METDO Tanzania

METDO Tanzania

Wednesday, April 12, 2017

RAIS MAGUFULI AWEKA JIWE LA MSINGI UJENZI WA RELI YA KATI (STANDARD GAUGE) SEHEMU YA DAR ES SALAAM HADI MOROGORO

Na Mathias Canal, Dar es salaam

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli Leo April 12, 2017  ameweka jiwe la msingi kuzindua ujenzi wa Reli ya kati mpya na ya kisasa ya umeme (Standard Gauge) sehemu ya Dar es salaam hadi Morogoro.

Tukio la uzinduzi limefanyika katika Stesheni ya Pugu Wilaya ya Ilala Jijini Dar es salaam na ujenzi utakapokamilika Treni hiyo itakuwa na uwezo wa kusafiri Kilomita 160 kwa Saa.

Katika hafla hiyo iliyohudhuriwa na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prf Makame Mbarawa (Mb), Balozi wa Uturuki Mhe Yesamin Eralp, Mwakilishi wa Benki ya Dunia Tanzania, Burundi, Malawi na Somalia Bi Bella Bird na Mwakilishi wa Maendeleo ya Afrika, sawia, Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe Paul C. Makonda, Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi Ndg Humphrey Polepole na viongozi wengine mbalimbali wakiwemo wananchi wa Mkoa wa Dar es salaam, Rais Magufuli ameamuagiza Prf Mbarawa ujenzi utakapoanza kuwaajiri wananchi waliohudhuria kwenye sherehe hizo za uwekaji wa jiwe la Msingi.

Rais Magufuli amesema kuwa ujenzi wa Reli hiyo ya kisasa utatumia gharama kubwa hivyo watanzania wote wanapaswa kutumia fursa ya ujenzi huo kwa kuongeza kasi ya uzalishaji na ufanyaji kazi ili kukuza kipato cha kila mwananchi na maendeleo ya Tanzania kwa ujumla.

Rais Magufuli ameeleza kuwa baada ya kukamilika kwa ujenzi wa Reli hiyo ya kisasa itarahisisha usafirishaji wa Mizigo na Abiria, Itakuza Biashara kati ya Tanzania na Nchi zingine kama Rwanda, Burundi, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Faida zingine ni pamoja na kukuza sekta ya uchumi nchini katika nyanja za Madini, Utalii, Kilimo na mifugo sambamba na Kurahisisha usafirishaji wa Malighafi.

Rais Magufuli pia amezitaja Faida za Reli hiyo ya kisasa kuwa ni pamoja na Kusaidia kutunza barabara nchini kwani usafirishaji wa mizigo kupitia reli ndio njia sahihi itakayoziwezesha barabara kutokuwa na magari mengi hivyo kudumu kwa kipindi kirefu.

Sambamba na hayo pia Rais Magufuli alisema kuwa baada ya kukamilika kwa ujenzi wa Reli idadi ya wananchi kuajiriwa inataraji kuongezeka ambapo takribani watu 600,000 watapata ajira huku 300,000 kati yao wakiwa kwenye ajira za kudumu lakini pia watu zaidi ya milioni moja watapata ajira za Moja kwa moja kupitia sekta ya viwanda.

Ujenzi huo wa Reli ya kati ya Kisasa (Standard Gauge) unataraji kukamila katika kipindi cha miezi 30 ambapo hata hivyo Rais Magufuli ameelekeza ikiwezekana kumalizika mapema ujenzi huo kwani fedha zote zilizotengwa kwa ajili ya ujenzi huo zipo tayari.

Ujenzi wa Reli ya Kati ya Kisasa (Standard Gauge) kutoka Dar es salaam mpaka Morogoro utahusisha ujenzi wa Stesheni sita ambapo takribani Dola 1.22 sawa na Shilingi Tilioni 2.8 za kitanzania zitatumika.

Hata hivyo ujenzi utakapokamilika utarahisisha huduma za usafiri ambapo safari ya kutoka Dar es salaam mpaka Dodoma itatumia masaa 2:45 na safari ya kutoka Dar es salaam mpaka Mwanza inataraji kutumia Masaa 7:40.

Rais Magufuli alisema kuwa kwa wastani huo wa muda kutakuwa na matokeo chanya na kuleta Faida kwa Bandari ya Dar es salaam kwani mizigo itatoka kwa haraka bandarini na kuwafikia wananchi kwa wakati.

Ujenzi wa Reli ya kati na ya kisasa (Standard Gauge) utakapokamilika itaifanya Treni ambayo inatarajiwa kuwa na Urefu wa Kilomita mbili na mabehewa 1000 kuwa na uwezo wa kubeba tani 35 za mizigo na kufikia Tani Milioni 17 kwa mwaka zaidi ya Tani milioni 12 ukilinganisha na Treni ya sasa yenye uwezo wa kubeba Tani milioni Tano kwa mwaka.

Sambamba na hayo pia Rais Magufuli alisema kuwa nchi ya Tanzania inapaswa kuwa na maendeleo makubwa kutokana na Rasilimali nyingi ilizonazo ikiwemo madini na tayari umetolewa mkopo kwa ajili ya ujenzi wa mwendokasi awamu ya tatu kutoka Gongolamboto hadi maeneo ya mjini.
Mwisho
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com