Na ACT- WAZALENDO, RUVUMA
CHAMA cha ACT wazalendo kupitia kwa katibu wake Ado Shaibu kimedhamilia kufanya mchakato wa kukusanya
maoni ya wananchama wake kuhusu tume huru ya uchaguzi ikiwa ni maelekezo ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Chama hicho .
Akizungumza na viongozi wa ACT
Wazalendo katika Jimbo la Nyasa Mkoani Ruvuma katika mwendelezo wa ziara yake
kwenye mikoa ya Ruvuma, Selous, Mtwara, Lindi, Pwani na Tanga yenye lengo la
ujenzi wa Chama, kuhamasisha na kufanya harambee ya michango ya wanachama ya
kugharamia Mkutano Mkuu wa Chama wa tarehe 29 Januari 2022 na kufafanua mageuzi
ya uendeshaji Chama kisayansi Ado shaibu amesema kuwa ofisi ya mwanansheria
mkuu wa chama imeagiza kukusanya maoni kwa wanachama wake.
"Kwenye kikao cha Wadau wa
Siasa Juu ya Hali ya Demokrasia nchini kilichofanyika Dodoma, suala la Tume
Huru ya Uchaguzi liliafikiwa na pande zote. Kwetu sisi ACT Wazalendo, hatua
inayofuata ni mjadala wa kitaifa kuhusu aina ya Tume Huru tunayoihitaji"
alisema Katibu Mkuu, Ado Shaibu.
Katibu Mkuu huyo wa ACT wazalendo amesema vikao vya chama (ACT Wazalendo Kamati Kuu ya mwezi Juni
na Halmashauri Kuu ya mwezi Oktoba 2021) vimeagiza Chama kulipa kipaumbele
suala la Tume Huru ya Uchaguzi.
Ameongeza kuwa mbali na maoni ya
wanachama, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa ACT Wazalendo imeagizwa kufanya rejea
ya uzoefu wa nchi nyingine zenye mifano ya Tume za Uchaguzi zinazopigiwa mfano
pamoja na Ripoti na Taarifa mbalimbali ikiwemo Rasimu ya Tume ya Jaji Warioba.
Ndugu Ado amewaeleza viongozi wa
Chama jimboni Nyasa kuwa Chama kitaendelea kulipa kipaumbele suala la Tume Huru
ya Uchaguzi ili chaguzi za mwaka 2024 (Serikali za Mitaa) na 2025 (Uchaguzi
Mkuu) ziwe huru, za haki na zenye kuaminika.
Katibu Mkuu anaendelea na ziara
yake mkoani Ruvuma na leo atakuwa jimbo la Songea Mjini.
0 comments:
Post a Comment