METDO Tanzania

METDO Tanzania

Sunday, August 8, 2021

SHAKA: CHAMA CHA MAPINDUZI KINAJIAMINI NA KUJITEGEMEA KIFIKRA


Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema uwezo wa viongozi na makada wa chama hicho unatokana na utayari, uthubutu na kuujua umma unataka nini, kwa wakati upi na namna ya kutimiza mahitaji husika kulingana na changamoto zinazowakabili wananchi.

Pia kimesema chama cha siasa ambacho hakiwezi kuheshimu matakwa ya wanachama,  wananchi na Taifa  hutanguliza maslahi binafsi ya viongozi kuliko maslahi mapana ya umma kama wafanyavyo upinzani na hapo ndipo penye tofauti kati yao na chama tawala.

Hayo yamesemwa jana na katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Itikadi na Uenezi Shaka Hamdu  Shaka alipoulizwa iwapo CCM ina utofauti na upinzani alisema kuna utofauti kati ya viongozi wake na upinzani vivyo hivyo katika ubora wa muundo na sera CCM huwezi kukifananisha na chama chochote nchini.

Shaka alisema kwanza vyama  upinzani hivyo  ukiacha kuwa ni vichanga, havijawa na uzoefu wa kutosha, viongozi  wake wamepatikana nje ya mifumo yenye kuaminika kwa jamii ikiwemo kutokimbazana na mahitaji ya wakati.

Alisema  mfano chadema iwapo kingelikuwa kinafanya tathmini au tafiti za kisiasa toka kwa wanachama wake na makundi mengine ndani ya umma kutaka kufahamu ajenda  ipi ni kipaumbele kwa wakati huu kati ya uchuni na katiba mpya, basi takwimu zingewaonesha kipaumbele namba moja ni uchumi.

Katika hili tunawakumbusha wakafanye rejea kwenye utafiti wa TWAWEZA sauti za wananchi ambao ulionesha vipaumbele vya wananchi na katika hivyo katiba haikuwepo, wananchi walitaja maji, afya, elimu, rushwa, miundombinu na uchumi. 

Alisema kutokana na chama hicho (Chadema) kushindwa kufanya  tafiti za msingi zenye kwenda sanjari na mahitaji ya wakati, ndiyo  maana kila wakati  kimekuwa kikijikuta kikishindana na nguvu za upepo kwa mujibu wa  wakati ndio maana hakijui kama uchumi wa watu ni kipaumbele cha kwanza na vingine hufuata baadaye.

"Chama bora na makini hujikita katika tafiti za kitaalamu kila mara ili kuweza kufahamu mahitaji ya wananchi na Taifa pamoja na namna nzuri ya kuyakamilisha.  Matakwa na mahitaji ya wakati yanapopishana na kuanza kuchomoza  ukaidi wa viongozi ni dosari na kiashiria kuwa chama husika kimepoteza ushawishi wake na kipo hatarini kuingia makumbusho ya kisiasa. Nguvu ya ushawishi sio uwezo wa kupaza sauti bali ni uwezo wa kuyaishi mahitaji ya wakati kwa njia sahihi." Alisema shaka.

Alisema kila  madhumuni, shabaha, sera na malengo yenu kadri mnapoitazama jamii  hapo ndipo mnapotakiwa  kusimama pamoja kama viongozi huku mkiwa mmejitayarisha, mnajiamini na  kujitegemea kifikra katika msimamo mmoja wenye manufaa ya wengi.

Aidha katibu mwenezi huyo alisema viongozi wasiojiamini kamwe hawawezi kuendeleza  malengo  yao ya msingi. Maana hawana moyo wa uvumilivu na subira hivyo ni vigumu sana kumudu migogoro ndani ya vyama wanavyoviongoza. Vyama vya upinzani vina viongozi wa aina hii wasiojiamini ndio sababu migogoro haikomi na vinadumaa.

"Sifa ya CCM ni  bidii, utayari, umoja  wake madhubuti, subira na ustahimilivu. Hayupo anayeweza kutenda na kutekeleza mawazo au fikra zake bila kupatikana uamuzi na msimamo wa  pamoja. Hivyo vikao ni muhimu sana kuliko uwezo binafsi wa mtu. Siku zote CCM huamua mambo yake kwa kutazama mahitaji ya wengi kupitia vikao" Alisema 

Shaka alisema aina ya viongozi wenye kuelewa hayo na kuyasimamia huwezi kuwakuta kwenye vyama vingine badala yake huko jamii itakutana na wapigania madaraka, wapenda vyeo na utawala na wala hutawaona viongozi  au wanasiasa makini.

"Yapo mataifa yenye katiba zinazoitwa katiba bora. Cha ajabu mataifa hayo yapo kwenye ukabila,  milio ya risasi, mapigano na umwagaji damu wao kwa wao. Yote ni kwa sababu wanasiasa wanapambana kusaka vyeo na kutafuta urahisi wa kupata madaraka ya kiutawala. Tanzania imepata gharama kubwa kujenga misingi ya amani, umoja, mshikamano iliyonayo leo ikiwa imewekewa misingi thabiti kwenye katiba. Kwa sasa tushirikiane na tushikamane vizuri kujenga uchumi kwanza." Alisisitiza shaka

Mwisho 
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com