Na Mathias Canal, Dar es salaam
Imebainika kuwa zipo Kanda za Video (CD) zinauzwa Mitaani kwa bei ya chini jambo ambalo linaua soko la Kazi za Wasanii nchini na kuwafanya wasanii hao kuwa na kipato kidogo kwa kazi kubwa wanayoifanya huku wakibakia katika Lindi la Umasikini.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe Paul C. Makonda wakati akitoa salamu za Mkoa wa Dar es salaam mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe Magufuli wakati wa halfa ya uzinduzi wa Mabweni 20 yenye ghorofa nne kila moja yaliyojengwa na Wakala wa Majengo nchini (TBA) katika Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM) Kwa gharama ya Shilingi Bil 10.
Rc Makonda Alisema kuwa Mtaa wa Kariakoo Jijini Dar es salaam uliwahi kuwa na maduka takribani 300 ya kuuza bidhaa za wazawa lakini yamesalia maduka mawili pekee huku maduka mengine yakiwa ni Yale yanayopakuwa Filamu kutoka kwenye mitandao na kuzisambaza Mtaani kwa bei ya chini ilihali nchi kama Nigeria na Ghana wananchi wake hawaruhusiwi kuuza filamu za nje ya nchi.
Alisema kuwa wasanii wa Bongo Movie nchini Tanzania wanalipia shilingi 500,000 Baraza la filamu, 300,000 kwa ajili ya kupewa kibali, Wanalipia shilingi 1000 kwa kila dakika moja wanapokwenda kukaguliwa kazi zao ili iweze kupitishwa na kuonekana imefaa kwa maudhui ya watanzania.
"Mhe Rais sisi wasaidizi wako tumeamua kuitafsiri kwa vitendo ndoto ya kuwapigania na kuwatetea watanzania wanyonge wanaonyonywa Mali zao na watu wachache wasiolitakia mema Taifa letu" Alisema Mhe Makonda
Alisema kuwa wasanii wanalazimika kuingia mkataba na Steps Entertainment ili awasaidie kusambaza kazi zao kwa makubaliano ya kuilipa kampuni hiyo kwa ujira wa usambazaji.
Rc Makonda alisema kuwa wasanii hao wanalipia kodi ya 30% ya mapato yao lakini wabadhilifu wanaoingiza filamu kutoka nje hawalipi kodi mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Hawalipii Baraza la filamu Tanzania wala sehemu yoyote, hivyo wanafanya kazi za wizi zinazokandamiza na kuua soko la kazi za wasanii wa Tanzania.
"Mhe Rais Katika Mtaa wa Kariakoo kuna duka moja lenye mzigo wa takribani Bilioni 4 za kitanzania lakini mzigo wote huo haulipiwi kodi kwahiyo Mhe Rais ukisikia kuna kelele huko wanaolia ni wengi wacha tuendelee kuwaliza ili wanyonge na masikini wapate haki yao" Alisema Rc Makonda
Hata hivyo Rc Makonda ametangaza kuanza Operesheni ya kuwabaini wezi wa kazi za wasanii katika Mkoa wa Dar es salaam huku akimpongeza Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Dkt Harrison Mwakyembe kwa dhamira yake njema na ushirikiano mkubwa katika kuwatetea wasanii nchini.
Baada ya uzinduzi wa Mabweni katika chuo Kikuu cha Dar es salaam Mhe Rais Magufuli pia ameweka jiwe la msingi ujenzi wa Nyumba za serikali katika Mtaa wa Magomeni Kota kwa ajili ya wananchi waliopoteza matumaini kutokana na umasikini unaowakabili.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment