METDO Tanzania

METDO Tanzania

Thursday, May 29, 2025

Dondoo za Aliyoyasema Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde katika Mkutano na Wahariri wa Vyombo vya Habari, Mei 24, 2025 Jijini Dar es Salaam.

 











Mada: Mafanikio ya Sekta ya Madini katika Kipindi cha Miaka Minne ya Uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan

1. Ongezeko la Bajeti – Bajeti ya Wizara ya Madini imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka. Kutoka shilingi bilioni 89 mwaka wa fedha 2023/2024 hadi shilingi bilioni 231 kwa mwaka 2024/2025. Kwa mwaka ujao wa fedha 2025/2026, tumeidhinishiwa bajeti ya shilingi bilioni 224. Asilimia kubwa ya bajeti hii inaelekezwa kwenye Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) kwa ajili ya kufanya tafiti za kina za jiolojia na ujenzi wa maabara ya kisasa ya uchambuzi wa madini katika eneo la Kizota, Dodoma. Lengo ni kuifanya GST kuwa kitovu cha huduma za maabara ya madini kwa Afrika nzima. Pia, maabara nyingine zinajengwa katika mikoa ya Geita na Chunya (Mbeya) ili kuboresha huduma za uchambuzi wa madini nchini.

2. Ongezeko la GDP – Mchango wa Sekta ya Madini katika pato la taifa (GDP) umeongezeka kwa kiwango kikubwa. Sera ya Madini ya mwaka 2009 pamoja na Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo kwa Miaka Mitano unalenga sekta kuchangia angalau asilimia 10 ya GDP ifikapo mwaka 2025. Hadi kufikia Desemba 2024, mwaka mmoja kabla ya muda uliopangwa, sekta ya madini tayari ilikuwa imefikia mchango wa asilimia 10.1, hatua ambayo ni ya kihistoria na ya kujivunia.

3. Mining Vision 2030: Kauli mbiu ya mpango huu ni “Madini ni Maisha na Utajiri.” Mpango huu unalenga kuongeza kiwango cha tafiti za kina za madini kutoka asilimia 16 ya sasa hadi asilimia 50 ifikapo mwaka 2030. Sekta ya madini pia inatajwa kuwa kichocheo kikuu cha sekta nyingine kama maji, kilimo, afya, viwanda, ujenzi na uchumi kwa ujumla. Kwa sasa sekta imechangia mzunguko wa fedha wa takribani trilioni 1.7 na mauzo yamefikia asilimia 56.2 ya jumla ya mauzo nje ya nchi.

4. Maduhuli – Katika mwaka wa fedha 2015/2016, sekta ya madini ilikusanya maduhuli ya shilingi bilioni 162. Makusanyo haya yameongezeka kwa kasi hadi kufikia bilioni 678 mwaka 2022/2023, na bilioni 753 mwaka 2023/2024. Kwa mwaka huu wa fedha 2024/2025, tumewekewa lengo la kukusanya shilingi trilioni 1. Hadi kufikia tarehe 24 Mei 2025, tayari tumekusanya shilingi bilioni 930, ikiwa ni mafanikio makubwa huku zikiwa zimebaki siku 37 kabla mwaka wa fedha kumalizika.

5. BOT yaanza ununuzi wa Dhahabu – Kufuatia marekebisho ya Sheria ya Madini mwaka 2024, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeanza rasmi kununua dhahabu kutoka kwa wazalishaji wa ndani. Sheria sasa inawataka wamiliki wote wa leseni za uchimbaji wa dhahabu kutenga angalau asilimia 20 ya uzalishaji wao kwa ajili ya kuuza BoT. Kuanzia Oktoba 2024 hadi sasa (miezi 8), BoT imenunua tani 3.7 za dhahabu. Kwa hatua hii, Tanzania inajiweka kwenye nafasi nzuri kuwa miongoni mwa nchi zenye akiba kubwa ya dhahabu barani Afrika – mfano, hivisasa Algeria barani Afrika inaongoza kwa kuwa na akiba ya tani 174, na Msumbiji iko nafasi ya 10 kwa tani 3.6.

6. Uwezeshwaji Wachimbaji Wadogo – Wachimbaji wadogo hivi sasa wanachangia asilimia 40 ya mapato yote yatokanayo na sekta ya madini. Serikali imefuta leseni na maombi 2,648 ili kuwawezesha wachimbaji wadogo kupata maeneo halali ya uchimbaji. Shirika la STAMICO limejipambanua kuwa mlezi wao, ambapo limewanunulia mashine 15 za kuchoronga miamba (drilling rigs). Pia, Serikali imefanya mazungumzo na benki mbalimbali kuwahamasisha kutoa mikopo kwa wachimbaji wadogo, ambapo sasa wanakopesheka. Tumeunda timu ya wataalam sita kutoka sekta binafsi na serikali kwa ajili ya kutoa ushauri wa kitaalamu kuhusu namna bora ya kuwainua wachimbaji wadogo. Kupitia Mfuko wa Dhamana wa Hazina (Credit Guarantee Scheme), wachache wataanza kunufaika na matarajio ni kueneza huduma hiyo kwa wengi zaidi.

