Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi,Vijana na Ajira Mh Anthony Mavunde amewataka Vijana mkoani Iringa kuchangamkia fursa mbalimbali za mafunzo ya Ujasiriamali yenye lengo la kukuza Ujuzi wa Vijana ili waweze kujiajiri na kuajiri Vijana wengine.
Mavunde ameyasema hayo leo mjini Iringa wakati akifunga mafunzo ya siku tatu ya Ujasiriamali yaliyoandaliwa na Umoja wa Vijana wa CCM Mkoa wa Iringa.Mavunde ameupongeza uongozi wa UVCCM mkoa wa Iringa chini ya Mwenyekiti Kenan Kihongosi kwa kuratibu na kuandaa mafunzo hayo ambayo yamejumuisha zaidi ya Vijana 600 bila kubagua Itikadi za kisiasa.
Aidha Mavunde alichukua nafasi hiyo kuitaka Manispaa ya Iringa kutenga maeneo maalum kwa ajili shughuli
Za uzalishaji mali za Vijana na kusisitiza pia juu ya utoaji wa fedha za mikopo kwa Vikundi vya Vijana ambayo ni asilimia 5 za mapato ya ndani ya Manispaa.
Akimkaribisha Mgeni Rasmi,Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mh Richard Kasesela ameiagiza Manispaa ya Iringa kuvilea vikundi vya Vijana na kuvikopesha fedha kwa mujibu wa taratibu na pia kuhakikisha wanawapa zabuni Vijana kutengeneza sare za Mwenge wa Uhuru 2018 ukiwa unakimbizwa Manispaa ya Iringa.
Naye Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Iringa Cde Kenan Kihongosi ameahidi kusimamia utoaji wa mafunzo kwa vikundi vya Vijana Mkoa wa Iringa na kubuni miradi itakayosaidia kuimarisha kiuchumi jumuiya ya Vijana Iringa.
0 comments:
Post a Comment