huku umiliki nyumba ama shamba ukifutwa.
‘’Unapopelekwa
mahakamani uwezekano wa kushinda haupo na pia itakulazimu kulipa gharama za
madadlali kwa kushindwa kulipa’’ alisema Kamishana Msaidizi Kayera.
Kwa
mujibu wa Kayera, kikao chake na watendaji wa kata za manispaa ya Tabora ni moja
ya harakati za ofisi yake ya Kanda ya magharibi kuhakikisha kodi ya serikali
inapatikana sambamba na kuwashirikisha watendaji kuwatambua na kuwapelekea hati
za madai wadaiwa sugu wa kodi ya ardhi katika mitaa yao ili kuwabana waweze
kulipa madeni yao.
Aidha,
Kamishna Msaidizi wa ardhi Kanda ya Magharibi alisema, utaratibu wa kulipa kodi
ya ardhi kwa sasa ni rahisi kwani unaweza kulipia kwa njia ya simu na malipo hayo
yanafanywa na wananchi waliopimiwa maeneo yao ingawa serikali iko katika hatua
za kuhakikisha maeneo yote ya mijini hata yale yasiyopimwa wamiliki wake
wanalipa kodi ya ardhi.
Kwa
upande wao watendaji wa kata za manispaa ya Tabora pamoja na kuunga mkono
jitihada za uhamasishaji wa ulipaji kodi ya ardhi wametaka kupatiwa taarifa
pamoja na ramani za maeneo yao kwa lengo la kutambua maeneo hasa pale
yanapotokea mabadiliko ya matumizi ya ardhi katika maeneo husika jambo
linalowapa wakati mgumu wakati wa kutekeleza majukumu.
Hata
hivyo, wametaka halmashauri ya Manispaa ya Tabora na ofisi ya Kamishna wa Ardhi
Kanda ya Magaharibi kuwawezesha wakati wa kufanya kazi ya kuwapelekea wadaiwa
wa kodi ya ardhi ikiwemo kuwapa motisha hasa wale watendaji wanaoishi maeneo ya
pembezoni ambapo watendaji wake wamekuwa na wakati mgumu kuwafikia wananchi
kutokana na kukosa nauli na gharama nyingine.
Wizara
ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kupitia ofisi zake za Kanda imekuwa na
kampeni kamambe ya kuhamasisha wananchi kulipa kodi ya ardhi na mashamba kabla
ya Juni 30 mwaka huu wa 2018, huku wale wadaiwa sugu wakipatiwa hati za madai
ili waweze kulipa madeni yao kabla ya hatua za kisheria hazijachukuliwa dhidi
yao.
-----------------------------------------MWISHO---------------------------------------------------------------
0 comments:
Post a Comment