Mkaguzi wa ndani wa Halmashauri ya
Manispaa ya Mtwara, Bw. Hussein Mussa, pamoja na maafisa wengine
wakiendelea na zoezi la uhakiki wa wastaafu wanaolipwa na Wizara ya
Fedha na Mipango, mkoani Mtwara.
Baadhi ya Wastaafu wanaolipwa na Wizara
ya Fedha na Mipango, wakikagua nyaraka zao muhimu kabla ya kufika katika
dawati la huduma kwenye zoezi la uhakiki linaloendelea mkoani Mtwara
Afisa TEHAMA Mwandamizi kutoka Wizara ya
Fedha na Mipango, Bi. Jacqueline Nyamugali (wa kwanza kushoto) akiwa na
maafisa wengine, wakitoa maelekezo kuhusu nyaraka muhimu za mmojawapo
ya wastaafu wanaolipwa na Wizara ya Fedha na Mipango wakati wa zoezi la
uhakiki linaloendelea mkoani Mtwara.
Kaimu Mhasibu Mkuu Pensheni, Scolastica
Mafumba, akikagua nyaraka na kutoa maelekezo muhimu kwa mmojawapo ya
wastaafu wanaolipwa pensheni na Wizara ya Fedha na Mipango waliofika
kuhakikiwa mjini Mtwara.
Mkaguzi wa ndani wa Halmashauri ya
Manispaa ya Mtwara Bi. Imelda Mmbaga akimhudumia mmoja wa wastaafu
wanaolipwa na Wizara ya Fedha na Mipango, wakati wa zoezi la uhakiki
linaloendelea katika mikoa ya Lindi na Mtwara Mtwara.
Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali
Msaidizi, Bw. Stanslaus Mpembe, akiongea na waandishi kutoka vyombo
mbalimbali vya habari nchini kuhusiana na zoezi zima la uhakiki wa
wastaafu wanaolipwa na Wizara ya Fedha na Mipango linaloendelea katika
mikoa ya Lindi na Mtwara. (Picha na Kitengo cha Mawasiliano
Serikalini-WFM)
Na Benny Mwaipaja-WFM, Mtwara
WIZARA ya Fedha na Mipango, imesema kuwa
wastaafu wanaolipwa na Wizara hiyo ambao hawatahakikiwa wataondolewa
kwenye orodha ya malipo ya pensheni kwa kuwa watakuwa wamekosa sifa.
Kauli hiyo imetolewa Mjini Mtwara na
Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali Msaidizi, Bw. Stanslaus Mpembe, wakati
wa uzinduzi wa uhakiki wa wastaafu wanaolipwa pensheni zao na Wizara
hiyo katika Mikoa ya Lindi na Mtwara.
Alisema kuwa lengo la uhakiki huo ni
kuiwezesha Wizara kuhuisha taarifa za wastaafu ili kupata kanzidata
(database) iliyo sahihi, kuwatambua wastaafu na kuiwezesha serikali
kulipa wastaafu wanaostahili.
“Kwa kuwa zoezi hilo ni la lazima na kwa
wale wastaafu ambao hawajahakikiwa kwa sababu mbalimbali katika mikoa
ambayo uhakiki umekamilika watalazimika kufika katika ofisi za Hazina
katika mikoa husika na kujiandikisha na baada ya uhakiki kukamilika
wataelekezwa utaratibu utakaotumika kuwahakiki” aliongeza Bw. Mpembe
Aidha Bw. Mpembe alisisitiza wastaafu
hao kufika wenyewe na sio kutuma wawakilishi, wakiwa na nyaraka zote
muhimu zikiwemo barua ya tuzo la kustaafu, barua ya kustaafu au
kupunguzwa kazini, nakala ya hati ya malipo ya kiinua mgongo au mkupuo,
barua ya ajira ya kwanza, kitambulisho cha pensheni, barua ya
kuthibitishwa kazini, kadi ya benki na picha mbili ndogo zilizopigwa
hivi karibuni.
Akijibu kuhusu malalamiko ya pensheni
ndogo kwa wastaafu, Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali Msaidizi, Bw.
Stanslaus Mpembe, amesema kuwa watakapo kamilisha zoezi la uhakiki
wataandaa taarifa namna zoezi zima lilivyo endeshwa na kuiwasilisha kwa
uongozi wa juu wa Wizara, likiwemo suala hilo la malalamiko ya pensheni
ya wastaafu.
Kwa upande wa wastaafu kutoka taasisi
mbalimbali za Serikali wanaolipwa na Wizara ya Fedha na Mipango
wameiomba Serikali iwaongezee viwango vya pensheni wanavyo lipwa ili
waweze kujikimu kimaisha kutokana na hali ya maisha kuwa ngumu.
Akitoa maoni katika zoezi la uhakiki wa
wastaafu linaloendelea katika mkoa wa Lindi na Mtwara, Mstaafu David
Christopher Mtakula, amesema utaratibu wa kuhakiki taarifa za wastaafu
ni njia nzuri ili kujiridhisha kuwa wanaolipwa ndio wanaostahili.
Zoezi hili la uhakiki linaloendelea
katika mikoa ya Lindi na Mtwara lilianza Oktoba 20, 2016 katika mkoa wa
Pwani na limeshafanyika katika mikoa 23 ya Tanzania Bara ambayo ni
Mbeya, Iringa, Njombe, Ruvuma, Songwe, Katavi, Rukwa, Morogoro, Dodoma,
Singida, Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Tanga, Mwanza, Kagera, Mara,
Shinyanga, Simiyu, Geita, Kigoma na Tabora.
0 comments:
Post a Comment