Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imewasilisha taarifa ya utekelezaji maagizo ya kutoondolewa vijiji 920 kati ya 975 vilivyokuwa katika migogoro maeneo ya hifadhi nchini kwa Wakuu wa mikoa wa Tanzania Bara.
Uwasilishaji taarifa hiyo umefanywa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mary Makondo jijini Dodoma mwishoni mwa wiki na kuhudhuriwa na Mawaziri, Manaibu Mawaziri, Makatibu Wakuu na Wataalamu kutoka wizara za Ardhi, Ofisi ya Raisi TAMISEMI, Kilimo, Mifugo, Maliasili na Utalii, Maji na Makamu wa Raisi ambazo Mawaziri wake walitembelea maeneo yenye mgogoro na kuja na mapendekezo yaliyosababisha Rais kuchukua uamuzi huo.
Awali wananchi waliokuwa wakiishi kwenye vijiji vya hifadhi walionekana wavamizi wakati serikali ilitoa hati za usajili kwa vijiji na wananchi wake kushiriki shughuli mbalimbali zikiwemo za uchaguzi jambo lililomfanya Rais John Pombe Magufuli kuchukua uamuzi wa kuvibakisha vijiji 920 baada ya kupata ushauri wa mawaziri wa sekta husika.
Akizungumza wakati wa kuwasilisha taarifa hiyo kwa Wakuu wa Mikoa ya Tanzania Bara Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mary Makondo alisema, utekelezaji maamuzi ya kutoondolewa vijiji 920 ni wa awali huku kazi kwa vijiji 55 vilivyosalia ikiendelea ambapo alisema itahusisha Wakuu wa mikoa, wilaya na wataalamu wengine.
Kwa upande wake Waziri wa Ardhi William Lukuvi aliwaambia wakuu hao wa mikoa kuwa, uwasilishaji taarifa ya utekelezaji maagizo yaliyofikiwa kuhusiana na vijiji 920 unafanyika kwa kwa lengo la kuwafahamisha ni vijiji gani vimefutwa na ipi ya kupunguzwa katika maeneo yao.
‘’kazi ya kubakisha vijiji kwenye maeneo ya mgogoro katika hifadhi imeanza na lengo hapa ni wananchi wasiishi kwa hofu na ninyi kama Wakuu wa mikoa lazima mfahamishwe ili kujua ni misitu gani imefutwa na ipi imepunguzwa’’ alisema Lukuvi
Kwa mujibu wa Lukuvi, wizara yake imeona ni wakati muafaka kuiwasilisha taarifa ya utekelezaji maagizo hayo kwa wakuu wa mikoa kutokana na wao kuwa na mamlaka katika maeneo yao na kuongeza kuwa pamoja na Wizara hiyo kushughulika na migogoro kwenye maeneo ya hifadhi lakini itaendelea kushughulikia migogoro mingine kwa utaratibu wa serikali.
Hivi karibuni Waziri Lukuvi alisisitiza kufanyika uchambuzi wa kina wakati wa utekelezaji maagizo hayo ili kuja majibu yatakayokidhi malengo ya uamuzi uliofanyika ambapo alisema wakati kazi ya uchambuzi ikiendelea wasimamizi wa sheria wanapaswa kuendelea kusimamia sheria na kuwatahadharisha kuwa makini wakati wa utekelezaji majukumu yao ili kuepuka uvunjifu wa amani.
Kwa muda mrefu wananchi wa Vijiji 975 vilivyo katika hifadhi wamekuwa katika mgogoro kwa kudaiwa kuwa wavamizi na kusababisha nyumba zao kuchomwa moto huku baadhi yao wakiwa wameishi maeneo hayo kwa zaidi ya miaka ishirini.
Mgogoro huo ulisababisha Rais John Pombe Magufuli kuingilia kati na kuridhia vijiji 920 kubaki maeneo ya hifadhi sambamba na kufutwa misitu ya hifadhi saba yenye ukubwa wa ekari 46,715 ili ipangwe upya. Pia Rais Magufuli alifuta mapori tengefu 12 yenye ukubwa wa ekari 707,659.94 na ardhi hiyo kugawiwa kwa wananchi kwa ajili ya makazi, kilimo na shughuli za ufugaji.
0 comments:
Post a Comment