METDO Tanzania

METDO Tanzania

Thursday, October 20, 2016

SERIKALI YATOA TAMKO KWA WATUMISHI WA UMMA KUJITOKEZA KUSAJILIWA VITAMBULISHO VYA TAIFA KABLA YA OKTOBA 31, 2016

mwg1
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Mwigulu L. Nchemba (Mb) akizungumza wakati wa mkutano na vyombo vya habari mkoani Dodoma kuhusu mwenendo wa zoezi linaloendelea la usajili wa Vitambulisho vya Taifa kwa Watumishi wa Umma. Katikati ni Waziri wa Nchi, Ofisi  ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mh. Angellah J. Kairuki (Mb) na Bi. Rose Mdami, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Hifadhi Hati, akimwakilisha Kaimu Mkurugenzi Mkuu NIDA
mwg2
Katikati ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Mwigulu L. Nchemba (Mb) Akisisitiza jambo wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari kuhusu zoezi la kusajili watumishi wa Uma nchi nzima. kulia ni Waziri wa Nchi, Ofisi  ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mh. Angellah J. Kairuki (Mb) na kushoto ni Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Meja Jenerali Projest Rwegasira
mwg3
Baadhi ya waandishi wa Habari nchini wakisikiliza kwa makini ufafanuzi unaotolewa na Mawaziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na Ofisi  ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora; kuhusu usajili wa Vitambulisho vya Taifa kwa watumishi wa Umma zoezi linaloendelea nchi nzima
mwg4
Baadhi ya waandishi wa Habari walioshiriki mkutano wa tathmini ya mwenendo wa Usajili Vitambulisho vya Taifa kwa watumishi wa Umma; mkutano uliofanyika ukumbi wa Kambarage, jengo la Hazina Dodoma
mwg5
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Mwigulu L. Nchemba (Mb) akiweka saini kitabu cha wageni alipotembelea ofisi za Usajili za Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa mkoani Dodoma, kukagua shughuli za usajili Watumishi wa Umma kabla ya kuzungumza na waaandishi wa habari kutoa tathmini ya mwenendo wa zoezi hilo
mwg6
Waziri akipokea maelezo ya namna shughuli za usajili zinavyo ratibiwa na ofisi ya usajili Wilaya ya Dodoma Mjini ; alipofanya ziara ya ukaguzi na kukutana na viongozi na watumishi wa Umma waliofika kupata huduma.

Serikali imewataka watumishi wote nchini walioajiriwa na Serikali, yakiwemo mashirika ya Dini na Taasisi  nyingine ambazo haziko kwenye orodha ya malipo ya mishahara ya Serikali lakini zinapata ruzuku kutoka Serikalini; kuwa wamesajiliwa katika zoezi  la Vitambulisho vya Taifa kwa Watumishi wa Umma linaloendelea kote nchini, kufikia Oktoba 31, 2016.

Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi  ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mh. Angellah J. Kairuki (Mb) alipozungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma, katika mkutano wa pamoja ulioitishwa kati ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Waziri ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Bi Kairuki amesisitiza; “waajiri na watumishi watakaoshindwa kutekeleza zoezi hili watachukuliwa hatua stahiki kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zilizopo”

Akifungua mkutano huo uliolenga kutoa tathmini ya mwenendo  wa zoezi linaloendelea la Usajili wa Vitambulisho vya Taifa kwa Watumishi wa Umma lilioanza nchi nzima tangu Oktoba 03, 2016, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mh. Mwigulu L. Nchemba (Mb) amesema mpaka sasa Mamlaka ya  Vitambulisho vya Taifa (NIDA)  imefanikiwa kusajili zaidi ya asilimia 50% ya watumishi wote nchi nzima na baadhi ya mikoa kukamilisha usajili kwa zaidi ya asilimia 95%. Ameutaja mkoa wa Geita kuwa mkoa unaoongoza kwa kufanya vizuri katika zoezi hilo

Amesema pamoja na kuwepo kwa changamoto mbalimbali zilizokwamisha zoezi hilo kukamilika kwa wakati uliopangwa; Wizara yake kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, wameamua kuongeza muda wa kukamilisha zoezi hilo kwa wiki mbili zaidi hadi Oktoba 31, 2016.

Amewataka watumishi kuondokana na upotoshwaji unaofanywa na baadhi ya watumishi kwamba zoezi hilo limelenga kuhakiki vyeti na badala yake wajitokeze kwa wingi kusajiliwa kwani Serikali imelenga kuunganisha taarifa za mfumo wa mishahawa wa Serikali na NIDA, ili mbali na kutatua tatizo la watumishi hewa; kupitia mfumo huu wa kielektroniki unaomtambua mtu kwa alama zake za kibaiolojia kuwa na maslahi mapana kwa taifa na kwa watumishi; kwa kuunganisha mifumo mingine ya Serikali ukiwemo mfumo wa Kodi, mifuko ya Hifadhi za Jamii, Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, Bima ya Afya, Uhamiaji, RITA Na Benki ili kutoa manufaa mapana kwa mtumishi.

Amelipongeza Jeshi la Wananchi wa Tanzania kwa kuwezesha kusambazwa kwa vifaa vya usajili nchi nzima, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Taasisi na Mashirika yote ya Serikali waliojitoa kufanikisha zoezi la Usajili.

Kupitia zoezi la Usajili Watumishi wa Umma, Tayari NIDA imefungua ofisi za usajili nchi nzima, ngazi ya Wilaya kusogeza karibu zaidi huduma inayotolewa kwa wananchi. Kwa mujibu wa Waziri Mwigulu Pindi zoezi  la usajili watumishi litakapokamilika usajili wa wananchi utaanza mara moja nchi nzima kwani zoezi la usajili vitambulisho vya Taifa limelenga kila mwananchi, Mgeni anayeishi kihalali nchini na Mkimbizi.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com