Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Omary Mgumba (Mb) akijibu swali bungeni leo tarehe 16 Aprili 2019 wakati wa mkutano wa kumi na tano wa Bunge la Bajeti Jijini Dodoma. (Picha Ziote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Omary Mgumba (Mb) akiteta jambo na Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) bungeni leo tarehe 16 Aprili 2019 mara baada ya kujibu maswali ya wabunge wakati wa mkutano wa kumi na tano wa Bunge la Bajeti Jijini Dodoma.
Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Innocent Bashungwa (Mb) akifuatilia mkutano wa kumi na tano wa Bunge la Bajeti Jijini Dodoma leo tarehe 16 Aprili 2019. Kulia kwake ni Mbunge wa Jimbo la Mlalo Mkoani Tanga Mhe Rashid Abdallah Shangazi.
Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo – Dodoma
Serikali
imeelekeza biashara ya zao la kahawa na mazao mengine kufanyika kupitia vyama
vya ushirika vya msingi (AMCOS) badala ya wanunuzi kwenda kwa wakulima moja kwa
moja.
Naibu
Waziri wa Kilimo Mhe Omary Mgumba (Mb) ameyasema hayo bungeni Jijini Dodoma leo
tarehe 16 Aprili 2019 wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Mbinga
Vijijini Mhe Martin Msuha aliyetaka kufahamu kwanini Serikali ilibadilisha
mfumo wa ununuzi na uuzaji kahawa kwamba ni lazima kupitia Vyama vya Ushirika
vya Msingi pia ni vyama vingapi vya Msingi vya Ushirika (AMCOS) vimeundwa
Wilayani Mbinga kufuatia kubadilishwa kwa mfumo huo.
Alisema
kuwa utaratibu huo utamuwezesha mkulima kunufaika na kilimo cha kahawa kwa
kuzalisha kahawa yenye ubora na kuuzwa kupitia minada ambapo wanunuzi
watashindanishwa na hivyo kupelekea mkulima kupata bei nzuri na yenye tija.
Mhe
Mgumba alisema kuwa Vyama vya
Ushirika huanzishwa na wananchi kutokana na mahitaji yao hivyo, kupelekea
kuwepo kwa aina mbalimbali za Vyama vya Ushirika kama vile Vyama vya Ushirika
wa kilimo na masoko, mifugo, uvuvi, viwanda, nyumba, fedha na madini. Kwa
mujibu wa Sheria ya Ushirika Na.6 ya Mwaka 2013.
Kadhalika,
alisema hadi sasa mkoa wa Ruvuma una jumla ya Vyama vya Ushirika vya msingi
(AMCOS) vya kahawa 67 na chama Kikuu cha Ushirika kimoja (MBIFACU) ambavyo vimeanzishwa
na wakulima wa kahawa katika Mkoa wa Ruvuma. Aidha, Wilaya ya Mbinga ina jumla
ya Vyama vya Ushirika vya msingi vya kahawa 58 ambavyo ndio vitasimamia na
kuendesha biashara ya kahawa katika Wilaya ya Mbinga.
Akijibu
swali la Mhe Conchesta Rwamilaza
ambaye ni Mbunge wa Viti maalumu kuhusu mradi wa kujenga
masoko eneo la Nkwenda na
Murongo katika Wilaya ya Kyerwa, Naibu Waziri wa Kilimo Mhe
Omary Mgumba alisema kuwa Masoko ya
Nkwenda na Murongo katika Halmashauri ya wilaya ya Kyerwa ni kati ya masoko
matano (5) ya kimkakati yaliyopangwa kujengwa kupitia mradi wa Uwekezaji katika
Sekta ya Kilimo Wilayani (District
Agricultural Sector Investment Project – DASIP) na ujenzi ulioanza kutekelezwa
mwaka 2006/07 hadi mwaka 2014.
Alisema masoko mengine yapo katika Halmashauri za; Busoka
(Kahama), Kabanga (Ngara) na Sirari (Tarime). Mradi huo uligharamiwa na Benki ya Maendeleo ya
Afrika (AfDB) na Serikali ya Tanzania.
Mhe Mgumba alisema
kuwa lengo la ujenzi wa masoko hayo ya kimkakati ilikuwa ni kuanzisha mfumo
thabiti wa masoko utakaongeza tija na pato kwa wakulima ndani ya Wilaya.
Alisema kuwa mfumo
huo utajenga mazingira wezeshi kibiashara katika maeneo ya mpakani ili
kurahisisha biashara na nchi jirani na kuinua hali za kiuchumi za wananchi wa
maeneo hayo na uchumi wa Taifa kwa ujumla.
Alisema hadi sasa mradi wa DASIP unafungwa Disemba 2013/14 kazi ya ujenzi wa
masoko hayo ilikuwa haijakamilika na yalikuwa katika hatua mbalimbali za
ujenzi.
Kwa kuzingatia umuhimu wa masoko hayo ya kimkakati
katika Halmashauri husika, Serikali imepanga kukamilisha ujenzi wa masoko hayo
na mengine nchini kupitia Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili
(ASDP II) ambapo katika bajeti ya mwaka 2019/2020 Serikali imetenga Shilingi
bilioni 2.9 kuendelea na ujenzi wa masoko hayo.
MWISHO.
0 comments:
Post a Comment