Hussein Makame, NEC
Tume ya
Taifa ya Uchaguzi (NEC) imevitaka vyombo vya habari kuialika tume hiyo
iwapatie elimu ya mpiga kura ili kukuza uelewa wa vyombo hivyo juu ya
sheria, kanuni, na taratibu zinazoongoza uchaguzi na kufahamu majukumu
ya tume hiyo.
Wito huo
umetolewa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC Bw. Kailima Ramadhani wakati
akieleza tathmini yake juu ya elimu ya mpiga kura inayotolewa na tume
hiyo ofisini kwake jijini Dar es Salaam hivi karibuni.
Alisema
NEC imejipanga kutoa elimu ya mpiga kura nchi nzima na iko tayari
kupokea maombi ya kwenda kutoa elimu hiyo kwa wamiliki wa vyombo vya
habari, wahariri na wafanyakazi wote wa vyombo hivyo ili kukuza uelewa
wa sekta hiyo.
“Niwaombe
vyombo vya habari, tumeanzisha programu ya elimu ya mpiga kura
tualikeni kwenye vyombo vyenu vya habari, mtualike tuje tuzungumze na
nyinyi vyombo vya habari kimoja baada ya kingine” alisema Bw. Kailima na
kufafanua kuwa:
“Sisi
tunataka kuzungumza na wewe mmiliki wa chombo na watumishi wako na
viongozi wenzako wote ili tukueleweshe kuhusu Sheria ya Taifa ya
Uchaguzi na Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, utaratibu mzima wa
uchaguzi na uijue Tume ili unapoandika ujue ninachoandika si cha
kubahatisha”
Bw.
Kailima alisema elimu hiyo kwa vyombo vya habari pia itaviwezesha kuwa
na uelewa mpana juu ya masuala mbalimbali ya uchaguzi na kutoa
changamoto kwa mtendaji huyo wa NEC pindi anapopata na nafasi ya
kuzungumza nao.
Katika
kutekeleza mkakati endelevu wa kutoa elimu ya mpiga kura nchi nzima, Bw.
Kailima ameanza kutoa elimu hiyo kupitia televisheni mbalimbali nchini
na kwamba yuko tayari kuzungumza na vyombo mbalimbali kutekeleza mkakati
huo.
Kwa
upande mwingine, Bw. Kailima amewataka Watanzania wakisikia kuna
maonesho au mkutano ambapo Tume inashiriki wafike banda la NEC waulize
maswali wapate ufahamu na watapata uelewa mkubwa juu ya mchakato wa
uchaguzi.
Akizungumza
kwa nyakati tofauti, Bw. Kailima alisema NEC itahakikisha inatumia
maonesho, mikutano na mikusanyiko mbalimbali ikiwemo mikutano ya kidini
ili kutoa elimu ya mpiga kura ikiwemo shule za sekondari nchini.
Alisema
lengo kuu la kutekeleza hayo ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2020 wananchi
wawe wamepata uelewa wa kutoa kuhusu taratibu za uchaguzi na kufahamu
majukumu ya Tume ili kupunguza malalamiko na upotoshaji unaofanywa
katika kipindi cha uchaguzi.
Tayari
Bw. Kailima ameshatoa elimu ya mpiga kura kupitia televisheni za Shirika
la Utangazaji la Zanzibar (ZBC) na Televisheni ya Afrika Mashariki
(EATV) na amesema NEC inajipanga kutoa elimu hiyo kupitia vyombo vya
habari na mitandao ya kijamii.
0 comments:
Post a Comment