Na WAMJW, DODOMA
Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsi, Wazee na Watoto Dkt.Dorothy Gwajima ameongoza kikao cha wataalamu
wa afya hapa nchini wakiwemo Madakitari Bingwa,Waganga Wakuu wa Mikoa,Wilaya na
Hospitali zote kikihusisha kamati ya kitaifa ya kufuatilia vifo vya wazazi
vinavyotokea kila siku kwa ajili ya kujadili na kuchambua taarifa za vifo
vilivyotokea tarehe 20 hadi 21/12/2021 kutokana na sababu za uzazi.
Kikao hicho kilichofanyika kwa
njia ya mtandao wa TEHAMA ambapo Dkt Gwajima amekiongoza ikiwa ni sehemu ya
mkakati wa Wizara ya Afya kuhakikisha kila kifo cha mzazi na mtoto mchanga kinafanyiwa tathimini ya kitaifa ndani ya saa
24.
Kufuatia kikao hicho Mojawapo ya
vituo vilivyoripoti vifo kwa siku ya leo ni pamoja na Zahanati ya Songambele,
Halmashauri ya Buhigwe Mkoa wa Kigoma ambapo Dkt. Gwajima amempongeza Muuguzi
Nyanduni Joachim na timu yake kwa kupigania maisha ya mzazi ambaye alichelewa
kufika kituoni waliweza kuokoa maisha ya mtoto na mama yasipotee akiwa kwenye
huduma.
Dkt. Gwajima ametoa wito kwa
wananchi kuhakikisha wanasikiliza ushauri wa wataalamu wa sekta ya Afya ili
wawahi kufika kwenye vituo vya kutoa huduma kwa wakati hali itakayotoa fursa
kwa wataalamu kuweza kutumia taaluma zao kuokoa maisha.
Amesema wizara ya Afya
imeimarisha ufuatiliaji wake kwa msaada wa TEHAMA ili kufikia kila kituo cha
kutoa huduma za Afya, hivyo wananchi wasiwe na wasiwasi na huduma zinazotolewa
pia watoe ushirikiano wa taarifa kwa wakati ili kama kuna uzembe wowote ambao
haujabainika uweze kuibuliwa na kuzuiwa.
Amesema, vifo vya wazazi na
watoto wachanga havikubaliki na kwa kila kifo uchambuzi utafanyika mubashara
ili kujiridhisha kuwa ilikuwa kinaepukika au hapana na kama juhudi zote stahiki
zilifanyika kwa wakati ili mapitio ya vifo yataonyesha kuimarishwa ili kuweza
kufikia vifo vyote nje ya vya uzazi na watoto wachanga.
Dkt. Gwajima ametoa wito kwa
wananchi kutoa ushirikiano wao wa taarifa za kuridhika au kutoridhika kwa
huduma kupitia namba za viongozi wa ngazi ya kituo, halmashauri, na mkoa
zilizobandikwa kwenye mbao za matangazo ya kituo pia wanaweza kuwasilisha moja
kwa moja wizarani kwenye namba 199 (namba ya kupiga) au 0734124191 namba ya
Waziri wa Afya Dkt.Gwajima 0734124191 kwa kutuma ujumbe tu)
Kwa upande wake Dkt. Ahmad
Makuwani, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya akina mama akiungana na mabingwa
wengine kwenye kutoka hospitali mbalimbali za rufaa za mikoa na kanda pamoja na
hospitali za halmashauri, vituo vya afya na zahanati amemuhakikishia Waziri
kuwa ataratibu usimamizi endelevu wa mkakati huu ambao umeonesha kuwa na tija
kwa ajili ya kuhakikisha zoezi hili ni ndelevu na lenye tija kwenye kuleta
mshikamano wa kitaaluma wa kuboresha uwajibikaji kwenye utoaji huduma na
kupunguza au kuondoa kabisa vifo hasa vile ambavyo vinaepukika.
Kikao hicho kilichoanza tangu
tarehe 20/12/2021 kitakuwa kinafanyika kila siku na kuongozwa na wataalamu
wabobezi kwa lengo la kufikia kila kituo ambako kifo kimetokea na kufanya
uchambuzi wenye kuibua mazuri, mapungufu na kuelimisha sambamba na kuchukua
hatua stahiki iwapo itabainika kuna uzembe
0 comments:
Post a Comment