METDO Tanzania

METDO Tanzania

Friday, August 6, 2021

NHC YAANZA MIKAKATI YA KUWEKEZA MAJENGO YA KIBIASHARA MAENEO YA MIPAKANI

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza wakati wa uzinduzi wa nyumba 50 zilizojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) katika eneo la Buhare Musoma mkoani Mara 
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akifungua pazia kuashiria uzinduzi wa nyumba 50 zilizojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) katika eneo la Buhare Musoma mkoani Mara
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akikata utepe kuzindua nyumba 50 zilizojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) katika eneo la Buhare Musoma mkoani Mara
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akitoka kukagua moja ya nyumba alizozizindua zilizojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) katika eneo la Buhare Musoma mkoani Mara

Na Munir Shemweta, MUSOMA

Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limeanza mikakati ya kuwekeza  majengo ya kibiashara katika maeneo ya pembezoni mwa nchi.

Kauli hiyo imetolewa leo Agosti 6, 2021na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Dkt Maulid Banyani wakati wa uzinduzi wa Nyumba za Makazi katika eneo la Buhare wilayani Musoma mkoani Mara uliofanywa na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula.

“Mheshimiwa Naibu Waziri,  kama ulivyoelekeza kwamba, Shirika liwekeze majengo ya biashara  maeneo ya pembezoni mwa nchi yetu, tulishaanza kufanya hivyo eneo la Mutukula, Kagera na sasa tunaangalia uwezekano wa kuwekeza kwenye mpaka wa Kenya na Tanzania” alisema Dkt Banyani.

Kwa mujibu wa Dkt Banyani, Shirika lake kwa sasa linafanya upembuzi yakinifu eneo la Sirari mpaka wa Tanzania na Kenya na uamuzi huo unatokana na timu iliyofanya ziara katika eneo hilo kukuta upande wa kenya umechangamka kibiashara  ukilinganisha na ule upande wa Tanzania.

Alisema, Shirika la Nyumba la Taifa likiwezeshwa ikiwemo kupatiwa ardhi kwa ajili ya uwekezaji majengo  litafanya mabadiliko makubwa na kutolea mfano wa jengo la TRA lilipo mpaka wa Tanzania na Kenya haliko vizuri ukilinganisha na lile la Kenya.

 “Mheshimiwa Naibu Waziri ili eneo la Sirari lichangamke kibiashara  kama ilivyo upande wa pili wa kenya lazima tuwekeze katika majengo ya kibiashara na lengo hapa ni kupendezesha mandhari ya mipaka yetu na kukuza biashara kimataifa” alisema Dkt Banyani.

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza katika uzinduzi huo alisema, mbali na mikakati ya shirika la Nyumba kuwekeza majengo ya kibiashara, halmashauri zilizoko maeneo ya pembezo zinapaswa kuitumia NHC kwa kulipatia ardhi ya kufanya uwekezaji.

“Pamoja na mikakati ya uwekezaji  maeneo ya pembezoni iko haja ya kulitumia shirika la nyumba la taifa kwa kuliwekea miundombinu mizuri ya kibiashara ili liweze kuwekeza maeneo ya mipakani ampapo Tanzania inaonekana iko nyuma ukilinganisha na nchi jirani” alisema Dkt Mabula.
Aidha, Naibu Waziri wa Ardhi alielekeza kujengwa shule ya msingi ya serikali katika eneo la Buhare zilipozinduliwa nyumba 50 baada ya kuombwa kufuatia eneo hilo kutokuwa na shule. Eneo hilo la Buhare lina ukubwa ekari 135 na zilizotumika ni ekari kumi pekee.

Vile vile, Dkt Mabula alitaka maeneo ambayo Shirika la Nyumba linafanya miradi yake, halmashauri husika zihakikishe linawezesha upatikanaji miundombinu kama vile umeme, maji na barabara kwa lengo la kupunguza gharama za upangishaji au uuzaji wa nyumba za shirika la Nyumba la Taifa.

Mkurugenzi wa NHC Dkt Maulid  Banyani katika uzinduzi wa nyumba hizo 50 katika eneo la Buhare alisema,Shirika lake pia limekuwa likitoa huduma kwa jamiii kama sehemu ya kurejesha faida kidogo linayoipata ili kusaidia maendeleo ya wananchi na kufafanua kuwa mwaka 2018 hadi 2020 Shirika lilisanifu na kujenga jengo la utawala la Chuo Kikuu cha Kilimo cha Mwalimu Nyerere kilichopo Butiama na kazi hiyo iligharimu kiasi cha shilingi milioni 200.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com