Mbunge wa jimbo la Ilemela mheshimiwa Daktari Angeline Mabula leo amefanya uzinduzi wa mradi wa ujenzi wa barabara ya kutoka Kitangiri mzunguko kupitia mwinuko inayoishia Kabuhoro itakayoanza kujengwa rasmi April 10, mwaka huu na kutegemewa kukamilika Novemba 11, 2018 ukigharimu jumla ya shilingi 785,011,735 ikijumuisha ujenzi wa mitaro, tabaka la barabara na alama za barabarani
Akizungumza katika uzinduzi huo mbunge huyo mbali na kuelezea juu ya miradi mikubwa ya ujenzi wa barabara inayoendelea ndani ya jimbo lake ikiwemo ule wa uboreshaji miundombinu ya miji ya kimkakati TSCP unaojumuisha ujenzi wa barabara ya kilomita 8 ya kutoka Sabasaba kupitia Kiseke na kuishia Buswelu amemuasa mkandarasi wa ujenzi wa barabara hiyo Jemen Contractors kuhakikisha anakamilisha mradi huo kwa wakati na kuzingatia ubora unaotakiwa sambamaba na kuwaasa vijana watakaotumika kama vibarua katika mradi huo kuwa waaminifu kwa kutojihusisha na vitendo vya ubadhirifu
‘… Tunatambua kuwa kuna taratibu za kizabuni katika kutekeleza miradi ya namna hii, Lakini nikuhakikishie tu kama utakamilisha mradi huu kwa wakati na kwa kuzingatia ubora unaotakiwa tutaendelea kufanya kazi na wewe …’ Alisema
Aidha mheshimiwa Daktari Angeline Mabula amewaasa wananchi watakaopitiwa na mradi huo kutoa ushirikiano kwa kuruhusu maeneo yao yawe wazi ili mradi uweze kukamilika na wale watakaostahili kulipwa fidia kisheria Serikali itafanya hivyo
Kwa upande wake mkurugenzi wa manispaa ya Ilemela John Wanga amewataka wananchi watakaonufaika na mradi huo kuitumia fursa ya hiyo kwa kuanzisha biashara na miradi mingineyo ya kiuchumi ili kujikwamua na umasikini kwani mradi huo utasaidia upatikanaji wa wateja kiurahisi baada ya kukamilika kwa njia za usafirishaji watu na bidhaa
Nae meneja wa wakala wa barabara za mijini na vijijini kwa mkoa wa Mwanza mhandisi Fuko amemshukuru mheshimiwa Rais kwa kuanzisha taasisi hiyo ya wakala wa barabara za mji na vijiji TARURA huku akiwaomba wananchi na viongozi ushirikiano ili kukamilisha mradi huo kwa wakati
Akihitimisha mwenyekiti wa umoja wa vijana wa chama cha mapinduzi taifa Kheri James mbali na kushukuru kwa kupata fursa ya kushuhudia uzinduzi wa mradi huo, amempongeza mbunge wa jimbo hilo kwa kufanikisha ndoto ya muda mrefu kwa wananchi wa Kirumba na Kitangiri ya kuwa na miundombinu ya uhakika inayopitika muda wote huku akiwaasa viongozi kuendelea kushirikiana katika kuwaletea wananchi wao maendeleo pamoja na kumuomba mkandarasi wa mradi huo kuwatumia vijana wa maeneo utakapopita mradi huo kama vibarua katika kutekeleza shughuli za kila za ujenzi wa mradi huo
' Ilemela ni yetu, tushirikiane kuijenga'
Imetolewa na
Ofisi ya mbunge
Jimbo la Ilemela
07.04.2018
0 comments:
Post a Comment