METDO Tanzania

METDO Tanzania

Saturday, April 15, 2017

RAIS MAGUFULI AZINDUA MABWENI YA CHUO KIKUU CHA DAR ES SALAAM

Na Mathias Canal, Dar ea salaam

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli Leo April 15, 2017 amezindua Mabweni yatakayotumiwa na wanafunzi wa chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM) kwa gharama nafuu ya shilingi 500 kwa siku ambapo kwa Muhula mmoja (Semista) watalipia kiasi cha shilingi elfu sitini pekee.

Akizungumza katika uzinduzi huo huku akiwa ameambatana na mkewe Mama Janeth Magufuli, Rais Magufuli amewapongeza Wakala wa majengo Tanzania (TBA) na wadau wote walioshiriki katika ujenzi huo zikiwemo wizara za Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Rais Magufuli amesema kuwa kwa muda mrefu wanafunzi wa chuo Kikuu cha Dar es salaam wamekuwa na matatizo ya makazi kwani wanaishi kwa kupanga katika maeneo ya mchanganyiko maeneo ambayo sio rafiki na ustawi wa Elimu yao huku wakitumia gharama kubwa hivyo aliamua kuanzisha ujenzi huo ili kuwanusuru na adha waliyokuwa wanakumbana nayo.

"Nafahamu Mabweni ya Mabibo yalijengwa miaka ya 2000 kwa gharama ya shilingi Bil 27 ambayo yanabeba wanafunzi 4000, lakini Mabweni haya yamejengwa miaka hii ya 2016/2017 na yamejengwa kwa gharama ya shilingi Bilioni 10 na yatabeba wanafunzi 3840 hii ndio raha ya hesabu naamini mmenielewa" Alisema Dkt Magufuli

Amesema kuwa jambo hilo linapaswa kuwa fundisho kwa viongozi wote wa serikali waliozoea kuchukua asilimia 10 ya malipo kwa majengo ya gharama kubwa wakati wangeweza kutumia gharama nafuu.

Rais Magufuli ameagiza wanafunzi wote watakaokuwa wanaishi katika Mabweni hayo kutozwa gharama ya Shilingi 500 ambayo kwa muhula mmoja itakuwa shilingi 60,000 badala ya shilingi 800 kwa Siku iliyokuwa imepangwa.

Katika Hatua nyingine Rais Magufuli ameiagiza Bodi ya Elimu ya Juu (TCU) kutowapangia wanafunzi vyuo vya kusoma badala yake kuwaacha wachague wenyewe kwani kufanya hivyo ni kuwanyima haki ya kuchagua vyuo walivyokusudia kusoma kulingana na ufaulu wao.

"TCU isiwapangie wanafunzi vyuo Bali wachague wenyewe na kama kuna vyuo havitachaguliwa mviache vife maana havikidhi vigezo vyao walivyovitaka ikiwemo sehemu nzuri za kulala kama hizi ninazozindua Leo" Alisema Rais Magufuli

Mabweni hayo 20 yenye ghorofa NNE kwa kila moja yamejengwa na Wizara ya Uchukuzi kupitia Wakala wa Majengo (TBA) yatawaidia wanafunzi takribani wanafunzi 3840 waliokuwa wanateseka kwa kuishi mitaani kwa kupata adha kubwa ya malazi katika mazingira magumu yasiyoweza kuwapa fursa ya kusoma na kufaulu vizuri.

Octoba 21, 2016 Rais Magufuli Aliweka jiwe la Msingi katika mradi wa ujenzi wa Mabweni 20 ya wanafunzi 3840 ikiwa ni utekelezaji wa ahadi aliyoitoa mwezi June 2016 wakati wa uzinduzi wa maktaba ya kisasa ya chuo hicho.

Hafla ya Uzinduzi wa Mabweni ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM) Imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Profesa Joyce Ndalichako (MB) Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt Hussein Mwinyi (MB) Waziri wa Ulinzi na Jeshi La Kujenga Taifa, Profesa Makame Mbarawa (MB) Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Makatibu Wakuu wa Wizara mbalimbali, Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi Ndg Humphrey Polepole, Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe Paul C. Makonda.

Pia Rais Magufuli ameweka jiwe La msingi kwenye ujenzi wa nyumba za wananchi alizowaahidi wananchi waliokuwa wamepoteza matumaini Katika eneo la Magomeni Kota.

Mwisho

Rais Dkt John Pombe Magufuli
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com