#Azma ya Serikali ni kufikisha Umeme kwa Kila mwananchi
Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Kapinga amewasihi Viongozi wa Vijiji, Kata na Vitongoji kuwahamasisha Wananchi kuweka umeme kwenye nyumba zao ili kutekeleza Azma ya Serikali ya kuhakikisha inafikisha Umeme kwa Wananchi wote Tanzania.
Mhe. Kapinga amesema hayo wakati akiwasha umeme kwa mara ya Kwanza katika Kijiji cha Ilambo Kata ya Ibumo wilayani Kilolo Mkoani Iringa, alipofanya ziara ya kukagua Maendeleo ya Utekelezaji wa Miradi ya Usambazaji Umeme Vijijini tarehe 15, 2023.
Amesema Serikali imekuwa ikitoa fedha nyingi kuhakikisha inatekeleza Miradi mbalimbali ya Maendeleo ikiwemo ile ya Kusambaza Umeme Vijijini ili kuwafikia wananchi wote.
"Viongozi wa Kata, Kijiji na Vitongoji ninyi mko na Wananchi muda wote pia ni daraja kati ya wananchi hao na Serikali kuu, hivyo ni vyema kuwahamasisha wananchi hao kuweka Umeme kwenye nyumba zao ambao wamefikiwa na huduma hiyo na wengine kuendelea kuandaa nyumba kwa kusuka nyaya ili kujiweka tayari kwa kuunganishwa na umeme pindi itakapofika katika maeneo yao; tunajua maendeleo ni hatua hivyo kila mmoja atafikiwa muhimu ni kujiweka tayari muda wote", alisisitiza Mhe. Kapinga.
Ameongeza kuwa Serikali inapenda kuona wananchi wake wanapiga hatua za maendeleo kupitia miradi wanayowapelekea, ni busara na vyema kuona miradi inayoitekeleza na kuwafikia wananchi inatumika kwa wananchi.
Amewaelekeza Shirika la Umeme Tanzania( TANESCO)na Wakala wa Nishati Vijiini(REA) kuhakikisha huduma ya Umeme inafika katika maeneo yote ili wananchi waifurahie na waone thamani ya miradi hiyo na fedha zinazotolewa na Serikali.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kilolo Peles Magili amewasisitiza wananchi kuendelea kutunza na kuilinda miundombinu ya Umeme ili iweze kutumika kwa muda mrefu.
Pia wananchi watoe taarifa kwa Mamlaka husika pindi wanapoona mtu yeyote anahujumu au kupanga njama ya kuiba ama kuharibu miundombinu hiyo kwa kuwa Serikali inatumia fedha nyingi kugharamia miundombinu hiyo.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment