Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF) limepokea kwa furaha maamuzi yaliyotolewa na Kamati ya Utendaji ya
CAF ya kuipa Tanzania nafasi ya kucheza fainali za Afrika za vijana
chini ya umri wa miaka 17 (Afcon U17). Mashindano haya yatanyika nchini
Gabon kuanzia tarehe 21 Mei, 2017 hadi 04 Juni, 2017.
Timu nane zitashiriki fainali hizi na
zimegawanywa makundi mawili, kundi A ni Gabon, Ghana, Guinea, Cameroon
na kundi B ni Mali, Niger, Angola na Tanzania. Washindi wawili wa kila
kundi wataliwakilisha bara la Afrika katika fainali za dunia huko India
mwezi Novemba mwaka huu.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
linatoa shukrani za pekee kwa Mh. Rais Dr John Pombe Magufuli kwa
jitihada za Serikali kusapoti michezo, tunamshukuru sana Mh. Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa Kassim kwa kutupa shime na kufuatilia kwa karibu
maendeleo ya timu.
Shukrani kwa Mh. Nape Nnauye na Wizara
kwa ushirikiano wa karibu aliotupatia wakati wote wa kuandaa timu na
kuelekea kwenye mashindano hatua ya mtoano.
Tunamshukuru sana Bw. Issa Hayatou Rais
wa CAF na Kamati yake ya Utendaji kwa kututendea haki, Bw. Leodeger
Tenga Rais wa heshima wa TFF na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya CAF
tunamshukuru na kumpongeza sana kwa jitihada binafsi alizofanya
kuhakikisha haki ya Tanzania haipotei.
Ninaishukuru sana Kamati ya Utendaji ya
TFF, Chama cha Mpira Zanzibar ZFA, Kamati ya Mpira wa Vijana ikiongozwa
na Bw. Ayoub Nyenzi, viongozi wa vyama vya mpira vya Mikoa, na
Sekretariet ya TFF ikiongozwa na Katibu Mkuu Bw. Mwesigwa Selestine kwa
kazi kubwa waliyoifanya kusimamia timu.
Tunamshukuru Dr. Paul Marealle mjumbe wa
Kamati ya Tiba ya CAF na Mwenyekiti wa Kamati ya Tiba ya TFF kwa
kufuatilia kwa karibu suala hili na kutoa ushauri wa kitaalam kwa TFF.
Shukrani za pekee kwa washirika wetu Azam Media, Airtel, Coca Cola na Kampuni ya SS Bakhresa. Mchango wao ni mkubwa katika kufikia mafanikio haya.
Shukrani za pekee kwa washirika wetu Azam Media, Airtel, Coca Cola na Kampuni ya SS Bakhresa. Mchango wao ni mkubwa katika kufikia mafanikio haya.
Wazazi wa vijana wetu wa Serengeti Boys
tunawashukuru kwa kuwaruhusu watoto wao washiriki kwenye mashindano
haya. Tunaomba waendelee na moyo huo.
Pongezi nyingi sana kwa wachezaji wetu
Serengeti Boys na benchi lao la ufundi kwa kututoa kimasomaso na
kuhakikisha bendera ya Tanzania inapeperushwa Gabon mwezi Mei. Kazi
kubwa mmeifanya, mmepambana na timu kubwa na mkatoka mashujaa.
Mmeiondoa Seycheles mashindanoni, mkaiondoa timu kubwa ya Afrika Kusini
mashindanoni na mkataoa sare ya jumla ya mabao 3-3 dhidi ya Kongo na
kutolewa kwa bao la ugenini. Wapinzani wetu Kongo hawakutenda haki kwa
kuchezesha wachezaji wakubwa kwa umri. CAF walipowaagiza, si mara moja,
ila mara tatu kuwa wamlete mchezaji husika anayetuhumiwa kuzidi umri
hawakufanya hivyo na wakatolewa mashindanoni.
Safari ya kwenda Gabon haikuwa fupi
ilikuwa ndefu. Kufuatia maono ya mbali ya TFF safari hii ilianza mwaka
2014 mara tu baada ya mashindano ya Copa Coca Cola ambayo yalihusisha
vijana umri chini ya miaka 15 wakati huo. Wachezaji bora katika
mashindano hayo walikusanywa pamoja wakawekwa kambini na kuanza mazoezi
yaliyoambatana na ziara za mechi za majaribio mikoani. Ni katika ziara
hizi vipaji vipya vilionekana na kuongezwa kwenye timu.
