METDO Tanzania

METDO Tanzania

Friday, August 6, 2021

WASAIDIZI HUDUMA ZA KISHERIA NCHINI WABAINI CHANZO CHA RUSHWA KUTOKEA KWENYE MABARAZA YA ARDHI

Msajili wa watoa Huduma ya msaada Kisheria Felister Mushi akihitimisha mkutano wa wasaidizi wa huduma za kisheria uliofanyika jijini Arusha.

Na.Faustine Gimu Galafoni.

Mkutano wa wasaidizi wa huduma za sheria hapa nchini ulioandaliwa na Wizara ya katiba na sheria umehitimishwa jijini Arusha huku wadau wakitoa ushauri kwa serikali namna ya kupitia sheria  mbalimbali ikiwemo kuangalia upya uendeshaji wa mabaraza ya ardhi ngazi za kata na wilaya ili kuweza kuondoa mianya ya rushwa inayoweza kujitokeza. 

Akizungumza na mtandao huu mara baada ya kuhitimishwa mkutano huo wa siku mbili Msaidizi wa huduma za kisheria  Malaki Kusekwa kutoka Wilayani Bunda mkoani Mara amesema mabara ya ardhi hutegemea posho kutoka kwa mlalamikaji na mlalamikiwa  jambo ambalo linaweza kuchochea rushwa.   .

“Tuishukuru sana wizara ya katiba na sheria kwa kuandaa mkutano huu nyeti katika masuala ya kisheria,jambo ambalo nimesisitiza ni kuhusu mabaraza ya ardhi ngazi ya kata kutokuwa na fungu na yamekuwa yakitegemea posho kutoka kwa mlalamikaji ama mlalamikiwa ili yaweze kuendesha kesi hali hii huchochea vitendo vya rushwa mtu  akiwa na pesa ndiye mwenye uwanda mpanda wa kushinda kesi hivyo ni vyema jambo hilo likaangaliwa na kupitiwa upya ili mabaraza haya yasitegemee posho kutoka kwa wenye kesi”amesema. 

Wakili Abia Richard kutoka kituo cha Msaada wa kisheria kwa wanawake [Women Legal Aid Centre-WLAC]  amesema pamekuwepo na changamoto ya kesi kukaa muda mrefu bila kuamuliwa chanzo kikiwa ni baadhi ya mawakili wasiokuwa waaminifu ambapo huwa wananunuliwa na watu wenye uwezo ili kuweza  kuwatesa watu wa hali ya chini.

“Unakuta mama masikini anazunguka na majalada zaidi ya miaka miwili au mitatu hili tumeweza kulizungumzia katika kikao chetu kwa kuwa serikali yetu ni sikivu kupitia wizara ya katiba na sheria inaweza kuyafanyia kazi kwanza kuipongeza sana kwa kuona umuhimu wa mchango wetu kwa mstakabali mzima wa taifa letu”amesema. 

Meneja mwandamizi wa program ya Mfuko wa Ruzuku masuala ya sheria Tanzania[LSF] Deogratias Bwire Wamesema hali hii huchochea vitendo vya rushwa kwani mlalamikaji au mlalamikiwa anayetoa fedha nyingi  hupewa kipaumbele zaidi na kushinda kesi ambapo pia wasaidizi hao wa kisheria wamesema pamekuwepo kwa changamoto ya kesi kukaa muda mrefu mahakamani chanzo kikiwa ni mawakili wasiokuwa waaminifu kununuliwa na watenda makosa ili kuhalalisha kushinda kesi.

“Wadau wameainisha changamoto ya tofauti ya takwimu na  changamoto  ya uratibu hivyo ushauri umetolewa kwa wizara mtambuka kukaa pamoja katika kufanikisha masuala mbalimbali ya uratibu”amesema.

Kupitia mkutano huo wasaidizi hao wa huduma za kisheria wamesema umewasaidia kuwajengea uwezo pamoja na kuweza kupitia maboresho ya sheria huku wakitumia fursa hiyo kuipongeza wizara ya katiba na sheria kwa kuwa mstari wa mbele kuwajengea uwezo.

Akihitimisha mkutano huo Msajili wa watoa Huduma ya msaada Kisheria Felister Mushi   amesema mkutano huo utakuwa chachu ya kufanya maboresho ya mfumo wa utoaji haki.

“Huu ni mwendelezo tumeyapokea ambayo tumeyapokea mwisho wake tuweze  kufanya maboresho katika mfumo mzima wa toaji wa haki kwa usawa ,lakini pia suala la uelewa,matumizi ya wanasheria kwenye halmashauri hivyo masuala kama hayo tunaendelea kuyafanyia kazi’’amesema. 

Miongoni mwa mada zilizojadiliwa katika Mkutano huo  wa siku mbili ni pamoja na huduma ya Msaada wa kisheria kabla ya kutungwa Sheria ya Msaada wa kisheria  Na.1 ya mwaka 2017 pamoja na maboresho ya huduma ya Msaada wa kisheria  chini ya Sheria ya Msaada wa kisheria Na 1 ya mwaka 2017.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com