METDO Tanzania

METDO Tanzania

Wednesday, April 12, 2017

MAAFISA MAENDELEO YA JAMII WAASWA KUTUMIA TAALUMA YAO KULETA MABADILIKO KATIKA JAMII

Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Ndg.Jumanne Sagini akizungumza na Maafisa maendeleo ya Jamii wa Halmashauri na Mikoa ya Kanda ya Ziwa katika kikao kikao chao cha kanda kilichofanyika Mjini Bariadi


Mwenyekiti aliyeongoza kikao cha Maafisa Maendeleo ya Jamii Kanda ya Ziwa ambaye ni Afisa Maendeleo ya Jamii katika Halmashauri ya Wilaya Serengeti, Ndg.Wambura Sunday akizungumza na maafisa hao (hawapo pichani) katika kikao cha kanda Mjini Bariadi



Baadhi ya Maafisa maendeleo ya Jamii wa Halmashauri na Mikoa ya Kanda ya Ziwa wakimsikiliza Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Ndg.Jumanne Sagini(hayupo pichani) katika kikao kikao chao cha kanda kilichofanyika Mjini Bariadi


Na Stella Kalinga

Maafisa Maendeleo ya Jamii wametakiwa kutumia taaluma yao kuleta mabadiliko katika jamii kwa kubaini fursa mbalimbali zinazoweza kuwaletea wananchi maendeleo katika maeneo yao.

Wito huo umetolewa na Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Ndg.Jumanne Sagini katika ufunguzi wa Kikao cha Maafisa Maendeleo ya Jamii kutoka katika Halmashauri na Mikoa ya Kanda ya Ziwa kilichofanyika Mjini Bariadi.

Sagini amesema kutokana na taaluma yao Maafisa Maendeleo ya Jamii wanaweza kuwasiliana na jamii na kueleweka kwa urahisi zaidi hivyo watumie fursa hiyo kuwashauri wananchi na vikundi mbalimbali kufanya shughuli zinazoweza kuwaingizia kipato ili waondokane na umaskini.

Amesema wananchi wengi wanafanya shughuli mbalimbali lakini wanakosa elimu, uwezeshwaji na taarifa sahihi za masoko na mitaji  ili kuendeleza shughuli wanazofanya, hivyo akawataka kutimiza wajibu wao katika kuelimisha na kuihamasisha jamii kuunda vikundi  hususani vijana na wanawake ili watambuliwe na kuwezeshwa.

Akizungumzia namna Maafisa Maendeleo ya Jamii katika mkoa wa Simiyu walivyoshiriki katika maendeleo ya Simiyu ya Viwanda, amesema walibaini vikundi vya vijana katika maeneo yao na kubuni uanzishwaji wa viwanda vidogo wiwili ambavyo ni Kiwanda cha kutengeneza Chaki (Maswa) na Kiwanda cha kusindika maziwa(Meatu).

“Maafisa Maendeleo ya Jamii wangu walishirikiana na Wakurugenzi wakabaini fursa mbalimbali  kwenye maeneo yao na vikundi vya vijana ambavyo kwa sasa vinaendesha miradi ya viwanda kwa kushirikiana na Halmashauri, kiwanda cha kutengeneza chaki kilichopo Maswa na kingine cha kusindika maziwa kipo Wilaya ya Meatu” alisema.

“Nawashauri na ninyi mfanye vitu vitakavyofanya mtambuliwe, fanyeni yale yanayogusa shida za wananchi, mkifanya hivyo wananchi watawatambua, viongozi watawatambua na Mungu pia atawatambua” alisema.

Mwenyekiti aliyeongoza kikao cha Maafisa Maendeleo ya Jamii Kanda ya Ziwa ambaye ni Afisa Maendeleo ya Jamii katika Halmashauri ya Wilaya Serengeti, Ndg.Wambura Sunday amesema maafisa hao wanafanya jitihada mbalimbali katika maeneo yao na wanaiomba Serikali iwasaidie kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili katika utendaji wao.

Aidha, Wambura amesema kikao chao kimependekeza uanzishwaji wa Chama cha wana taaluma ya Maendeleo ya Jamii Tanzania ili kudhibiti ubora na viwango vya utoaji huduma katika Taaluma ya Maendeleo ya Jamii. 

Kikao cha Maafisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri na Mikoa ya Kanda ya Ziwa  kimefanyika kwa lengo la kubadilishana uzoefu na kupashana habari juu ya masuala mbalimbali ya utendaji wa sekta hiyo na vikao kama hivi vimefanyika katika kanda nyingine sita za Tanzania katika maeneo tofauti.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com