Na.
Fred Kibano
Mratibu wa Sehemu ya
Elimu Maalum Ofisi ya Rais TAMISEMI, Julius Migea amesema Serikali imeanzisha Mpango wa stadi za Kusoma, Kuandika na
Kuhesabu (KKK) kwa watoto wenye mahitaji maalum ili kuwabaini na kuwawezesha
kumudu stadi hizo muhimu kwa maendeleo yao na Taifa.
Migea aliyasema mjini
Dodoma wakati wa kuanza rasmi kwa zoezi hilo lenye lengo la kuwabaini watoto
wenye mahitaji maalum kama uoni hafifu, viungo vya mwili, kutosikia, kushindwa
kuongea na matatizo mengine.
“Mpango huu wa kukuza
stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) ulianzishwa kwa lengo la
kukabiliana na kiwango duni cha kumudu stadi hizo za msingi kilichobainika
miongoni mwa wanafunzi wa shule za msingi nchini, na watoto waliolengwa ni
wenye umri kati ya miaka mine hadi sita”
Migea alisema kuwa
uendeshaji wa uchunguzi wa nchi nzima kwa watoto wenye umri wa miaka 4 hadi 6 ni
kwa ajili ya kuwabaini watoto wenye mahitaji maalum ili waweze kupatiwa afua
stahiki ikiwa ni pamoja na kuwaandikisha shule stahiki. Kwa hivi sasa, tayari timu
za maafisa waliopewa mafunzo maalum zimekwisha kwenda katika mikoa na
halmashauri zote nchini na wameanza kuwabaini watoto hao wenye mahitaji maalum
wanaoishi katika kata, vijiji, vitongoji na mitaa.
Mmoja wa Waratibu wa
kazi ya kubaini watoto wenye mahitaji maalum Stephen Mwendi amesema zoezi la
kubaini watoto wenye mahitaji maalum mkoani Dodoma linaendelea vizuri katika
wilaya ya Kondoa Mji na Halmashauri ya Kondoa, baada ya kumaliza Halmashauri ya
Manispaa ya Dodoma na baada ya hapo watakwenda katika halmashauri nyingine za
mkoa wa Dodoma.
“sisi tunaendelea vizuri
na zoezi la kuwabaini watoto wenye mahitaji maalum katika Halmashauri ya Mji
Kondoa na Halmashauri ya wilaya ya Kondoa na tunatarajia zoezi litakamilika kwa
wakati kwani vituo karibu vyote vinafikika”
Mwendi pia amezitaja
baadhi ya changamoto zinazowakabili katika zoezi hilo kuwa ni za kawaida lakini
wanatarajia taarifa ya mwisho itawasilishwa Serikalini ili kuifanyia kazi kwa wakati
katika sekta hiyo muhimu.
“muda wanaofika
walengwa wakati mwingine wanafika tukiwa tumeondoka na kutulazimu kuwarudia
tena, pia mahitaji yaliyoanishwa katika ubanishaji ni miaka 4 hadi 6 lakini
tunakutana na watoto wengi wa umri zaidi ya miaka 10, 18 ijapokuwa kwa
kuwaangalia wanakuwa na maumbo madogo kama watoto na vile vile wengi wa wazazi
wanafikiria kuwa zoezi hilo ni kwa ajili ya kuwapatia misaada jambo ambalo si
kweli na hivyo tunaendelea kuwaelimisha”
Mmoja wa wazazi
walioleta watoto katika Halmashauri ya Kondoa Mji, mama wa Abubakari Hussein
amesema mwanaye alipata ulemavu wa viungo alipokuwa na miaka 4 hadi sasa ambapo
ana miaka 16 anapatanaye shida sana na anaoimba Serikali imsaidie kumsomesha
mtoto huyo na kumpatia mahitaji madogo madogo kwani anaishi katika nyumba ya
kupanga, lakini pia Serikali iwajengee shule maalum kwa ajili ya watoto wa aina
hiyo ambao wamevuka umri wa kuandikishwa wa miaka 4 hadi 6.
Katika Halmashauri ya wilaya
ya Kondoa kata ya Mnenia, mmoja wa wazazi, Mussa Dudu amesema mjukuu wake Haji
Twalib ambaye anatatizo la kichwa kikubwa, kutokuongea vizuri na tumbo kuwa
kubwa amepata ushauri wa kitaalam ikiwa ni pamoja na kujaza fomu ya kumwona
daktari na fomu ya kujiunga na shule na ametoa maoni kwa Serikali kufanya
utafiti zaidi kwani kuna baadhi ya wazazi wanaficha watoto wao wenye ulemavu (mahitaji
maalum) majumbani.
“nashukuru juhudi za
Serikali kwa zoezi hili zuri kwani kijana wangu (mjukuu) hakuwahi kupata
uchunguzi wowote, nimepata fomu ya ubainishaji ili niende hospitali na kupeleka
shuleni, Serikali pia itupe msaada ili kuweza kuwahudumia watoto hawa na pia
Serikali ifanye uchunguzi kamili kwani kuna watoto wanafichwa tu na wazazi
hawahamasiki wanasema huyu ni mlemavu tampeleka wapi. Pia natoa wito kwa
Serikali kuwatumia Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji ili kuweza kuwafichua
wototo kama hao”
Ubainishaji wa kundi la
watoto wa aina hii kawaida unatakiwa kufanyika kabla ya zoezi la uandikishaji
ili wapatiwe afuastahiki, kwani awali zoezi hili lilikuwa halifanyiki kabla ya
kuanza masomo na kupelekea watoto wenye changamoto za kujifunza kutokuwa na
maendeleo mazuri ya kitaaluma, kuacha masomo, kutopenda masomo na kukosa haki
yao ya msingi kutokana na kuwa katika mazingira yasiyo rafiki ya kusomea.
Serikali imekuwa ikitekeleza
Mipango mbalimbali katika sekta ya elimu, ambapo kwa hivi sasa kupitia Mpango
wa Kukuza stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (Literacy and Numeracy
Education Support - LANES) inatekeleza mikakati ya kuhakikisha wanafunzi wote
walioandikishwa shule za Msingi wanapata stadi za KKK ambazo ni msingi muhimu
wa maendeleo ya kitaaluma katika ngazi zingine za Elimu.
0 comments:
Post a Comment