METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, April 25, 2017

Bunge Laibana Serikali Kuhusu Wachimbaji Waliofukiwa Machimbo ya Kitunda

Bunge limeiagiza serikali kufuatilia na kupeleka majibu kuhusu tukio la kufukiwa kwenye mgodi kwa wananchi wanaochimba madini katika machimbo ya Kata ya Kitunda, wilayani Sikonge, Tabora pamoja na kupata idadi kamili ya waliofukiwa.

Agizo hilo lilitolewa bungeni jana na Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Zungu (pichani) wakati akijibu mwongozo ulioombwa na Mbunge wa Sikonge, Joseph Kakunda (CCM) aliyeomba mwongozo kwa kuwa alikuwa na jambo zito la kitaifa kutokana na kufukiwa kwa wachimbaji hao, hivyo kuiomba serikali ilifanyie kazi na kupatiwa ufumbuzi wakina.

Zungu alimpa pole mbunge huyo na wote waliofikwa na tukio hilo, huku akiiagiza serikali kulifanyia kazi kupitia wizara zinazohusika kwa kushirikiana na mbunge na wananchi wa maeneo hayo ili kupata uhakika wa idadi kamili ya waathirika.
 Pia aliwataka kuhakikisha maeneo kama hayo hayapati tena madhara makubwa, na wabunge kwa umoja wao katika maeneo yao waisaidie serikali.

Alisema wakati mwingine wabunge wamekuwa wakivunja sheria na masharti ambayo yanawekwa na serikali kuhusu mambo mbalimbali ili tu wapate kukubalika kwa wapiga kura wao. 
“Nilivyoingia bungeni tangu asubuhi nimepokea maswali na pole nyingi kutoka kwa wabunge kutokana na tukio la kufukiwa kwenye mgodi wa wananchi wa Tanzania wanaochimba kule Kitunda,” alisema Kakunda wakati wakiwasilisha mwongozo wake.

Kakunda alisema idadi kamili ya wachimbaji katika mgodi wa Kitunda haijulikani kwa sababu hakuna usajili wowote wa wanaoingia au kutoka katika mgodi huo. Alisema serikali inakadiria kwamba kuna wachimbaji kati ya 5,000 hadi 7,000. 
“Sasa mheshimiwa mwenyekiti usiku wa kuamkia Aprili 20 mwaka huu, machimbo hayo yalipata ajali na walifukiwa wananchi na mpaka jana (juzi) Aprili 23 mwaka huu ilifukuliwa miili sita.

"Mheshimiwa Mwenyekiti wananchi wanaamini, na wachimbaji wa eneo hilo wanaamini kwamba kuna wananchi zaidi bado wapo chini ya machimbo hayo, sasa mheshimiwa mwenyekiti ilitumika kijiko cha ujenzi wa barabara badala ya vifaa maalumu ambavyo huwa vinatumika kwenye migodi mikubwa kufukua ardhini kuokoa pamoja na kufukua maiti,” alisema.

Mbunge huyo, katika mwongozo wake aliomba kutoa hoja, Bunge hili lijadili hoja yake kwa kanuni kama kanuni zinavyowaongoza ili maazimio watakayofikiwa yatoe mwongozo kwa serikali na kuweka utaratibu wa usimamizi wa usajili na uratibu na msaada wa haraka wa tatizo kama hilo linapojitokeza ili kuondoa manung’uniko ya wananchi na hata wabunge yanapotokea majanga kama haya ya Kitunda kwenye migodi.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com