7. Viwanda vya kuongeza thamani – Kifungu cha 100 cha Sheria ya Madini kinawataka wawekezaji wanaoomba leseni kuwa na mpango wa kuongeza thamani ya madini. Eneo la Mgodi wa Buzwagi (unaofungwa baada ya kusitisha shughuli za uchimbaji) limegeuzwa kuwa eneo maalum la uwekezaji wa viwanda (Special Economic Zone). Moja ya viwanda vitakavyojengwa ni pamoja na Kiwanda cha Kusafisha Makinikia cha Tembo Nickel Refining Limited, hatua inayolenga kuongeza thamani ya madini ya nickel na ajira nchini.

8. Minada ya Vito – Serikali imerejesha rasmi minada ya ndani ya madini ya vito kwa lengo la kuongeza thamani ya madini haya, hasa Tanzanite ambayo ni adimu duniani. Tumefanya minada Mirerani mwezi Desemba 2024 na Arusha Februari 2025, juhudi hizi pia ni sehemu ya rebranding ya Tanzanite ili kutambulika zaidi kimataifa.

9. Marekebisho ya Sheria – tumefanya marekebisho ya Sheria mwaka 2024, ambapo sasa inabainisha kuwa leseni za uchimbaji mdogo wa madini ni kwa ajili ya Watanzania pekee. Hata hivyo, msaada wa kitaalamu kutoka kwa wageni unaruhusiwa kwa masharti maalum, ikiwemo mkataba rasmi unaopitiwa na Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini ili kuhakikisha Watanzania wananufaika. Pia, Marekebisho haya yamepunguza migogoro mingi kati ya wachimbaji wadogo na wawekezaji.

10. Miradi Mikubwa – Serikali inaendelea kusimamia na kuvutia uwekezaji kwenye migodi mikubwa kama ule wa Nyanzaga uliopo wilayani Sengerema.

11. STAMICO – Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) limepiga hatua kubwa kutoka kuingiza mapato ya shilingi bilioni 1 hadi bilioni 84 ndani ya kipindi cha miaka minne. Hivi sasa shirika linajilipa  mishahara lenyewe, linatoa gawio Serikalini na limepanga kuanzisha miradi mikubwa ya kimkakati kuanzia mwaka wa fedha ujao ili taifa linufaike zaidi. Kuna pia mpango wa kuanzisha kampuni tanzu ya miradi.

12. Local Content & CSR – Ajira kwa Watanzania kwenye sekta ya madini zimeongezeka. Kwa sasa ajira za moja kwa moja ni zaidi ya 19,356, ambapo asilimia 97 ya ajira hizo ni kwa Watanzania. Watanzania pia wanashikilia nafasi nyingi za juu kwenye migodi. Aidha, wameanza kutoa huduma muhimu kama vile utengenezaji wa vifaa vya migodini, hatua ambayo inachochea uchumi wa ndani.

13. Madini Mkakati – Serikali iko mbioni kukamilisha mkakati maalum wa namna ya kuyavuna na kuyaendeleza madini mkakati kama vile graphite, nickel, rare earths n.k., kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo.

14. MBT – Mining for a Brighter Tomorrow – Mpango huu unalenga kusaidia makundi ya wanawake na vijana kwa kuwapatia leseni na maeneo ya uchimbaji. Tayari tumeanza Nyamongo, mkoa wa Mara, kwa kugawa zaidi ya leseni 48 kwa wachimbaji zaidi ya 2000, na wadau mbalimbali wameonyesha nia ya kushiriki katika kuwawezesha makundi haya.

15. Vituo vya Ukodishaji Mitambo – Serikali imeanzisha vituo vya ukodishaji wa mitambo ya kisasa kwa bei nafuu ili kuwasaidia wachimbaji wadogo kuchimba kwa tija na kwa ufanisi zaidi.

16. Gold Coins – Serikali ipo kwenye mazungumzo na Benki Kuu ya Tanzania kuhusu kuanzisha sarafu za dhahabu (Gold Coins) kwa ajili ya uwekezaji na akiba ya thamani. Lengo ni kuwawezesha Watanzania kuhifadhi dhahabu benki na kuitumia kwa malipo kama vile mafuta ya petroli na dizeli.

17. Vikao vya majadiliano na wawekezaji – Serikali inaendelea kufanya vikao vya wazi na wawekezaji wa Sekta ya Madini – wa Kati na Wakubwa – ili kusikiliza changamoto zao na kuzitatua kwa wakati, kwa lengo la kuimarisha mazingira ya uwekezaji nchini.

18. Masoko na vituo vya ununuzi – Serikali imeimarisha upatikanaji wa masoko ya uhakika kwa wachimbaji wadogo kupitia vituo vya ununuzi wa madini. Hatua hii inalenga kuwapa wachimbaji bei nzuri, kuwasaidia kupata mapato ya haki na kudhibiti utoroshaji wa madini nje ya mfumo rasmi. Tuna masoko 43 nchi nzima na Vituo vya Ununuzi 109.

19. Mahusiano ya Kimataifa (MoUs) – Wizara ya Madini imesaini mikataba ya ushirikiano na nchi mbalimbali ikiwemo Uingereza (UK), Sweden, Finland na nyingine nyingi kwa ajili ya kukuza ujuzi, teknolojia na kupata mitaji kwa ajili ya maendeleo ya sekta kwa manufaa ya taifa.

Share:

Related Posts:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © 2025 WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com