METDO Tanzania

METDO Tanzania

Friday, December 15, 2023

TANZANIA YAIBUKA MSHINDI WA KWANZA MAONESHO YA JUAKALI YA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI


Na; Mwandishi Wetu - Bujumbura BURUNDI

Mjasiriamali kutoka Tanzania ameibuka mshindi wa kwanza wa jumla kwenye Maonesho ya 23 ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki maarufu kama Nguvu Kazi/Juakali yaliyomalizika jijini Bujumbura, Burundi leo tarehe 15 Desemba 2023.

Mshindi wa pili ametokea Kenya huku mshindi wa tatu akitokea Uganda.

Mjasiriamali huyo, Dkt. Herieth Mkanga anayejishughulisha na utengenezaji wa Batiki ameibuka mshindi kwa kutengeneza vazi maarufu la “Suti ya Samia” ikiashiria mtindo wa nguo unaopendelewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan. 

Akizungumza mara baada ya kupokea tuzo hiyo, Dkt. Mkanga amesema kuwa amefurahia ushindi huo ambao ni mkubwa kwake na kwa Tanzania na kwamba tuzo hiyo ni chachu kwake ya kuendelea kujituma zaidi na kutengeneza bidhaa nyingi na  zenye ubora ili kulikamata soko la Afrika Mashariki, Afrika na Duniani kwa ujumla.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Ukuzaji Ajira, Bi. Kissa Kilindu amewahamasisha wajasiriamali kote nchini kujiamini na kuchangamkia fursa mbalimbali za biashara, masoko na uwekezaji zinazotangazwa na Serikali ndani na nje ya nchi.

Wakati huohuo, Wajasiriamali wawili wenye ulemavu wa macho kutoka Zanzibar, Bw. Abdul Kadir Amini Ahmed na Bw. Khamis Khamis Haji wanaojishughulisha na utenegenezaji wa mikeka wamepongezwa na waandaji wa maonesho hayo kwa kufanikiwa kushiriki maonesho hayo kikamilifu licha ya hali ya ulemavu waliyo nayo huku jamii ikitakiwa kuiga mfano wao wa kujituma katika kazi badala ya kutegemea kuomba kusaidiwa.


Maonesho ya 23 ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo yamebeba Kaulimbiu isemayo “Kuunganisha Wajasiriamali Wadogo na wa Kati wa Afrika Mashariki kufanya biashara katika Eneo la Afrika Mashariki” hufanyika kila mwaka kwa utaratibu wa mzunguko kutoka nchi moja kwenda nchi nyingine ambapo maonesho ya 24 yanatarajiwa kufanyika nchini Sudan Kusini mwaka 2024.

MWISHO
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com