Mkurugenzi wa shirika la AGAPE,John Myola akizungumza katika warsha kwa warsha kwa wawakilishi wa vikundi vya vijana na watu wazima wanaoshiriki katika mapambano dhidi ya mila na desturi kandamizi wilayani Kishapu
*****
Shirika la AGAPE Aids Control Programme limeendesha warsha kwa wawakilishi wa vikundi vya vijana na watu wazima watakaokutana na waidhinisha ndoa wilayani Kishapu mkoani Shinyanga ili kukabiliana na mila na desturi kandamizi zinazochangia ndoa na mimba za utotoni.
Warsha hiyo ya siku moja imefanyika leo Ijumaa Aprili 6,2018 katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya ya Kishapu.
Miongoni mwa wadau walioshiriki katika warsha hiyo ni vijana,wazee maarufu,viongozi wa kimila,viongozi wa dini,wanasheria,viongozi wa dini ,idara ya afya na maafisa kutoka Shirika la AGAPE.
Akizungumza wakati wa warsha hiyo,Meneja Mradi wa kutokomeza mila na desturi kandamizi Peter Amani alisema warsha hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi huo unaotekelezwa na shirika la AGAPE kwa kushirikiana na shirika la Save The Children kwa ufadhili wa Umoja wa Ulaya.
“Lengo la warsha hii ni kuwajengea uwezo wawakilishi wa vijana na watu wazima kuhusu madhara ya mila na desturi kandamizi zinazochangia kuwepo kwa mimba na ndoa za utotoni ambapo wawakilishi hawa watakwenda kutoa elimu hii kwa wathibitisha ndoa katika jamii”,alisema Amani.
Alisema shirika hilo linatekeleza mradi huo katika kata 12 za halmashauri ya wilaya ya Kishapu na katika warsha hiyo,washiriki wametoka katika kata sita ambazo ni Lagana,Mwamashele,Itilima,Mwakipoya,Masanga na Mwamalasa.
Kwa upande wake,Mkurugenzi wa shirika la AGAPE,John Myola alisema watoto wameendelea kukosa haki zao kutokana na baadhi ya watumishi katika vyombo vya dola ikiwemo mahakama kuendekeza rushwa na kukwepesha sheria kulinda wahalifu hasa wale wanaowapa mimba na kuozesha watoto.
Nao viongozi wa dini Sheikh Adam Njiku na Mchungaji Lucas Mwigulu waliiasa jamii kupeleka shule watoto na kutowabagua watoto wa kike.
Aidha waliomba sheria za nchi ziseme dhahiri kuwa umri halisi wa kuolewa ni kuanzia miaka 18 badala ya kuchanganya sheria ya ndoa ya mwaka 1971 inayoruhusu mtoto kuolewa akiwa na umri kuanzia 14/15 kwa ridhaa ya wazazi.
Naye mzee wa mila, Suzana Mbalu alisema ndoa na mimba za utotoni zinachangiwa na mmomonyoko wa maadili katika jamii hivyo kuwataka wazazi na walezi kuwa karibu na watoto wao ambao wanakumbwa na na utandawazi na kuiga maisha ya mataifa mengine duniani.
ANGALIA PICHA HAPA CHINI
Meneja Mradi wa kutokomeza mila na desturi kandamizi Peter Amani kutoka shirika la AGAPE akielezea malengo ya warsha kwa wawakilishi wa vikundi vya vijana na watu wazima watakaokutana na waidhinisha ndoa wilayani Kishapu mkoani Shinyanga.
Washiriki wa warsha hiyo wakiandika dondoo muhimu…
Meneja Mradi wa kutokomeza mila na desturi kandamizi Peter Amani akielezea kuhusu madhara ya mila na desturi kandamizi kwa watoto.
Mkurugenzi wa shirika la AGAPE,John Myola akiwahamasisha washiriki wa warsha hiyo kutumia elimu waliyopewa kuielimisha jamii kuhusu madhara ya mila na desturi kandamizi na kuhakikisha watoto wanapata elimu itakayowasaidia katika maisha yao.
Sheikh Adam Njiku kutoka Bakwata Kishapu akielezea kuhusu taratibu za uthibitishaji/uidhinishaji wa ndoa katika dini ya Kiislamu. Sheikh Njiku aliiasa jamii kupeleka watoto wa kike shule kwani wanawake ni wasaidizi wakubwa katika familia na jamii kwa ujumla
Mchungaji Lucas kutoka kanisa la KKKT Kishapu akielezea kuhusu taratibu za uthibitishaji/uidhinishaji wa ndoa katika dini ya Kikristo. Aidha aliwataka wazazi kutoozesha watoto kwa kuwalazimisha huku akisisitiza nguzo kuu katika ndoa ni upendo na utii.
Mzee wa mila, Suzana Mbalu akielezea kuhusu taratibu za uthibitishaji/uidhinishaji wa ndoa kimila ambapo alisema hakuna mila inayoruhusu mtoto aolewe chini ya miaka 18 isipokuwa jamii imebadilika kutokana na utandawazi unaosababisha jamii kuiga maisha ya mataifa mengine.
Wakili wa AGAPE, Ellen Lucas akielezea matakwa ya kisheria juu ya ndoa na mimba kwa watoto kwa sheria za Tanzania.
Picha zote na Kadama Malunde- Malunde1 blog
0 comments:
Post a Comment