*Ni
wale wanaotaka kununua pamba
BENKI mbalimbali nchini zimewahakikishia
wafanyabiashara wa zao la pamba kuwa zina fedha za kutosha kuweza kuwakopesha
ili wanunue pamba yote itakayozalishwa katika msimu wa mwaka huu nchini.
Pia viongozi wa benki hizo wamesema wako tayari
kusaidia katika uwekezaji wa miundombinu ya aina yeyote ama eneo litakalohitaji
mkopo wa fedha ili kufanikisha mchakato wa ununuzi wa pamba katika msimu huu
ikiwa ni pamoja na kusaidia ujenzi wa maghala.
Hayo yamesemwa leo (Jumatano, Februari 21, 2018) na
viongozi wa benki mbalimbali nchini katika mkutano ulioitishwa na Waziri Mkuu
Kassim Majaliwa uliowahusisha wafanyabiashara wote wa pamba , Wakuu wa Mikoa
,Viongozi wa Halmashauri na wadau wote.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti viongozi wa benki za
NMB, CRDB, TIB, EXIM, AZANIA, Mkombozi, Bank of Africa, Equity na Eco
waliwahakikishia wafanyabiasha hao mbele ya Waziri Mkuu kwamba wana fedha za
kutosha na wako tayari kuwapa mikopo ili wakanunue pamba mara msimu
utakapoanza.
Akizungumza katika mkutano huo, Waziri Mkuu amewataka
wanunuzi wa zao hilo kuandikisha katika ofisi ya Mkurugenzi wa Bodi ya Pamba
kiasi cha pamba wanachohitaji kununua pamoja na maeneo ambayo wanatamani kwenda
kununua.
Waziri Mkuu amesema suala hilo litaiwezesha
bodi kufahamu idadi ya wafanyabiashara watakaonunua pamba pamoja na kiasi
wanachohitaji na eneo husika. “Serikali itaendelea kusimamia zao hilo
kikamilifu.”
Amesema kwa sasa wanauhakika kuwa
pamba yote itanunuliwa kwa sababu benki zimewathibitishia kwamba ziko tayari
kuwakopesha wafanyabiasha, hivyo wadau wote watambue kuwa Serikali
itashirikiana nao hadi katika hatua za mwisho za ununuzi.
Waziri Mkuu aliwahakikishia
wafanyabiashara hao kwamba maombi waliyoyatoa kuhusu uboreshaji wa mauzo ya zao
hilo yatayafanyiwa kazi na Serikali itaendelea kusimamia zao hilo ili ununuzi
wake uwe rahisi.
Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo, Dkt. Charles
Tizeba amesema wamejipanga kikamilifu katika kudhibiti ubora wa pamba, ambapo
amewataka viongozi wa maghala wasipokee pamba chafu.
Pia amewataka wakulima wa pamba
wasithubutu kuchanganya na maji, mawe au mchanga kwa sababu wataharibu soko.
Serikali itapambana na watu wote wakaothubutu kuharibu zao hilo kwa kcuhukua
hatua kali za kisheria kwani huo ni uhujumu uchumi.
Aliendelea kusema kuwa uamuzi wa
Serikali kusimamia ongezeko la uzalishaji wa zao la pamba unakwenda sambamba na
mazao mengine makuu ya biashara ambayo ni korosho, chai, tumbaku, kahawa na
mahindi kwa upande wa chakula.
Dkt. Tizeba amesema inatazamiwa kuwa
ifikapo 2021 mchango wa mazao katika pato la Taifa unakadiriwa kufikia sh.
trilioni 13.6, ambapo yataliwezesha Taifa kuvuka mstari wa kiwango cha
umasikini.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt.
Philip Mpango amesema kuwa zao la pamba lina mchango mkubwa katika kukuza
uchumi, hivyo watahakikisha zao hilo linaendelea kukua.
Dkt. Mpango amezitaka benki zichukue
tahadhari kwa mikopo chechefu hivyo wajiridhishe kama wakopaji wote
wanatumia mikopo hiyo kwa mujibu wa makusudio.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATANO, FEBRUARI 21, 2018.
0 comments:
Post a Comment