METDO Tanzania

METDO Tanzania

Friday, May 27, 2022

DUNIA YAUNGANA KUDHIBITI UFUGAJI KUKU KATIKA VIZIMBA, YASISITIZA UFUGAJI HURIA KWA USTAWI WA KUKU



NA MWANDISHI WETU

KATIKA kipindi cha mwaka 2020 hadi 2022, kumekuwepo makubaliano ya kisera ya kukomesha ukatili dhidi ya kuku na kitiwa saini zaidi ya mashirika 500 duniani ambapo Bara la Afrika yapo mashirika 15 ambayo yamekubali ukomeshaji wa ukatili dhidi ya kuku.

Aidha, zaidi ya mashirika 2,300 ya chakula dunia yamepitisha sera za ustawi wa kuku ambazo huondoa vizimba vinavyotumika kufuga kuku wanaotaga mayai ambapo kampuni 982 zimekamilisha kwa ufanisi ufugaji kuku wa mayai matumizi ya vizimba vya betri.

Hadi kufikia Aprili 2022, asilimia 88 ya kampuni zilizotoa ahadi ya matumizi ya mayai ambayo hutagwa na kwa kutumia ufugaji huria wa kuku, zimetimizwa matakwa hayo.

Ili kuhakikisha mkakati huo unafikiwa, Mei 16, 2022 Shirika linalotetea haki za wanyama Open Wing Alliance (OWA) ilizindua ripoti ya ufugaji huru ya mwaka 2022.

Ripoti hiyo ya pili iligusia uzalishaji mayai yatokanayo na ufugaji huria wa kuku ambapo ripoti hiyo inatoa fursa kwa kila kundi na umma kuelewa kwamba kampuni nyingi zinatimiza ahadi zao za ustawi wa wanyama, lakini kuna baadhi ya kampuni ambazo zinarudi nyuma linapokuja suala la maendeleo, uwazi katika haki za wanyama.

Muungano wa The Open Wing Alliance duniani, umekuwa ukifanya kazi bila kuchoka kuhakikisha kunakomeshwa matumizi ya kikatili ya kuwafungia kuku wanaotaga mayai kisha kuingizwa katika mfumo wa chakula hasa viwandani.

Muungano huo unahusisha zaidi ya mashirika 80 kutoka nchi 63 ambayo yamekuwa yakifanya kazi kwa zaidi ya muongo mmoja ili kupata ahadi ya kukomesha ukatili dhidi ya kuku kutoka kwa kampuni kubwa zaidi za chakula duniani.

Tanzania nayo haiko nyuma katika mapambano dhidi ya ukatili wa wanyama, kwani OWA imekuwa ikishirikiana na mashirika mbalimbali ya ustawi wa wanyama.

Miongoni mwa mashirika hayo ni shirika la Education for African Animals Welfare (EAAW) katika kutekeleza shughuli zake hususan utoaji wa elimu na kampeni zinazolenga kukomesha ukatili dhidi ya wanyama hasa kuku waliofungiwa kwenye vizimba.

Akizungumzia mkakati wa kutokomeza ukatili dhidi ya kuku, Mkurugenzi wa OWA, Alexandria Beck, anasema kuendelea kupata ahadi nyingi katika kutekeleza sera ya ustawi wa wanyama, ni kiashirio muhimu cha maendeleo kwa wanyama wanaofugwa kwa ajili ya chakula.

“Ingawa tunajua kwamba ahadi pekee hazitasababisha kuboreshwa kwa hali za wanyama. Ili kuwaokoa kuku kutokana na maisha ya ukatili ya kufungiwa kwenye vizimba vya chuma, tunahitaji kuona kampuni zinatengeneza na kutoa taarifa kuhusu maendeleo kuelekea malengo yao ya ufugaji huria,” anaeleza.

Beck anasema takwimu zinaonyesha kwamba siku zijazo hakutakuwa na ufugaji wa vizimba na zaidi ya asilimia 11 ya kuku duniani, hawafugwi katika vizimba.

Yapo baadhi ya mashirika ambayo yana sera ya kuondoa matumizi ya vizimba katika kufikia asilimia 100 ya mayai yatokanayo na kuku wasiofugwa kwenye vizimba, bado hawajaweka wazi hadharani maendeleo yao ya hatua iliyofikiwa katika maeneo yao.

Miongoni mwa kampuni hizo ni Hilton Hotels, Radisson Hotels Group na Unilever. Hata hivyo, barani Afrika kuna mashirika yaliyofikia na kutimiza ahadi ya uondoaji vizimba katika ufugaji wa kuku, ambayo ni Danone, Marriott, Starbucks na Kraft Heinz ambayo yanaripoti kwa uwazi hatua zilizofikiwa.

Mapema mwaka huu, kampuni ya kimataifa ya Majid Al Futtaim ambao ni wauzaji wakubwa wa mazao ya kuku kupitia maduka ya Carrefour nchini Kenya, Kameruni, Uganda na Misri walitoa ahadi ya kutekeleza sera ya kimataifa yakutofungamana na wauzaji mayai ya kuku wanaofugwa katika vizimba.

Majid Al Futtaim ilionyesga namna ambavyo watumiaji wa mayai wanavyojali ustawi wa wanyama. Hata hivyo bado kuna changamoto kwa ustawi wa kuku katika ukanda wa Afrika, kwani zipo kampuni zimekuwa zikisuasua kukubaliana na sera ya uondoaji vizimba kwa kuku wa mayai wanaofugwa.

Pia, wauzaji wa mayai kwa reja reja kama vile Pick n Pay, Shoprite na Massmart, wanahitaji kujitolea zaidi kwa kusisitiza ufugaji kuku bila vizimba ili kudhihirisha kwa umma kwamba wanajali ustawi wa wanyama hususan kuku.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com