TFF inavishukuru sana vyama vya mpira
vya India, Seychelles, Madagascar, Rwanda na Korea Kusini kwa
kufanikisha kambi za kimataifa za Serengeti Boys. Kambi hizi zilitoa
fursa kwa vijana wa Serengeti Boys kupata uzoefu wa kimataifa kupitia
michezo ya kujipima nguvu waliyocheza dhidi ya timu kubwa duniani kama
Marekani, Korea Kusini, Misri, Malasyia, Madagascar na India.
Tunayashukuru sana makundi yote ya
mashabiki wa timu zetu za Taifa kwa kutoa hamasa wakati wote Serengeti
Boys ilipocheza. Washiriki mbali mbali kwenye mitandao ya jamii
tunawashukuru kwa kufuatilia kwa karibu maendeleo ya timu na kuwatia
moyo vijana. Tuendelee na moyo huu.
Vyombo vya habari tunavishukuru sana kwa kutoa taarifa mbali mbali zinazohusu timu, kuandika makala na kuhamasisha vijana.
Sasa tunayo kazi kubwa mbele yetu,
kuhakikisha Tanzania inarudi na Kombe toka Gabon. Nimeliagiza benchi la
ufundi liandae program ya maandalizi ya timu kuelekea Gabon 2017.
Program hii itahusisha kambi ndani ya nchi (ambayo tayari imeanza) na
kambi ya angalao mwezi mmoja nje ya nchi, TFF iko mbioni kutafuta kambi
hii na karibu tutafanikiwa kuipata, itakuwa ni katika nchi iliyoendelea
kisoka.
Serengeti Boys haina mdhamini. Gharama
za maandalizi ni kubwa na hazitapungua dola za kimarekani laki nne na
zitajumuisha gharama za mechi za majaribio (gharama za mechi hizi
hazipungui dola 50,000.- kwa kila mechi), gharama za kambi ndani ya
nchi, gharama za kambi nje ya nchi ambazo hazitapungua dola laki moja
($100,000), usafiri wa kwenda na kurudi Gabon,gharama za timu wakati wa
mashindano ikiwemo usalama wa timu Gabon, pamoja na vifaa na matumizi
mengine. TFF kupitia mfuko wake wa TFF Football Development Fund
itafanya kila jitihada kuhakikisha pesa hizi zinapatikana ili
kuhakikisha timu yetu inafanya vizuri Gabon. Hatutaki viwepo visingizio
kama ambavyo huwa inatokea kwa nchi nyingine.
Tunatoa wito kwa Serikali, mashirika
binafsi na umma, watu binafsi, makundi mbali mbali ya jamii kwa pamoja
tushirikiane tuhakikishe kila kinachohitajika kinapatikana ili
kuhakikisha mafanikio ya timu. Sekta ya umma na ya binafsi karibu mtoe
ushamini kwa Serengeti Boys ili nanyi mkuze jina la biashara zetu.
Bahati nzuri jina la Serengeti Boys linachukua jina la moja ya vivutio
vyetu vikubwa vya utalii, hii ni fursa kubwa ya kutangaza jina la nchi
yetu na vivutio vyake vya utalii kupitia timu hii na fainali hizi za
Afrika.
Fainali hizi za Afrika zitakuwa ni fursa
pekee kwa wachezaji wa Tanzania kuingia kwenye anga za Kimataifa.
Wachezaji wengine wakubwa duniani wakiwemo kina John Obi Mikel,
Celestine Babayaro, Nwanko Kanu, Kelechi Ihenacho, Samuel Kuffour, Nii
Lamptey, Michael Essien wametokea kwenye fainali hizi.
Ushiriki wa Tanzania katika fainali hizi
itakuwa ni fursa ya pekee ya kuwa hamasisha wadau wa mpira wa miguu
Tanzania ili na sisi tuweze kuanda fainali zijazo nzuri za Afrika za
vijana chini ya umri wa miaka 17 mwaka 2019. Tanzania ni mwenyeji wa
fainali hizi. Siku ya fainali ya Gabon Afcon U17 kabla ya kombe
kutolewa Tanzania tutakabidhiwa rasmi utambulisho wa kupokea
mashindano haya toka kwa Gabon .
Ninaomba nimalizie kuwaomba Watanzania
wenzangu timu yetu ya Serengeti Boys tuiweke kwenye sala na dua zetu ili
izidi kupata mafanikio.
Mungu ibariki Serengeti Boys.
Mungu ibariki Tanzania.
Mungu ibariki Afrika.
Ahsanteni sana.
Jamal Malinzi
Rais Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
DAR ES SALAAM
07 FEBRUARI, 2017.
Jamal Malinzi
Rais Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
DAR ES SALAAM
07 FEBRUARI, 2017.
0 comments:
Post a Comment