**********
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amezitaka benki zilizoko kwenye mikoa inayolima
pamba zihakikishe kuwa kesho Jumapili zinatoa huduma kwa wateja ili
wanunuzi wa pamba wakamilishe taratibu za mikopo.
“Kesho
mabenki yanayotoa huduma Jumapili ni vema yafanye kazi, ili wanunuzi wa
pamba waje wakamilishe taratibu zote za makaratasi na Jumatatu wapate
hela ya kuanzia kazi. Hata mkifunga saa 6 mchana, wao wabakie hadi saa
10 ili mradi wakamilishe taratibu zote,” amesema.
Ametoa wito huo leo mchana (Jumamosi, Agosti 3, 2019) wakati akizungumza na Wakuu wa Mikoa nane inayolima pamba ya Mara,
Mwanza, Simiyu, Geita, Kagera, Shinyanga, Singida na Tabora pamoja na
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Pamba na Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB.
Waziri
Mkuu amesema kikao kilichofanyika jana (Ijumaa, Agosti 2, 2019) baina
ya Benki Kuu, wanunuzi wa pamba na wamiliki wa mabenki kimeafiki kuanza
kutoa mikopo kwa wanunuzi ili waanze kununua pamba kuanzia keshokutwa
(Jumatatu, Agosti 4, 2019).
Amesema
kazi ya kununua pamba ikianza, ilipwe kwanza iliyokusanywa ili ianze
kusombwa na iweze kupisha nafasi kwa pamba mpya itakayoendelea
kununuliwa na kupelekwa kwenye maghala.
Amemtaka
pia Mwenyekiti wa Wanunuzi, Bw. Christopher Gachuma ahakikishe anaweka
ufuatiliaji ili kujua kujua ni kiasi gani cha pamba kimenunuliwa kutoka
kwa nani na wapi. “Endeleeni na uratibu wa ununuzi mjue nani amenunua
nini, wapi na kwa gharama ipi.”
Pia
amewataka wataalamu wa Wizara wa Kilimo waende mikoani, watu wa mabenki
na Benki Kuu washirikiane na taasisi ambata kama Bodi ya Pamba, Tume ya
Ushirika na AMCOS ziratibu vizuri kila mwananchi anayepeleka pamba na
wahakikishe analipwa.
Wakati
huohuo, Waziri Mkuu amewataka wanunuzi wa pamba na wafanyabiashara wote
wajenge viwanda hapa nchini ili kupata suluhisho la kudumu la soko la
pamba. “Natoa wito kwa wafanyabiashara nchini wajenge viwanda vya
kusokota nyuzi na kutengeneza nguo.
Amesema
hivi sasa nchini, kuna viwanda viwili tu vya kusokota nyuzi ambapo
kimoja kiko Dar es Salaam na kingine kiko Shinyanga ambavyo uwezo wake
ni mdogo. “Leo tumenunua pamba lakini tutaanza kupata changamoto ya
usafirishaji wa kuipelekea nje ya nchi kuiuza. Tukiwa na viwanda hapa
ndani, tatizo la soko halitakuwepo.”
Kwa
upande wake, Mwenyekiti wa Wamiliki wa Mabenki, Bw. Abdulmajjid
Nsekela, aliwahakikishia wakuu wa mikoa yote na wanunuzi waliokuwa
wakishiriki mkutano huo kutoka kwenye mikoa yao kwamba fedha itapatikana
kuanzia Jumatatu (keshokutwa).
“Napenda
kuwahakikishia kuwa kwenye kikao cha jana, benki zote zimeridhia kwamba
zitatoa mikopo kwa wanunuzi. Tulikubaliana kwamba wanunzi wote
walioomba mikopo waje haraka kuchukua fedha zao, waliopata lakini wakawa
hawajachukua mikopo waje pia kuchukua.
“Mabenki
yako tayari kutoa fedha hizo, na tutasimamia ili kuhakikisha fedha
zinatolewa kwa wakati na wanunuzi wanapata hela,” alisema mbele ya
Waziri Mkuu.
Naye
Mwenyekiti wa Wanunuzi wa Pamba, Bw. Christopher Gachuma alisema
wanunuzi wako tayari kununua pamba ili itoke mikononi mwa wakulima iende
kwa ginners (wenye vinu vya kuchambua pamba.
“Kuanzia
wiki ijayo, tutajitahidi kununua pamba kwa haraka na kwenye maeneo
yasiyo na wanunuzi tutakutana na kujipanga ili tuwafiie wote. Ila kwenye
mikoa ya pembezoni kama Katavi, ambako hakuna ginneries, tunaomba upendeleo maalum sababu ya umbali uliopo.”
Naye
Waziri wa Kilimo, Bw. Japhet Hasunga amesisitiza kuwa wanunuzi
wanaoenda kununua pamba wilaya za Meatu, Igunga na Singida wawe makini
na wapeleke kwenye ginneries maalum za kuchambua mbegu na siyo za
kusindika mafuta.
Katika
hatua nyingine, Waziri wa Nchi (OR-TAMISEMI), Bw. Selemani Jafo
ameiomba Benki Kuu ya Tanzania (BoT) isimamie kwa karibu makubaliano ya
kikao cha jana ili utekelezaji wake uende kwa haraka zaidi.
“Ningeshauri
Mwenyekiti wa Wanunuzi afuatilie wafanyabiashara wake, ili wakipata
hiyo fedha, waende wakatimize malengo yaliyokusudiwa. Na Wakuu wa Mikoa
mkutane na wanunuzi wa mikoa yenu kila baada ya siku mbili, ili muweze
kubaini kwa haraka changamoto zinazowapata na kuzisuluhisha kwa haraka,”
alisema.
0 comments:
Post a Comment