METDO Tanzania

METDO Tanzania

Thursday, September 29, 2022

SERIKALI, WADAU WAONGEZA KASI KUDHIBITI KICHAA CHA MBWA


NA MWANDISHI WETU

KICHAA cha mbwa ni ugonjwa unaosababishwa na virusi vya kichaa cha mbwa ambavyo huathiri wanyama wote hususan mbwa na binadamu. Ugonjwa huu hauna tiba bali unakingwa kwa chanjo na kuzingatia ufugaji bora wa mbwa.


Kichaa cha mbwa huambukizwa kwa njia ya kung’atwa na mbwa mwenye ugonjwa, lakini pia binadamu anaweza kuambukizwa kwa kugusa mate ya mbwa mwenye kichaa.


Siku ya kichaa cha mbwa duniani huadhimishwa Septemba 28 ya kila mwaka ikiwa ni kumbukumbu ya siku aliyofariki mgunduzi wa chanjo ya ugonjwa huo.


Hapa nchini, serikali na wadau wa ustawi wa wanyama wanashiriki katika kuadhimisha siku hiyo  kwa kutekeleza uchanjwaji wa mbwa katika maeneo mbalimbali.


Mwaka huu, kauli mbiu iliyoongoza maadhimisho haya duniani inasema “Kichaa cha mbwa, afya moja, vifo sifuri” ikiwa na lengo la kutokomeza vifo vinavyosababishwa na ugonjwa wa kichaa cha mbwa.


Wadau wa ustawi wa wanyama ambao ni shirika lisilo la kiserikali linalojihusisha katika ustawi wa wanyama nchini, Education for African Animals Welfare (EAAW) na Meru animals Welfare (MAWO) wameshiriki katika kuiunga serikali mkono kwenye mapambano dhidi ya ugonjwa wa kichaa cha mbwa.


Akizungumza kwa niaba ya wadau hao, Mkurugenzi wa EAAW, Ayubu Nnko, anasema kwa muda mrefu wamekuwa wakishirikiana na Wilaya ya Mkalama mkoani Singida kwa kutoa chanjo ya kichaa cha mbwa na matibabu huku MAWO wakihudumia Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara.


Nnko anaeleza kuwa mwaka huu walizindua maadhimisho hayo Septemba 23 mwaka huu katika vijiji vya Yulansoni na Msingi, Kata ya Kinyangiri, Wilaya ya Mkalama, ambapo mpaka sasa zaidi ya mbwa 518 na paka 29 wamekwishapatiwa chanjo huku shughuli hiyo itaendelea hadi Oktoba mbili mwaka huu kwa kuhusisha vjiji vya Nduguti na Maziliga.


Kwa upande wa Simanjiro, MAWO wameweza kuendesha shughuli hiyo katika vijiji vya Naisinya, Naepo, Mererani, Shambarai na Orkesmet.


Akizungumza katika uzinduzi wa maadhimisho hayo wilayani Mkalama katika Kijiji cha Yulansoni, Daktari wa mifugo wilayani hapo, Elias Mbwambo, alilishukuru  EAAW akisema kuwa shirika hilo limekuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya kichaa cha mbwa.


Daktari huyo anaitaka jamii kutoa ushirikiano pale wanapoletewa chanjo kwa kuhakikisha wanashiriki ipasavyo katika matunzo ya mbwa na paka ili kuepusha madhara.


Mbwambo anaeleza kuwa mbwa wamekuwa wakifugwa na binadamu tangu ustaarabu ulipoanza kwa malengo mbalimbali yakiwemo ulinzi, kuchunga mifugo na uwindaji ambapo kwa Tanzania zaidi ya asilimia 98 ya mbwa wanaofugwa ni wa asili na mbwa wachache ni wa kisasa ambao hufugwa zaidi maeneo ya mjini.


Anasisitiza kuwa mbwa kama mifugo wengine wanatakiwa kupatiwa huduma zote za msingi kama chakula, maji, matibabu, malazi na kuogeshwa kwa dawa za kuua wadudu na kwa mujibu wa sharia za nchini, mbwa hatakiwi kuachwa akitembea mitaani.


Anawatahadharisha wafugaji kuhakikisha mbwa wanafungwa katika banda au mnyororo muda wote wa mchana na kwa mbwa wanaotumika kwa kazi za kuchunga mifugo au kuwinda, ni vyema wakawa chini ya uangalizi wa mwenye mbwa ili wasidhuru watu wengine.


Pia, anasisitiza kuwa ni vyema mbwa akapatiwa mafunzo ya msingi ili aweze kutii amri ya anaemmiliki kama njia ya kuepusha madhara


Ni dhahiri kuwa kuna madhara mbalimbali yanayosababishwa kwa kutokuzingatia ufugaji bora wa mbwa ambayo ni kung’ata na kujeruhi watu au mifugo, kusababisha hofu, kuwa tishio kwa jamii, kueneza magonjwa kama vile kichaa cha mbwa na tegu wa mbwa.


Dalili za ugonjwa wa kichaa cha mbwa ni mbwa kubadilika tabia, kuwa mkali au mpole kuliko ilivyo kawaida, kushindwa kula, kukwepa maji na kupooza miguu ya nyuma.


Viashiria vingine vya ugonjwa huo ni mbwa kudondosha mate mengi na ulimi kuning’inia nje ya mdomo, kubweka mara kwa mara akitoa mlio usio wa kawaida.


Kwa upande wake, Mkurugenzi wa EAAW, Nnko, anasema kuna umuhimu jamii hasa kwa maeneo ya vijijini kushirikishwa kwa kiasi kikubwa katika tafiti na uenezwaji wa elimu kuhusu matunzo ya wanyama, kwani kwa kufanya hivyo itakuwa rahisi kwa serikali na wadau kutatua matatizo yanayowakabili wananchi na sekta ya mifugo.


Aliviomba vyombo vya habari kushiriki zaidi katika kutangaza shughuli zinazofanywa na serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuendeleza sekta ya mifugo, ustawi wa wanyama na jamii.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com