Mamlaka
ya Mapato Tanzania (TRA) inapenda kuutaarifu umma kuwa, kwa mujibu wa
vifungu vya 8 na 16 vya Sheria ya Ushuru wa Bidhaa Sura ya 147,
wazalishaji wote wa bidhaa zinazotozwa Ushuru wa Bidhaa na wazalishaji
wa malighafi ya kutengenezea spiriti wanatakiwa kusajiliwa na kupewa
leseni na Kamishna Mkuu wa TRA kabla ya kuanza uzalishaji. Bidhaa
zinazotozwa Ushuru wa Bidhaa zimeainishwa katika jedwali la nne la
Sheria husika. Baadhi ya bidhaa hizo ni kama Bia, Sigara, Spiriti,
Mvinyo na Vinywaji baridi.
Masharti ya Leseni
Maombi
yote yatumwe kwa Kamishna Mkuu kwa kutumia fomu ya maombi ya leseni
inayopatikana katika ofisi za TRA au tovuti: www.tra.go.tz
Maombi tofauti yafanywe kama ifuatavyo:
Kwa kila
kiwanda ambacho kitatumika kuzalisha bidhaa. Leseni itatumika kwa
kiwanda kilichopewa leseni pekeeKwa kila aina ya bidhaa itakayozalishwa
na leseni itatumika kuzalisha bidhaa husika pekee.
Mmiliki
wa leseni hataruhusiwa kuhamisha umiliki wa leseni husika, kubadili
kiwanda au kuzalisha bidhaa tofauti katika kiwanda kilichopewa leseni
bila kufanya maombi na kuruhusiwa na Kamishna Mkuu.
Baada ya
kupewa leseni, mzalishaji anatakiwa kumjulisha Kamishna Mkuu juu ya
tarehe ya kuanza uzalishaji ndani ya siku 21 tangu uzalishaji huo
kuanza.
Pindi
bidhaa yoyote inapoamuliwa kwa mujibu wa Sheria ya Bunge kuanza kutozwa
Ushuru wa Bidhaa, mzalishaji wake anapaswa kumjulisha Kamishna Mkuu na
kuomba leseni ya uzalishaji ndani ya siku 21 baada ya bidhaa husika
kuanza kutozwa Ushuru wa Bidhaa.
Leseni ya uzalishaji itakwisha muda wake kila tarehe 31 Disemba ya mwaka ambapo mmiliki atatakiwa kuomba leseni mpya.
Wazalishaji
wa spiriti yenye vionjo na isiyo na vionjo (Denatured and Undenatured
Spirit) pia wanatakiwa kuomba leseni za uzalishaji kwa Kamishna Mkuu.
Uzalishaji
wa bidhaa zinazotozwa Ushuru wa Bidhaa bila ya leseni ni kosa
linalopelekea adhabu ya faini au kifungo au faini na kifungo ikiwa ni
pamoja na kutaifishwa kwa mitambo na bidhaa zote zilizohusika katika
utendaji wa kosa hili. Wazalishaji wote wanaaswa kumiliki leseni halali
katika wakati wote wa uzalishaji na TRA kwa kushirikiana na wadau
wengine wataendesha ukaguzi endelevu kuhakiki matakwa haya ya sheria.
Waombaji
wanatakiwa kufanya maombi katika ofisi yoyote ya TRA ambako viwanda
husika vinapatikana ili kuepuka adhabu kali zinazotokana na ukiukwaji wa
matakwa haya ya sheria.
“Pamoja Tunajenga Taifa Letu”
Limetolewa na:
Idara ya Huduma na Elimu kwa Mlipakodi
TRA-Makao Makuu
Dar es Salaam
0 comments:
Post a Comment