Serikali
imesema kuwa itahakikisha inashughulikia mtandao wa wafanyabiashara
wakubwa wanaojihusisha na dawa za kulevya bila ajizi, ambapo vyombo
vyote vya kisheria vimeagizwa kushirikiana kwa kusimamia sheria
ipasavyo.
Hayo
yalisemwa jana Jijini Dar es salaam na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
wakati wa ufunguzi wa kongamano linalohusu mmomonyoko wa maadili na
athari za dawa za kulevya lililoandaliwa na Baraza Kuu la Waislamu
Tanzania (BAKWATA) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana
na Dawa za Kulevya.
Alisema
kuwa kila mzazi au mlezi aone aibu, uchungu na ajutie anapoona mtoto
yoyote akienda kinyume na utaratibu wa kawaida wa maisha na ni vema
wakatumia nafasi yao kwa kuwahimiza vijana hao waishi maisha ya nidhamu
na yenye kumpendeza Mwenyezi Mungu.
“Ni
ukweli usiopingika kuwa mmomonyoko wa maadili ni miongoni mwa vichocheo
vinavyopelekea matumizi ya dawa haramu za kulevya, hivyo ni matarajio
yangu kuwa mtaliangalia kwa kina tatizo la mmomonyoko wa maadili ambalo
kwa kiasi kikubwa linatuathiri kama Taifa katika mipango ya Serikali na
maendeleo ya Taifa letu,” alisema Majaliwa.
Aidha,
aliongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kujenga jamii
yenye kuzingatia maadili nchini na Rais, Dkt. John Magufuli amekuwa
akisisitiza Watanzania wote kuzingatia maadili katika jamii kwa kufanya
kazi kwa bidii na kujiepusha na vitendo vyote vya rushwa na ubadhirifu.
Naye
Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za
Kulevya nchini, Rogers Siang’a aliwaomba viongozi wa dini kuunga mkono
Mamlaka hiyo kwa sababu inafanya kazi kubwa ambayo inahitaji msaada wa
watu wote.
Kwa
upande wake Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Alhaji Abubakary Zuberi
alisema viongozi wa dini nchini wana jukumu la kukataza maovu na
kuiamrisha jamii kufanya mambo mema badala ya kuiachia Serikali pekee
kufanya kazi hiyo.
0 comments:
Post a Comment