Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula ameanza ziara ya kutembelea Halmashauri kuu za Chama cha Mapinduzi kwa kata zote 19 za Jimbo la Ilemela kueleza Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi aliyokabidhiwa na chama chake mara baada ya kushinda kiti cha Ubunge mwaka 2015
Mhe Dkt Angeline Mabula leo ameanza kwa kuitembelea kata ya Kayenze kabla ya kufika Sangabuye na baadae kuhitimisha kata ya Bugogwa akiambatana na wataalamu wa Serikali kwa ngazi ya kata husika, madiwani wa kata husika, Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana UVCCM, Katibu wa Umoja wa Wanawake UWT na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa wilaya hiyo
Akiwa katika ziara hiyo Mhe Dkt Angeline Mabula ameeleza juu ya shughuli na miradi mbalimbali ya Uvuvi na Kilimo, Elimu, Afya, Maendeleo ya Jamii na Ustawi, Maji, Miundombinu na Ujenzi iliyotekelezwa katika Jimbo lake kama inavyotaka Ilani ya Uchaguzi ya Chama chake huku akitaja baadhi ya vitu hivyo kuwa ni Uboreshaji wa Elimu na Miundombinu yake kwa kugawa kompyuta kwa baadhi ya shule, kugawa matofali kwaajili ya ujenzi wa madarasa na taasisi nyengine za Umma, kugawa Madawati kwa shule za jimbo lake kupitia fedha za mfuko wa Jimbo, mfuko wa The Angeline Foundation na wadau wengine, Kufungua barabara mfu za mkoloni kupitia fedha za mfuko wa Jimbo na fedha binafsi, kukarabati majengo ya baadhi ya Vituo vya afya kikiwemo Buzuruga, kuwalipia wazee na watu wasiojiweza huduma ya Tiba kwa kadi TIKA, Ujenzi wa madaraja na Ujenzi wa visima vya Maji safi na salama
‘… Ndugu zangu mie ni muuza duka na wenye duka ni nyie chama cha mapinduzi hivyo nimekuja kutoa hesabu za nilichokifanya tangu mnikabidhi duka lenu, Yapo mambo mengi tumeyafanya baada ya kukabidhiwa Ilani ya Uchaguzi na leo tumekuja kuwaeleza tuliyoyafanya kwa kipindi cha miaka miwili tangu mtupe ridhaa hii …’ Alisema
Aidha Mhe Dkt Angeline Mabula hakuacha kuelezea juu ya umuhimu wa zoezi la urasimishaji na upimaji makazi na kuwataka kuhakikisha wanapata hati miliki ya maeneo yao ili kuyaongezea thamani na uhalali huku akiwachangia kiasi cha pesa wakazi wa kata ya Kayenze walipomuomba kuwaunga mkono kufanikisha ujenzi wa shule yao ya Sekondari ili kupunguza adha ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma hiyo sanjari na kuwaomba kutumia nishati ya umeme vijijini REA katika shughuli za uzalishaji kupitia sera ya Serikali ya awamu ya Tano chini ya Mhe Rais Dkt John Magufuli ya Tanzania ya Viwanda
Kwa upande wake Katibu wa Itikadi na Uenezi wa wilaya hiyo Komredi Dennis Lekela Kankono aliyewakilisha Uongozi wa Chama kwa ngazi ya wilaya mbali na kukiri kuridhishwa na utekelezaji wa Ilani unaofanywa na Mbunge Mhe Dkt Angeline Mabula amewataka madiwani na wenyeviti wa mitaa kuiga mfano wa alichokifanya mbunge kwa kuhakikisha wanatoa taarifa za utekelezaji wa Ilani kulingana na ngazi ya halmashauri kuu zao kwa maana ya kata na matawi
‘ Ilemela ni yetu, tushirikiane kuijenga ’
Imetolewa na
Ofisi ya Mbunge
Jimbo la Ilemela
11.01.2018
0 comments:
Post a Comment