METDO Tanzania

METDO Tanzania

Saturday, July 11, 2020

MABULA, AMEWATAKA WANANCHI WALIOPIMIWA VIWANJA KUTUMIA FURSA YA SIKU 90 KUOMBA HATI


Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Angeline Mabula akisaini kitabu cha wageni alipowasili kuembelea Maonesho ya 44 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (SABASABA) yanayofanyika katika Viwanja vya Mwl. Julius Nyerere barabara ya Kilwa Jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Angeline Mabula (Kulia), akizungumza na Mkazi wa Dar es Salaam, Dkt. Paulina Chiwanga kabla ya Kumkabidhi hati miliki alipotembelea banda la wizara hiyo katika Maonesho ya 44 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (SABASABA) yanayofanyika katika Viwanja vya Mwl. Julius Nyerere barabara ya Kilwa Jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Angeline Mabula(kulia), akimkabidhi hati miliki  Mkazi wa Dar es Salaam, Dkt. Paulina Chiwanga katika Banda la Wizara hiyo alipotembelea Maonesho ya 44 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (SABASABA) yanayofanyika katika Viwanja vya Mwl. Julius Nyerere barabara ya Kilwa Jijini Dar es Salaam.

Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeendelea kuimarisha huduma zake kwa wananchi wanaopata fursa ya kutembelea banda la Wizara hiyo katika Maonesho ya 44 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (SABASABA) kwani imeongoza idara mbalimbali ambazo zinatoa huduma muhimu kwa wananchi.

Akizungumza wakati wa Kutembelea Maonesho ya SABASABA, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Angeline Mabula ameipongeza Wizara hiyo kwa ubunifu wa kuja na Idara ambazo ni muhimu kwa wananchi kama vile, Utoaji wa Hati, Bodi ya Mipango Miji na Idara ya Upimaji na Ramani.

“Kwa Maonesho ya SABASABA mwaka huu kwa upande wa Wizara ya Ardhi imekuwa ni fursa kubwa kwa wananchi kuja kupata huduma katika idara za Wizara hii, huduma nyingi zinatolewa kwenye maonesho hayo ikiwemo utoaji wa hati, kwani hati zaidi ya 10 zimetolewa, huduma za mabarza ya ardhi na elimu kuhusu upimaji ardhi kwa wananchi”, Dkt.Angeline Mabula.

Aidha Mabula alisema kuwa katika Maonesho hayo Makampuni ya Upimaji yamepata fursa ya kuja kujitangaza kwa wananchi kuhusu huduma zinazotolewa na makampuni hayo, pia makampuni  ya kuuza vifaa ambavyo vinatumika katika kutatua kero za wananchi kwenye sekta ya upimaji na kuepusha migogoro ya Ardhi Nchini.

Dkt. Mabula pia alitoa maagizo kwa Bodi ya Usajili wa Makampuni ya urasimishaji kusimamia vyema idara hiyo ili wananchi waweze kupata huduma iliyobora, mpaka sasa makampuni zaidi ya sita yemefungiwa kufanya kazi hiyo kwani yalikuwa yakifanya kazi chini ya kiwango na ameielekeza bodi hiyo kuyapitia makampuni yote.

Kupitia Maonesho hayo Dkt.Mabula aliwataka wananchi waliopimiwa viwanja na bado hawajaomba hati miliki ya viwanja hivyo wafanye hivyo ndani ya siku 90 zilizotolewa na bunge za kuomba hati na kupatiwa ndani ya siku hizo.

“Wananchi ambao wamekamilisha zoezi la upimaji na hawajapata hati nawashauri tu wakaombe na kuchukua hati hizo ili waweze kuwa na miliki ya viwanja vyao ndani ya siku 90, tuna viwanja 900 nchi nzima ambavyo vimepimwa lakini wamiliki hawajapata hati miliki, nawaomba wananchi kutumia fursa hii ya siku 90 tofauti na hapo wataanza kutoshwa pango la ardhi tokea siku waliyopimiwa hata kama ni mwaka 1,999 watatakiwa kulipa kodi yote kwa hiyo ni fursa nzuri kwa wananchi”, Alisisitiza Dkt.Mabula.

Aidha, Dkt.Mabula alitoa ushauri kwa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), kuwa vijana wanaoenda kupata mafunzo ya Jeshi hilo kwa  kujitolea kuwekwa katika vikundi  Kimkoa au  Kiwilaya ilikupata mkopo kutoka Halmashauri zao na  kufanya ujasiriamali kutokana na ujuzi wanaofundishwa wakiwa katika mafunzo hayo ili waweze kujitekemea wakiwa wanasubiri ajira

Kwa upande mwingine, Dkt.Mabula alifurahishwa na huduma ya kufanya matibabu kwa wagonjwa wenye mawe kwenye figo  kwani Hospitali ya Taifa Muhimbili imekuja na teknolojia mpya ya matibabu kwa kutumia mtetemo na kuvunja mawe ambapo wagonjwa wanapata huduma hiyo bila upasuaji.

Katika suala la Nchi kuingia katika uchumi wa kati, Dkt.Mabula alisema kuwa Wizara ya Ardhi ni wezeshi katika suala hilo kwani imekuwa ikiwawezesha wawekezaji kuwekeza kwa kuwawapa ardhi iliyopimwa kwa ajili ya viwanda na maeneo mengine ya uwekezaji.

“Wizara ya Ardhi ni Wizara wezeshi katika sekta ya viwanda na ndiyo maana katika suala zima la upimaji na  mipango miji, lazima kuwe na maeneo ya viwanda ili tukipata wawekezaji walahi wasipate tena shida ya kupata ardhi kwa hiyo sekta hii imewezesha Tanzania kufikia uchumi wa kati”, alisema Dkt.Mabula.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com